by Admin | 12 May 2020 08:46 pm05
Lipo tukio ambalo, wengi wetu tunalijua lihusulo yule kijana aliyepagawa na mapepo, ambapo tunaona baba yake alimchukua na kumpeleka kwa mitume wa Yesu, lakini walishindwa kulitoa lile pepo, lakini baadaye kidogo walipomwona Bwana anashuka milimani, baba yake yule kijana alimkimbilia Bwana, na kumwambia nisaidie mwanangu, nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumtoa..
Ndipo Bwana Yesu akawaambia wamlete kwake, sasa alipofika tu kwake, mambo yalikuwa nje ya matarajio ya watu wengi waliokuwepo mahali pale.. Embu tusome tena Pamoja Habari hiyo kwa utaratibu, lipo jambo jipya naamini tutalipata mwisho wa Habari hiyo.
Marko 9:17 “Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu;
18 na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze.
19 Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu.
20 Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu.
21 Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto.
22 Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia.
23 Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.
24 Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.
25 Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena.
26 Akalia, AKAMTIA KIFAFA SANA, akamtoka; naye AKAWA KAMA AMEKUFA; hata wengi wakasema, Amekufa.
27 Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama”
Kama tunavyoona ule mstari wa 26 anasema, pepo yule akalia, halafu akamtia kifafa sana, Neno “sana” sio kitendo cha kawaida, ukitaka kujua si kitendo cha kawaida utaona kwa mahangaiko yake mtoto yule na kelele zake kuliwasababisha mpaka watu waliokuwa mbali wasogee karibu, wakisema kuna nini pale? Wakawa wanakuja kwa kasi..wengine walidhani pengine mtu anaungua moto, au kapewa sumu,..pengine baba yake yule kijana akafikiri mbona sasa hali hii ndio imekuwa mbaya Zaidi kuliko mwanzo..wale watu wengine wakafikiri na wao, afadhali alivyokuwa mwanzo, huyu mtu ndio kaharibu kabisa mambo, hali yake imekithiri zaidi..
Tengeneza picha, Na kibaya Zaidi ni kitendo kilichofuata cha yule kijana kutulia baada ya muda mfupi, akawa hapepesi midomo tena kama mtu mwenye kifafa anavyofanya siku zote, wala macho, wala haonekani kama anapumua, alikuwa kimya.. Unadhani jambo gani lingefuata kwa wale watu waliokuwa pale..Ni wazi kama tunavyosoma Habari walisema..Kijana AMESHAKUFA huyu..
wengine pengine wakakimbia saa hiyo hiyo wakisema hii ishakuwa kesi sasa, wengine pengine walianza kudondosha machozi..n.k.
Lakini ule upande wa pili Je! Bwana Yesu muda wote huo alikuwa anafanya nini?
Jibu ni alikuwa anaangalia uponyaji wa Mungu unavyofanya kazi ndani ya yule kijana.. alitulia kimya mpaka pale alipoona kazi ya Mungu imekamilika ndani ya yule kijana,…. Na ghafla tu wakati watu wanaendelea kufikiria tufanye nini?, Wanamwona Bwana anakwenda kumshika kijana mkono na kumnyanyua..
Alivyonyanyuka hakunyanyuka kama mgonjwa mwenye maruwe ruwe, hakunyanyuka kwa kuyumba yumba kama mtu ambaye hajapona vizuri, bali alinyanyuka kama vile mtu aliyeamka usingizini, asubuhi, akiwa fresh, akiona tabasamu zuri la Kristo likiyatazama macho yake.. Kijana akijiona mwepesi, mtulivu, kama vile sio yeye, na tangu huo wakati akawa mzima kabisa..
Sasa ni kwanini Kristo achague, njia kama ile kumponya yule kijana? Na sio zile zilizozoeleka kwamba anafika tu anamgusa mtu na saa hiyo hiyo anapona bila mateso yoyote wala mahangaiko kama yale..
Ni kuonyesha kuwa Kristo anavyowaponya watu wengine Roho zao kwa namna hiyo hiyo pasipo wao kujijua.. Kuna wakati mtu atamwomba Mungu niponye roho yangu..Niponye shida zangu, niponye vifungo vyangu, niponye magonjwa yangu.. Lakini baada ya kuomba vile mambo ndio yanakuwa tofauti, hali ndio inakuwa mbaya Zaidi kinyume na matarajio yake,.. mwingine ni mgonjwa, ugonjwa wake unaonekana kama ndio unazidi, mwingine ana mapepo, maroho hayo ndio yanaonekana kama yanazidi..wala usiogope maadamu ulishamwomba Kristo juu ya uponyaji wako, ujue kuwa hayo maroho yameshakutana na Kristo mwenyewe, hivyo ndio yanavyoungua ndani yako kwa Neno lake..na wakati si mwingi yatatoweka moja kwa moja.
Huo ugonjwa unaokusumbua muda mrefu, umemwomba Kristo akuponye, ameshakusikia na ameshakuponya, lakini hizo dalili za ugonjwa zinazoonekana kama zinazidi, zisikutishe, wakati utafika utaondoka kabisa..usiogope maneno au hisia za wanaokuzunguka, wamekukatia tamaa kiasi gani Kumbuka yule kijana alifikia hatua ya kuonekana amekufa kabisa..hana tumaini tena, lakini ghafla alishikwa mkono na kunyanyuliwa juu na Kristo..Ni nani anayeweza kufa mbele ya Kristo?..yeye ndiye UFUFUO NA UZIMA!
Hivyo na wewe maadamu umemkabidhi Kristo shida yako ujue kuwa hutakufa nayo..Utakufa na nyingi lakini sio hiyo, unachopaswa kufanya ni kuamini Tu.. Basi hicho tu, amini kuwa Kristo amekusikia na atameshakuponya…Lakini hakikisha upo ndani ya Kristo kwanza.
Vilevile katika roho, ukimwomba Kristo akuvushe katika daraja lingine, usishangae kuonekana na watu umekufa kabisa kiuelekeo machoni pa watu..Hiyo ni kawaida..Hivyo uwe tayari kwa hilo pia..kwasababu ni sharti aondoe yote yasiyofaa ndani yako, na ndipo alete mapya ndani yako, kwa Kristo ni lazima upoteze ndipo upate, usipokuwa tayari kufanya hivyo, ni huwezi kuvushwa hatua nyingine..Kwahiyo hilo nalo uwe nalo tayari.
Bwana akubariki sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAP
Mada Nyinginezo:
Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..
Je ni kweli huwezi kuijua karama yako mpaka uwekewe mikono na wazee?
CHUKIZO LA UHARIBIFU
MPINGA-KRISTO
USIMWOGOPE YEZEBELI.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/05/12/fahamu-jinsi-kristo-anavyoponya-watu-roho/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.