DAKIKA MOJA TU, INAKUFANYA UMWAMINI SHETANI?

by Admin | 12 June 2020 08:46 pm06

Luka 4:5 “ Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu KWA DAKIKA MOJA.

6 Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo”.

Hilo ni moja ya jaribu shetani alilomletea Bwana kule jangwani..

Lakini jiulize ni kwa nini iwe kwa dakika moja?, kwanini amwonyeshe ndani ya muda mfupi kiasi hicho, kwani alikuwa na haraka gani? Chukulia mfano mtu aje na kukwambia nataka kukuonyesha plani ya mji wetu na shughuli zote zinazofanyika ndani yake kwenye CD..Ni wazi kuwa hawezi kumaliza kukuonyesha kila kitu kwa dakika moja, itachukua dakika nyingi sana kama sio masaa, lakini tunaona hapa kwa ibilisi iliwezekana..

Alifanikiwa kumuonyesha Bwana milki zote za ulimwenguni kwa kitendo cha dakika moja..Ni kwanini afanye hivyo? Sio kwamba alikuwa hawezi kumwonyesha milki zote kidogo kidogo, huo uwezo alikuwa nao lakini sikuzote ni desturi yake, kutompa nafasi mtu ya kutafakari vizuri kazi zake..

Hakutaka Bwana atafakari nyuma ya milki zile kuna nini? Bali alikuwa anamwonyesha haraka haraka, ule upande mzuri tu wa fahari hizo, ili kusudi kwamba Bwana achukue maamuzi ya haraka haraka ya kumsujudia bila hata kutafakari vema, ili awe amemshinda. Hakumwonyesha Bwana wagonjwa waliolala hoi mahospitalini waliokuwa wanahitaji msaada, hakumwonyesha watu waliofungwa kwa kuonewa, au wanaotumikishwa na nguvu za giza, hakumwonyesha maskini wa roho, wala mayatima ambao wazazi wao waliuawa na huyo huyo shetani, hakumwonyesha uchawi uliokithiri katika hiyo miji n.k ..yeye alimwonyesha tu mali, na fahari..Lakini hakumweza Bwana kwasababu pale alikutana na Mkuu wa Uzima mwenyewe ambaye anajua vyema kuzipambanua roho!.

Hii ni mbinu ambayo shetani anaitumia hata sasa kuwaangusha wengi katika dhambi..kwamfano akitaka leo kummaliza mtu na dhambi ya uasherati, mara moja atamletea katika mawazo yake uzuri wa kufanya lile jambo..Lakini hatamruhusu kutafakari ni nini kipo nyuma yake, na yeye bila kutafakari vyema, moja kwa moja ataingia humo, kuitenda, hajui kuwa nyuma yake kuna hata hatari hata ya kifo hata kupata ukimwi, nyuma yake kuna mimba zisizotarajiwa, nyuma yake kuna kupata aibu, na kibaya Zaidi kuliko vyote ni kuwa nyuma yake kuna laana itokayo kwa Mungu..

Au mwingine shetani anamletea mawazo ya kuwa Tajiri kwa dakika moja, atamwambia njoo utapata utajiri wa haraka, bila kufikiri vema kuwa akienda kule, atakutana na waganga wa kienyeji waliolaaniwa, hajui kuwa nyuma yake kuna kutoa kafara, kuna uchawi, kuna kutumikishwa, na mwisho wake ni kifo, na baada ya hapo ni ziwa la moto..au anakutana na kazi ya wizi au utapeli, pasipo kutafakari nyuma yake kuna kifo, au kifungo, mtu anaingia huko…..Sasa yeye kwasababu kaonyeshwa pesa tu za haraka haraka ambazo hazihitaji kuzihangaikia sana, anaingia humo na kupotelea humo..

Mwingine, anakutana tu na kazi Fulani ya ghafla, halafu baada ya hapo anashurutishwa akaifanye, lakini yeye badala achukue muda kumwomba Mungu na kuichunguza kazi ile, moja kwa moja atakwenda kuingia nayo mkataba na kuifanya kisa tu imemuahidia mshahara mzuri, hajui kuwa kazi ile ililetwa na shetani, ili kuharibu utaratibu wake aliokuwa nao wa kusali, wa kumtumikia Mungu, na kibaya Zaidi anakuja kugundua kazi yenyewe inafanya shughuli za kipepo kama uuzaji pombe, au bidhaa haramu na mambo mengine ya ajabu.

Mwingine atakuwa anatembea madukani, ghafla anakutana na simu ya mtu imejiegesha mahali ambapo haionekani, na saa hiyo hiyo shetani anaanza kumletea mawazo ya dakika moja ya wizi, kumwonyesha faida za simu ile akienda kuuza atapata laki kadhaa, ndani ya dakika chache baadaye..kisha atanunua hiki na kile.. Na yeye bila kuruhusu fikra zake kuwaza mbali anakwenda kuiiba, bila kujua nyuma yake, kuna kupigwa na watu, kuna kuchomwa moto, kuna kufungwa, na kibaya Zaidi kuna laana ya Mungu, kwamba hata kama hatakufa pale siku ya mwisho atakwenda motoni..

Mithali 13:11 “Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa”.

Mwingine kamwona mwanamke na hapo hapo kamtamani, bila kupata muda mrefu wa kumchunguza tabia zake, yeye wazo la dakika moja tu, anaingia humo, na ndio hapo baadaye anakuja kugundua alikuwa ni mke wa mtu aliyemwacha mume wake, au kahaba tu, na ghafla matatizo ndani ya nyumba yanaanza. Vivyo hivyo na mwanamke naye, shetani atampitishia dakika moja mwanaume mwenye fedha, na yeye bila kujitafakarisha anaingia moja kwa moja, kumbe ndio kaenda kuharibu Maisha yake moja kwa moja.

Na sehemu nyingine nyingi za Maisha ni vivyo hivyo..Shetani huwa anawaletea watu mawazo ya chap-chap ..Ya dakika moja tu yanayovutia lakini nyuma yake yana miaka mingi ya majuto.

Ndugu, tusiwe wateja wa shetani..biblia inasema..

1Yohana 2:15 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, TAMAA YA MWILI, NA TAMAA YA MACHO, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.

17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele”.

Zingatia hilo, ni moja kati ya majaribu makuu 3 ya ibilisi aliyoyaona yanawazomba watu wengi kwake, na ndio maana akamchagulia na Bwana, hivyo hatashindwa kutuletea na sisi (mimi na wewe), hivyo tuwe makini sana na mambo ya humu ulimwenguni

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO

MTAIFAHAMU KWELI NAYO HIYO KWELI ITAWAWEKA HURU.

Kati ya Unyakuo,dhiki kuu, utawala wa miaka 1000 kipi kinaanza

MOTO HUFA KWA KUKOSA KUNI.HATA UASHERATI NAO

NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/12/dakika-moja-tu-inakufanya-umwamini-shetani/