by Admin | 12 June 2020 08:46 pm06
Isaya 66:15 “Maana Bwana atakuja na moto, na magari yake ya vita kama upepo wa kisulisuli; ili atoe malipo ya ghadhabu yake kwa moto uwakao, na maonyo yake kwa miali ya moto.
16 Kwa maana Bwana atateta na wote wenye mwili, kwa moto na kwa upanga wake; nao watakaouawa na Bwana watakuwa wengi’.
Bwana Yesu atakaporudi mara ya pili, yaani siku ile mbingu zitakapofunguka na kila jicho kumwona hatarudi tena kwa upole kama alivyokuja hapo mwanzo, biblia inatuambia atakuja na jina jipya..Siku hiyo hataitwa tena YESU, Jina linalomaanisha mwokozi, hapana kwasababu hatakuja tena kuokoa, bali atakuja na jina jipya ambalo kwasasa bado halijafunuliwa..
Jina hilo litakuwa ni la kifalme, la kimamlaka, lenye uweza na ukuu mwingi sana..Watu watakamwona siku hiyo duniani hatawaamini kuwa huyu ndiye Yule tuliyekuwa tunamsikia habari zake, akihubiriwa na watu dhaifu…Kwasababu hatakuwa vile tena..
Siku hiyo wale watakaomwona, hakuna atakayesaliwa na nguvu hata kidogo, kwasababu wataingiwa na hofu kubwa, wataomboleza kusivyokuwa kwa kawaida, na ndio maana tunapaswa tusiichezee hii neema kabisa, kwasababu haitakuwa hivi siku zote.
Mtu mmoja nilikuwa ninamweleza habari za hukumu ya mwisho, na jinsi watu waovu watakavyoangamizwa, akaniambia ninamhukumu…Nikamuuliza nimekuhukumu wapi?..Akanipa lile andiko la Yule mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, ambaye Yesu aliwaambia wale watu waliomleta kwake, kuwa asiyekuwa na dhambi awe wa kwanza kumtupia Yule mawe…Nikamwambia ni kweli mimi sitakutupia mawe lakini Kristo siku ile atakutupia mawe wewe..na utakufa, kama usipotubu sasa.
Najua unaweza kuuliza ni wapi Kristo anaua..
Soma hapa..
Ufunuo 2:22 “Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;
23 NAMI NITAWAUA WATOTO WAKE KWA MAUTI. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake”.
Hayo ni maneno yaliyotoka katika kinywa cha Kristo mwenyewe!. ATAWAUA WAOVU..Na kama vile yale maandiko pale juu yanavyotuambia..watakaouliwa hawatakuwa wachache bali ni wengi sana..
Ndugu, kikombe cha ghadhabu ya Mungu kinakaribia kujaa, (kama hujui vizuri kasome kitabu cha Ufunuo 16) Unyakuo ukishapita yatakayofuata si mambo mazuri!, ni mambo mabaya ambayo laiti ungeonyeshwa leo, usingetamana hata adui yako awepo hicho kipindi, Kwasababu siku atakaposhuka, jua litazimwa lote, na nyota na mwezi vitaondoshwa, duniani kutakuwa giza tororo, kutakuwa na tetemeko kubwa ambalo halijawahi kutokea tangu dunia iumbwe, na baada ya yeye kushuka wale ambao watakuwa bado hai atawaua mara moja..Hakuna huruma!.
Ufunuo 19:11 “Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.
12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.
13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.
15 NA UPANGA MKALI HUTOKA KINYWANI MWAKE ILI AWAPIGE MATAIFA KWA HUO. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.
16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA Bwana WA Mabwana………..
20 Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti;
21 na wale waliosalia waliuawa kwa upanga wake yeye aliyeketi juu ya yule farasi, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.”.
Bado tu unayapenda maisha ya dhambi? Bado tu unazidi kutazama pornografia, unafanya uasherati, unakula rushwa, unakwenda Disko, unaiba, unatembea na waume/wake za watu?…
Usilisahau hili Neno.. “WATAKAUAWA NA BWANA WATAKUWA NI WENGI”
Ni heri tumkimbilie yeye maadamu bado anaokoa sasa, Kabla Bwana hajaondoka Mtume Yohana alikuwa anaegemea kifuani kwake alikuwa anadeka kama mtoto karibu na Bwana, lakini Yohana huyo huyo anamwona Bwana Yesu Yule Yule kwenye maono Patmo kama miale ya moto, anatisha sana mpaka anaanguka chini ya miguu yake kwa hofu…Hivyo wakati wa neema ukiisha, Kristo hatakuwa Yule tunayemjua sasa…hivyo Bwana atusaidie neema hii tuithamini sana.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/12/nao-watakaouawa-na-bwana-watakuwa-wengi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.