MALEZI YA MTOTO MCHANGA.

MALEZI YA MTOTO MCHANGA.

Yafahamu malezi ya mtoto mchanga kibiblia.


Ukitaka mtoto wako mchanga awe na afya na ukuaji bora, na baadaye aishi Maisha aliyokusudiwa na Mungu ya mafanikio rohoni..Basi ni vema ukatafuta ushauri wa kiblia, ili ujue ni jinsi gani unapaswa umlee mwanao tangu akiwa katika hatua za awali za uchanga wake.

TUKIANZANA NA MALEZI  YA KIMWILI:

Embu tukiangazie kisa kimoja katika biblia, naomba usome chote, na mwisho wa Habari hiyo utajifunza jambo kubwa sana ambalo pengine hata hukuwahi kulitafakari hapo kabla..Ni tukio linalomuhusu Sulemani na wanawake wale wawili makahaba.

Tusome..

1Wafalme 3:16 Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake.  17 Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani.  18 Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu.  19 Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia. 20 Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu.  21 Nilipoondoka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe? Amekufa. Hata asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa.  22 Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.  23 Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu.  24 Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme.  25 Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu.  26 Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe.  27 Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake.  28 Na Israeli wote wakapata habari za hukumu ile aliyoihukumu mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.

Katika Habari hiyo nataka utazame  mambo makuu matatu..

 1. Jambo la kwanza: Jinsi ya uwekaji mtoto.
 2. Jambo la Pili: Utazamaji wa mtoto.
 3. Jambo la Tatu: Unyonyeshaji.

Tukianzana na hilo la kwanza: Utaona mwanamke yule mwerevu, alikuwa kila alipolala alikiweka kichanga chake Ubavuni. Ikiwa na maana alijitahidi kwa kadiri awezavyo kulala chali, ili mtoto apate nafasi ya kumwegemea yeye aidha ubavuni pake au kifuani pake, na sio yeye amwegemee mtoto,..Lakini yule mwingine hakulijali hilo, alimgeuza mtoto kuwa godoro, akamlalia..Na matokeo yake yakawa ni kifo.

 • Zingatia: Unapozaa mtoto, hakikisha mwanao muda wote yupo ubavuni pako.. Hakikisha Unamjali wakati wote, hata ule wakati ambao hujalala, mweke mgongoni mwako, usimwache kizembe zembe bila kumwangalia hiyo  itakuwa ni kwa usalama wa mwanao.

Pili: Kama yule mwanamke angekuwa “hamchunguzi/hamdadisi” sana mtoto wake: Basi angeibiwa mwanawe bila habari. Lakini yeye tangu siku ya kwanza alikuwa anamkagua hadi kufikia siku ya tatu tayari alikuwa ameshamjua mwanawe ndani nje..,!, alijua umbile la mwanawe, na alama zake,..Hata pale alipojaribu tu kuchanganyiwa mtoto alilimtambua hilo mara moja.

 • Zingatia: Je! Wewe umeshamjua mtoto wako wote ndani ya siku tatu za kwanza? Kiasi kwamba wakiwekwa katikati ya  vichanga 1000 utaweza kumtaumbua mwanao? . Fanya hivyo kwasababu Hiyo itakusaidia pia kugundua tatizo ikiwa litampata mwanao kwa haraka.Lakini ikiwa wewe upo buzy tu, na mambo yako, humwangalii mtoto wako.Unamwachia msaidizi wako akufanyie kila kitu Ujue lipo jambo litamwiba mwanao, na wewe usijue chochote. Akiumizwa wewe hutajua, akiugua wewe hutajua chochote n.k.

Malalamiko mengi, ya wazazi, kuhusu Watoto wao kudhalilishwa kijinsia yanatokana na wazazi kutokuwa na tabia ya kuwachunguza Watoto wao, wanakuja kugundua  hali imeshakuwa mbaya sana hairekebishiki. Anza kujijengea tabia hiyo ni kwa heri yako na kwa usalama wa kichanga chako.

Tatu: wanawake wale walikuwa ni wanyonyeshaji wa maziwa yao wenyewe ya asili kwa vichanga vyao na sio ya ng’ombe.

 • Zingatia: Ukiishia kumpa mtoto wako mchanga maziwa ya makopo, kwa kuogopa kuharibika maumbile yako basi ujue upendo wake utahamia kule kwa Wanyama. Fanya hivyo ikiwa tu hakuna jinsi, labda mtoto kagoma kunyonya, au mama maziwa hayatoki, au pana matatizo mengine  ya kiafya lakini vinginevyo mnyonyeshe mwanao maziwa yako mwenyewe kwa afya bora wa mwili wake, na kinga zake, hata madaktari wanashauri hivyo.

KWA UPANDE WA MALEZI YA KIROHO.

Sasa ili mtoto wako mchanga awe na ulinzi wa ki-Mungu maishani mwake..Mchukue ukamweke wakfu mbele za Mungu. Hakikisha pia huendi mikono mitupu, ambatanisha na sadaka yako ya shukurani kwa Mungu kwa kile alichokupa/alichowapa.

Ipo mifano mingi ya kimaandiko ya wanawake wenye akili walipeleka Watoto wao wapeleka mbele za Bwana wabarikiwe, na mpaka leo tunaona Watoto hao jinsi walivyokuwa nguzo muhimu katika Imani, Ukimsoma Samweli, yeye hakuwa vile hivi hivi tu, bali ni baada ya mama yake kumpeleka mbele za Bwana (Soma Samweli 1&2).

Ukimsoma Yohana Mbatizaji naye vivyo hivyo,. Ukimsoma pia Bwana wetu Yesu Kristo naye vivyo hivyo, wote walipelekwa mbele za Bwana. Vivyo hivyo mchukue mwanao, mpeleke nyumbani kwa Bwana awekwe wakfu kwa Bwana kwa kuwekewa mikono na wachungaji au wazee wa kanisa..Hiyo itakuwa ni salama ya Maisha ya baadaye ya mwanao.(Luka 2:22-24).

Huhitaji kusubiri mpaka awe mkubwa, siku za mwanzoni mwanzoni, au wiki za mwanzoni haraka bila kukawia mpeleke kwa Bwana..Kumbuka mtoto mchanga habatizwi kulingana na maandiko, Hivyo usifanye hivyo kwasababu haitasaidia chochote. Mpeleke akawekewe mikono tu awe wakfu kwa Bwana.

Na hili ndio jambo kuu kuliko yote ya kuzingatia. Unaweza ukaijali afya yake, lakini kama Mungu hamtambui ni kazi bure.Kwasababu shetani ndiye atakayemtambua.

Vilevile ni jukumu lako kumwombea mwanao kila wakati, Tenga muda maalimu wa kumwombea, walau lisaa 1 kila kipindi. Mwombee afya yake, mwombee ukuaji wake, mwombee kila pembe ambayo Mungu atakuongoza. Vilevile unapomwimbia Mungu imba Pamoja naye,  Na hiyo ndio dalili nzuri upendo Mungu anaotaka mazazi aonyeshe kwa vichanga vyao.

Hivyo kwa kuhitimisha zingatia hayo mambo makuu 5.

 1. Muweke ubavuni mwako  daima.
 2. Mjue mtoto wako.
 3. Mnyonyeshe maziwa yako mwenyewe.
 4. Kamweke wakfu kwa Mungu.
 5. Mwombee.

Lakini kumbuka pia yote hayo ili yawe na maana ni lazima na wewe kama mzazi/wazazi, muwe mmemkabidhi Kristo Maisha yenu (yaani muwe mmeokoka). Hizi ni nyakati za mwisho na za hatari sana kama ulikuwa hujui, Pale Bwana Yesu aliposema..

Mathayo 24:19  “Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! 20  Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. 21  Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe”.

Jiulize ni kwanini alisema, ole kwa wanyonyeshao kama wewe?..Alisema hivyo kwasababu alijua mwisho ukiwakuta watu wa namna kama ya kwako, wakati huo utakuwa ni mgumu sana kwao..Embu jiweke  katika mazingira kama hayo halafu usikie YESU karudi kulinyakua kanisa..Umebaki hapa duniani , halafu mpinga-Kristo anaanza kuchinja watu utakuwa katika hali gani na mwanao.

Angalia magonjwa yanayotokea duniani ya ajabu (covid-19), angalia, majanga, angalia matetemeko makubwa, mauaji ya ajabu na ya kinyama, angalia tetesi za vita vya ki-atomiki na kuibuka kwa manabii wa uongo..Hapo hatuwezi kusema tuna vizazi vingine mbele vya kuishi, pengine mimi na wewe tutashuhudia tukio zima la Unyakuo..Sasa utakuwa wapi ikiwa leo hii hujaokoka ndugu yangu..

Lakini ukitubu sasa, Kristo yupo tayari kukusamehe, unachopaswa kufanya ni kumaanisha tu, kutoka katika moyo wako, na kusema kuanzia leo mimi ninaacha dhambi ninamgeukia..Na wakati huu huu Kristo ataanza kufanya kazi ndani ya Maisha yako, Hivyo kama upo tayari kufanya hivyo leo.

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ubarikiwe sana

Mada Nyinginezo:

KILEMBA CHA NEEMA, JE! UMEMVIKA MWANAO?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments