NI WAKATI WA KUJIPIMA, WEWE KAMA MTUMISHI WA MUNGU!

NI WAKATI WA KUJIPIMA, WEWE KAMA MTUMISHI WA MUNGU!

Fuatilia kisa hii,

Binti mmoja akiwa bado mdogo wa miaka 9 aliwauliza wazazi wake, Je! Wazazi wangu Niishi maisha gani ili nifanikiwe,

Wazazi wake wakamwambia, mwenetu, wewe huihtaji kwenda shule kupata elimu, wala huna haja ya kujua jambo lingine lolote kwa wakati huu wewe tafuta pesa kwa namna yoyote ile utakayoona ni rahisi, ukishazipata basi maisha yako yatakuwa sawa..

Ndipo Yule msichana akalizingatia hilo akaendelea kukua, hakujali elimu yoyote ya maisha mpaka alipofikisha umri wa miaka 12 akajiingiza mtaani, Na kule mtaani alikutana na makahaba wakamshawishi ajiingize katika shughuli kama za kwao za kujiuza, atapata fedha kirahisi..Ndipo Yule msichana kwasababu alishauriwa hivyo hivyo pia na wazazi wake, akaona ni ushauri mzuri na yeye pia akajiingiza kwenye biashara hiyo na kweli akaanza kupata fedha, na alipowaletea wazazi wake fedha zile, na kuwaeleza jinsi alivyozipata, basi wale wazazi wake, hawakumuonya kwa lolote japo walijua madhara ya vitendo vile, wakamwacha aendelee, ili awe anawaletea fedha nyingine nyumbani..

Na Yule binti aliendelea kuifanya ile kazi kwa bidii kwasababu aliwaonea huruma pia wazazi wake wasije wakaishi maisha ya shida,..aliendelea hivyo kwa miaka, mpaka akabobea katika hiyo kazi, Na kila mwisho wa mwezi anawapelekea wazazi wake fedha nyingi sana..

Lakini siku moja alianza kuumwa ghafla , hali yake ikabadilika sana, wazazi wake walivyoona vile walijua kabisa mwanao kwa dalili zile lazima atakuwa amesha athirika, lakini kwa hofu hawakumshauri akapime afya yake, bali walimfariji tu, wakimwambia hiyo itakuwa ni hali ya magonjwa ya kawaida tu, uwe unakunywa pain-killer hali itakuwa sawa…endelea tu kutafuta fedha mwenetu..(wakisema hivyo kuogopwa binti asije kujua akaacha hiyo kazi ya kuwaletea fedha).

Lakini Yule binti hali yake ilipozidi kuwa mbaya, mpaka akawa hawezi hata kutembea, ikabidi yeye mwenyewe siku moja, ajiamulie kwenda hospitali kupima, na alipopima afya yake,akagundulika kuwa ana virusi vya ukimwi..

Baada ya hapo akaanza kulia sana, akajutia maisha yake,akitazama na umri wake, ingawa mwenyewe mwenyewe tu alishasikia sikia kuhusu gonjwa hilo lakini hakulitilia maanani sana, kama angelisikia kutoka kwa wazazi wake waliomzaa…akaenda kuwaeleza wazazi wake, akiwahadithia sababu zilizomfanya apate ugonjwa ule, alizoelezwa na daktari, ndipo Akawauliza wazazi wake, kama je walijua kazi ile ingeweza kumletea madhara makubwa kama yale huko mbeleni.. ndio walikiri waziwazi ndio tulijua kuwa utaathirika, lakini tuliogopa kukwambia..Mtoto akasema nyie kama wazazi ulikuwa ni wajibu wenu kunionya mimi kama mtoto madhara yake kwani mimi nilikuwa ni bado sijajitambua, mmesubiri mpaka mimi mwenyewe nimejigundua mpaka dakika hii hali imekuwa mbaya,..Je! ni kweli mlikuwa mnanipenda au mlikuwa mnanitumia tu?

Habari hiyo inatufundisha nini?

Tukiona mpaka leo hii, Mkuu wa nchi anatangaza watu WATUBU DHAMBI ZAO, kwasababu wamemkosea Mungu, na wananchi pia wanafanya hivyo..Halafu sisi tunaojiita ni manabii na mitume, na watumishi, na waalimu hatukuwahi kuwaonya watu kabla ya mambo haya, kuwa ni sababu ya dhambi zetu, mpaka wamegundua wao wenyewe..basi tujue tuna dhambi kubwa mbele za Mungu..

Watu wasiomjua Mungu leo hii wanagundua tatizo, ni nini?.. kuwa ni DHAMBI lakini sisi, miaka nenda rudi, tunawahubiria tu injili za mafanikio, na huku tunajua dhambi bado ipo mioyoni mwao, tunawahubiria amani tu, hatuwaonyi dhambi zao, kisa tunaogopa hawataleta zaka, hawataleta sadaka…Ni nani aliyekuambia utumishi wa Mungu ni zaka tu na sadaka?.

Tujue kuwa watu wanapokwenda kumtafuta Mungu, wanamaanisha kweli kutafuta uzima wa nafsi zao, lakini wewe unapowaelekeza kwenye biashara, na mafanikio, na mwisho wa siku wanagundua kuwa hayawezi kutatua matatizo yao..Wanakuonaje wewe nabii, au mtume au mwalimu?

Hutaki kuwaonya watu kuwa hii dunia inakwenda kuisha na siku si nyingi unyakuo utapita na mpinga-Kristo atanyanyuka, na ataleta dhiki kubwa duniani ambayo hajiwahi kutokea kwa watu ambao watakuwa wameachwa,..kinyume chake sisi tunawahubiria mwaka huu watakwenda China kufanya biashara, na watashusha makontena, watabarikiwa..Hayo makontena wanayokwenda kushusha China mwaka huu yako wapi?.

Hatuwahubirii kuwa yapo mapigo ya vitasa saba, ambayo Mungu atayaleta juu ya dunia nzima kipindi sio kirefu kwa wale wote wasiomcha Mungu, kiasi kwamba magonjwa haya tunayoyaona leo hii, yatakuwa si kitu kulinganisha na hayo yanayokuja huko mbeleni..Ili watu watu watubu leo waache dhambi,tupone!..lakini sisi Tupo busy kuwatabiria tu majumba na magari. Ni nani aliyekuambia mioyo yao ipo kwenye magari na majumba?

Hutaki kujua hali za watu rohoni kuwa mtu akifa leo kama hajaokoka, atakwenda kuzimu, matokeo yake tuwasisitize watengeneze mambo yao na Mungu hata ikitokea wamekufa ghafla, basi wanakuwa upande salama, upo bize, kuanzia mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka, kuwatabiria mema, angali wapo bado katika dhambi. (Mbaya zaidi ni kwamba tunaujua ukweli lakini hatutaki kuwaambia watu). Tafakari ingekuwa ni dada yako wa damu, au ndugu yako..

Na wewe pia unayehubiriwa jiulize, Kristo akirudi leo, utakuwa katika upande upi? Usiridhishwe tu na mahubiri ya vichekesho, na burudani, ndugu ijali roho yako, siku hizi ni za mwisho. Haya tuyaonayo sasa ni mwanzo wa utungu tu…Yanakuja mengine makubwa zaidi na ya kutisha kuliko haya biblia imeshatabiri.

Lakini wakati unafika, ambao Mungu ataleta hukumu juu ya manabii wote wa Uongo, na Watumishi wote, wanaolitumia jina la Mungu isivyopasa..wakati huo unafika, nao upo karibu sana..

Yeremia 23:14 “Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, HUTIA NGUVU MIKONO YA WATENDAO MAOVU, HATA IKAWA HAPANA MTU AREJEAYE NA KUUACHA UOVU WAKE; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.

15 Basi Bwana wa majeshi asema hivi, katika habari ya manabii, TAZAMA, NITAWALISHA PAKANGA, nitawanywesha maji ya uchungu; kwa kuwa kutoka kwa manabii hao wa Yerusalemu kukufuru kumeingia katika nchi yote”.

Siku zote tujifunze kuiogopa ghadhabu ya Mungu na tujiepushe nayo na wengine pia.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

WAKAMTUKANA MUNGU, WALA HAWAKUTUBU.

JINSI NEEMA YA MUNGU ILIVYOKUWA KUBWA KWA MKE WA LUTU.

Chapa zake Yesu ni zipi hizo?

EWE MKE! HESHIMA YAKO IPO KWA WAKWE ZAKO.

ANGALIA UZURI WAKO, USIGEUKE KUWA KITANZI CHAKO.

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

Kwanini yule mtu afe kwa kuliwa na simba?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments