PALE UNAPOKUWA NA SABABU ZA KUMLAUMU MTU, UFANYE NINI?

by Admin | 19 June 2020 08:46 pm06

Ni mara chache sana inatokea mtu anakosana na mwingine bila sababu yoyote, (Hiyo mara nyingi huwa inatokea kutokana na wivu), Lakini kutokuelewana kwingi au kuchukiana na watu, au kutokusameheana, au kukosana na watu mara nyingi huwa kunatokana na sababu Fulani..Kwamfano utakuta mtu amemdhulumu mwenzake, tukio hilo linamfanya yule aliyedhulumiwa amchukie yule mdhulumuji, au mtu amemuua ndugu yake, hilo linamfanya ndugu ya mfiwa amchukie yule muuaji..Au pengine amemtukana, au amemdhalilisha kwa namna moja au nyingine, au amemsengenya, au amempiga n.k…Hizo zote ni “sababu” zinazoweza kumfanya mtu asimpende yule mwingine..

Zinaweza zikawa ni sababu za msingi kabisa ambazo hata ukifa mbele za Mungu, unaoujasiri wa kumwambia Mungu ni kwanini ninamlaumu mtu yule, ni kwasababu alikuwa ni muuaji, ni fisadi, ni mchawi n.k.

Lakini Je biblia inatufundisha nini tunapojikuta katika mazingira kama hayo?

Inasema..

Wakolosai 3:12 “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,

13 mkichukuliana, na kusameheana, MTU AKIWA NA SABABU YA KUMLAUMU MWENZAKE; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.

14 Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.

15 Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani”.

Soma tena huo mstari wa 13 Unasema.. “Mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake”.. unaweza ukawa na sababu zote za msingi za kumlaumu mzazi wako kwanini hakukupeleka shule wakati ulikuwa na uwezo, unazo sababu za msingi za kuwalaumu viongozi wako, au waalimu wako kwanini hawakuwajibika kutimiza wajibu wao.. Lakini biblia inasema…Kama Bwana alivyotusamehe sisi, vivyo hivyo na sisi tuwasamehe wao.

Mtu mwingine anaweza kusema mtu Fulani nilimsaidia hiki na kile, lakini baadaye alipokuwa hana shida, alianza kunizungumzia maneno mabaya kwa watu wengine akiniita mimi mchawi.. Hivyo maisha yangu kamwe sitakaa nimpende yule mtu, Ni kweli unazosababu zote za kufanya hivyo, kwa hali ya kibinadamu sababu zote zipo za kumwekea kinyongo..Lakini Mungu anatuambia Pamoja na sababu zetu, tunapaswa tuwasamehe kama vile Bwana alivyotusamehe sisi.

Tukijua kuwa Mungu naye anazosababu za kutosha za kutuhukumu na sisi, kwa mambo yote maovu tunayomtendea kila siku, lakini anatusamehe tu bure, Matusi tuliyokuwa tunatukana yalimtosha kutuhukumu na kututupa kuzimu, dhambi tulizozifanya zinatosha kumpa Mungu sababu za kutushusha Jehanum.

Na ndio maana anatuambia tena mahali pengine..

Luka 6:37 “…. msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa”.

Unaona? Zipo faida nyingi za kusamehe(kuachilia), na faida mojawapo ambayo ni kubwa, ni kwamba utasikia mzigo mzito umedondoka moyoni mwako, na utaona amani ya ajabu imemwagika ndani yako.Lakini ukibakia na vinyongo, ujue kuwa Mungu naye atakuwekea kinyongo.

Hatuna budi kujifunza hili kila wakati, kwasababu maisha ya humu ulimwenguni yamejaa makwazo ya kila namna, kama hutakutana nalo leo, basi utakutana nalo kesho.. Hivyo na sisi tukiruhu makwazo yatawale mioyo yetu, kwa kutokuwasamehe wale ambao wanatuudhi, au kutukera kwa makusudi, tujue kuwa tuna dalili kubwa ya kutoiona mbingu.

Hivyo tujifunze kusamehe, na kuachilia hata kama tunazo sababu zote za kufanya hivyo.

Mwisho kabisa soma kisa hiki na Bwana akubariki.

Mathayo 18:23 “Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.

24 Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi.

25 Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni.

26 Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

27 Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.

28 Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho.

29 Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

30 Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni.

31 Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka.

32 Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi;

33 nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe?

34 Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote.

35 Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake”.

Bwana akabariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

NGUVU YA MSAMAHA

Kwanini Bwana Yesu, aliruhusu yale mapepo yawaingie nguruwe?

 

KUMBUKUMBU LA DHAMBI.

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/19/pale-unapokuwa-na-sababu-za-kumlaumu-mtu-ufanye-nini/