UFALME WAKO UJE.

by Admin | 26 June 2020 08:46 pm06

Shalom,

Bwana Yesu alituambia tusalipo tuseme hivi..

Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, UFALME WAKO UJE,..

Ni kweli, tunajua kuwa siku moja ufalme wake utakuja duniani..Lakini upande wa pili wa shilingi yaani sisi tunaousubiria ufalme huo unadhani tungepaswa tuwe katika hali gani?..Nadhani ulishawahi kujikuta katika hali ya kumsubiria mtu au kitu mahali Fulani halafu kwa bahati mbaya kikachelewa/akachelewa kidogo, ile hali unatakayokuwa nayo wakati ule bila shaka si ya kawaida, dakika tano tu utaziona kama ni lisaa limoja limepita, na ndio maana kila sekunde utampigia simu kumuuliza umefika wapi? Mbona sikuoni? Fanya haraka bwana!, Kimbia au chukua pikipiki,, nimesimama hapa muda mrefu nakungoja tu sikuoni? Ni nini kimekukumba? Umekwama wapi? ..n.k.. Unaona Hiyo yote ni kumuharakisha ili tu afike, kwasababu kusubiri kunaumiza.

Lakini haiwezekani ukasema unamsubiria mtu, halafu masaa matatu yanapita, na bado huna hata wasiwasi, humpigii simu kumuuliza hata amefika wapi, au huna hata mpango wa kuulizia atafika saa ngapi, wewe umesimama tu unasema unamngoja, ni wazi kuwa hilo jambo haliwezekani vingenevyo utakuwa na shughuli zako nyingine za kando.

Na ndicho hicho Mungu anachotaka kuona kutoka kwetu, sisi tunaosema tunamngojea Bwana, ni lazima tuwe tunamkumbusha juu ya siku ile ya kuja aihimize ifike haraka, UFALME WAKE UJE HARAKA! (upesi)..Ndugu hichi ni kipengele muhimu sana ambacho Mungu anatazamia kila mkristo wa kweli aliyezaliwa mara ya pili awe anamwomba yeye daima, na ndio maana Bwana Yesu alikiweka katika sala hiyo ya msingi.

Kipimo kizuri cha kujitambua kama kweli umejiweka tayari kwa ajili ya kwenda mbinguni au La, basi ni kwenye kipengele hichi, Jipime je! Ndani yako ipo ile shauku ya kutamani siku ile ya mwisho ifike au La?. Kama haipo basi ujue hata unyakuo ukipita leo hii huendi popote, utabaki tu hapa duniani.

Ni kama tu Mwanafunzi shuleni, yule aliyejiandaa vizuri na mtihani wa mwisho, pale anapokumbuka tu mtihani wa taifa unakuja, huwa anatamani siku hizo zifike haraka amalize zake akapumzike, lakini yule ambaye hajajiandaa, utaona yeye ni kinyume chake, atatamani hata muda uzidi kuongezwa tu wa kuendelea kubaki shule…kwasababu hakujua kilichompeleka shuleni.

Na sisi kama wakristo wapitaji hapa duniani Bwana anatazamia, kila siku tunapoamka tunapolala tunapaswa tumwombe, tutamani na tumkumbushe jambo hilo, kuwa siku ile ya kwenda zetu kwa Baba mbinguni ifike haraka. Aharikishe neema ya wokovu ya kuwaokoa watu wake, mambo yaishe haraka tukapumzike kwake milele. Siku ya unyakuo, siku ile ambayo tutamwona Bwana wetu Yesu uso kwa uso mawinguni ifike!, Tukaile ile karama ya mwanakondoo na malaika mbinguni tuliyoandaliwa tangu zamani.

Siku ambayo tutaiona mbingu mpya na nchi mpya, kwa mara ya kwanza ikishuka ambayo haitakuwa na machozi tena, wala misiba, wala magonjwa, wala vita, wala matetemeko, wala chuki, wala mashindano, wala mahangaiko ya dunia hii, wala umaskini, wala ubaguzi.. siku hiyo tunaiomba na tunaitamani ifike.

Hili ni jambo ambalo kila siku tunatakiwa tumwombe Mungu, Unaweza ukaliona halina thamani machoni pako, lakini mbele za Mungu lina maana sana.. Lakini sisi tukiwa kila mara tunapomwendea Mungu ni kuomba tu magari, nyumba, biashara, wake, kila siku mambo ya kiduniani tu ndiyo tunayompelekea yeye….Hatuna muda wa kutafakari kuwa hii dunia inafika mwisho, na dunia inapita (1Yohana 2:17) Tujue kuwa Mungu anatuona kama hatujastahili kuurithi ufalme wake. Tupo tu.

Anza leo kujijengea desturi hii, ya kumhimiza Mungu, juu ya ufalme wake, aliotuahidia tangu zamani uje haraka ulimwenguni, Na hiyo ni ndio inayothibitisha kuwa kweli tunatamani unyakuo ufike haraka, kweli tunatamani kufutwa machozi, Hizo ndizo hoja zenye nguvu kwa Mungu wetu.

Kama tu viumbe vyenyewe (swala, twiga, mbwa, tausi, punda, ng’ombe n.k.) wanatazamia kwa shauku siku hiyo ya sisi kutukuzwa, inakupasaje wewe na mimi? Ambao ndio warithi wenyewe..Tunapaswa macho yetu yaelekee kule Zaidi.

Warumi 8:18 “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.

19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.

20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini”.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

JIFUNZE KUELEWA MAANA YA KUOA/KUOLEWA KABLA YA KUINGIA HUKO.

JINSI DHAMBI INAVYOMGHARIMU MTU SANA.

JE! Kaini alimpatia mke wake wapi?

JINSI WATU WANAVYOZAMA KATIKA USHIRIKINA NA UCHAWI.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/26/ufalme-wako-uje/