Yuko azuiaye sasa hata atakapoondolewa! ni nani huyo?

by Admin | 17 July 2020 08:46 pm07

SWALI: Naomba unisaidie hii 2 wathesalonike 2:7 “Yuko azuiaye sasa Hadi atakapoondolewa, naomba unisaidie huu mstari unamaanisha Nani huyo anayezuia na Ni kwa nini?”


JIBU: Ukianzia kusoma tokea mistari ya juu kidogo utaona inazungumzia habari za mpinga-Kristo ambaye biblia inamtaja kama “Asi” kwamba mwisho wa dunia hautafika kwanza kabla ya yeye kufunuliwa hapa duniani..

Kwasababu wakati ule, watu wa kipindi kile walidhani kuwa pengine wapo tayari katika wakati wenyewe wa mwisho wa dunia, Lakini mtume Paulo aliwapa siri ambayo alifunuliwa na Roho Mtakatifu na kuwaambia, ule mwisho hautakuja kwa namna hiyo, bali ni sharti kwanza yule Asi (yaani Mpinga-Kristo) afunuliwe duniani, aonekane kazi zake na mienendo yake, na kwamba watu wakishamwona huyo sasa ndio wajue kuwa dunia itakuwa na kipindi kifupi sana cha kuendelea kuwepo, ambacho si zaidi ya miaka 7 kulingana na unabii wa kibiblia.

Lakini pamoja na hayo aliendelea kuwasisitiza kuwa japokuwa Asi mwenyewe (Mpinga-Kristo), hajafunuliwa kwa wakati wao lakini ile siri yake ilikuwa imeshaanza kutenda kazi, akiwa na maana kuwa mienendo ya mpinga-Kristo ilikuwa imeshaanza kuonekana tangu ule wakati isipokuwa tu ilikuwa katika siri..Bado haijapata nafasi yote.

2Wathasalonike 2:5 “Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?

6 Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7 Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.

Sasa swali ni kwanini siri hiyo ya kuasi isijidhihirishe yote tangu ule wakati hata sasa ambapo imepita zaidi ya miaka 2000?.

Mtume Paulo anasema ni kwasababu Yupo azuiaye, Na huyo sio mwingine zaidi ya “Roho Mtakatifu”. Ikumbukwe kuwa Roho Mtakatifu ndiye mtunza uhai wa vitu vyote na viumbe vyote tangu mwanzo, Mungu asingeiumba hii dunia iwe makao mazuri ya watu kama sio Roho wake kutua kwanza juu ya uso wa nchi. Hii ikiwa na maana akiondolewa basi dunia inarudia katika hali yake ya ukiwa kama ilivyokuwa hapo mwanzo.

Leo hii unaona ni kwanini watu wanamtafuta Mungu, ni kwasababu Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani yao, ni kwanini wanaomba?, sababu ni hiyo hiyo ya Roho Mtakatifu, ni kwanini duniani hakuna vita vikali vya kiatomiki ambavyo vinaweza kuichakaza dunia mara moja nikwasababu Roho Mtakatifu anazuia..Ni kwanini Volcano, haviimezi dunia yote, ni kwasababu Roho Mtakatifu anazuia.

Lakini upo wakati ambapo, Mungu atamwondoa duniani kazi yake itakapoisha. Ambayo itaisha na watakatifu wa Mungu watakaonyakuliwa siku ile kwenda mbinguni. Maana yake kwamba ikitokea leo hii unyakuo umepita, basi na kazi ya roho Mtakatifu ya kuokoa (yaani ya kuwavuta watu kwa Mungu), na kuzuia amani duniani nayo inakuwa imeisha, Anaondoka..Ndio hapo yule Asi (yaani Mpinga-Kristo) naye anapata nafasi ya kufanya uharibifu wake wa kuleta dhiki kuu duniani, hapo ndipo mataifa yote duniani nayo yanapata nafasi ya kukusanyika kuleta vita kuu ya dunia ambayo haijawahi kutokea, hapo ndipo baadhi ya mapepo yaliyokuwa kifungoni yanaachiliwa duniani kwa muda ili kuwatesa watu, hapo ndipo dunia nayo itapoteza muhimili wake, matetemeko makubwa yatatokea duniani, volcano zitafumuka ardhini, jua litazima na mwezi kuwa damu na nyota kuanguka..na dunia itarudia kuwa ukiwa kama ilivyokuwa kabla ya Edeni.

Yaani hayo yote yatatimia ndani ya kipindi kifupi tu cha miaka saba.

Jiulize, unyakuo ukipita leo, mimi na wewe tutakuwa wapi?. Bwana alisema tutawezaje kupona tusipouthamini wokovu mkuu namna hii?

Hizi ni nyakati za hatari. Tubu dhambi kama bado hujafanya hivyo, na kama tayari basi zidi kudumu ndani ya neema ya Kristo mpaka siku ya mwisho wa unyakuo.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je! Shetani alitolea wapi uovu?

Nitaitofautishaje sauti ya Malaika na ya Roho Mtakatifu?

 Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako,katika kufanya maombezi?

WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA.

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI AU KUTOA TALAKA?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/17/yuko-azuiaye-sasa-hata-atakapoondolewa-ni-nani-huyo/