MANENO ALIYOWEZA KUTAMKA YESU TU PEKE YAKE.

by Admin | 18 July 2020 08:46 pm07

Yapo maneno ambayo huwezi kuzungumza, isipokuwa kwanza unaelewa vizuri ni nini unazungumza vinginevyo unaweza kujiweka kwenye kitanzi mwenyewe na kuingia matatizoni..

Kuna wakati Bwana aliwaambia wale watu wanaoshindana naye maneno haya…

“Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi..”? (Yohana 8:46)

Maneno haya si mepesi kabisa, Kumbuka juu kidogo tu kwenye sura hiyo hiyo swali la namna hii hii aliwauliza wale watu waliomfumania yule mwanamke katika uzinzi, lakini majibu yake ni kuwa sio tu kutomtupia yule mwanamke mawe, bali pia waliona aibu kuendelea kubaki maeneo yale, kwa mtihani huo mgumu waliopewa.

Yohana 8:7 “Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.

8 Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

9 Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao;

akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati”.

Unaona? Lakini hapa na yeye pia anajiweka katika hicho kitanzi na kuwauliza watu.. Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi?

Jaribu kujiweka wewe katika hiyo nafasi ukiwa kama kijana wa miaka 33 ambaye tayari umeshapitia mambo mengi katika maisha, halafu unasimama katikati ya umati wa watu wanaoshindana na wewe, unawauliza ni nani kati yenu anayenishuhudia kuwa nina dhambi?

Je! Wewe unaweza kusema hayo maneno?(Mimi siwezi)..Ndugu zako wote wamesimama karibu nawe , marafiki zako wote uliowahi kuishi nao na kusoma nao, wote pia wamesimama karibu hapo, majirani zako nao wapo, wafanyakazi wenzako wanasimama hapo vilevile halafu unawauliza wote “Kati yenu ninyi ni nani anayenishuhudia kuwa nina dhambi”..

Ni nani alishawahi kuniona au kusikia nimemsengenya mtu, ni nani nilishawahi kumdanganya au alishawahi kunisikia nadanganya, ni wapi nilishawahi kutamani, ni wapi nilishawahi kumvunjia mtu heshima, au kumwonea wivu, au kumwekea kinyongo, au kuonyesha unafki, kumfokea, kumtukana? ..Kama yupo hapa asimame, au ajitokeze, asimeme wewe siku fulani nilikuona ukikwepa kodi kwenye ile biashara yenu ya useremala…

Lakini wote waliosimama pale, hakuonekana hata mmoja aliyekuwa na la kumshitaki Yesu..sio jambo rahisi kama tunavyofikiri,

Na ndio maana mahali pengine biblia inasema..

1Petro 2:22 “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.”

Ni Yesu peke yake, katika ulimwengu mzima, katika vizazi vyote, ambaye tangu amezaliwa mpaka anakufa, hakuwahi kutenda dhambi hata moja, japokuwa alipitia majaribu mazito ya dhambi kuliko hata sisi.

Ndugu yangu Kwa YESU pekee mimi nimetia nanga! Sijui kwako?, kwasababu hakuna mwingine kama yeye, huyu pekee ndio wa kumtumainia, ni huyu pekee ndio wa kumtegemea kutusaidia kushinda huu ulimwengu kama yeye alivyoshinda, ni huyu huyu pekee ndio atakayetuokoa tukimwamini. Mimi na wewe tukimfanya kuwa rafiki wa maisha yetu, jambo la kwanza na la ajabu ni kuwa anatusamehe dhambi zetu zote, halafu anatuhesabia haki bure pasipo matendo yetu kwa neema, kiasi kwamba mbele za Mungu tunaonekana kuwa tumestahili haki yote.

Kisha baada ya hapo anamtuma Roho wake Mtakatifu ndani yetu. Ambaye kazi yake ni kutupa sisi nguvu ya kuishinda dhambi kama yeye alivyoishinda, na kutuongoza katika kuijua kweli yote.

Hivyo kama bado hujaokoka, saa ya wokovu ni sasa, fanya haraka mkaribishe Yesu maishani mwako. Kama umezichoka dhambi kweli, kama hutaki nafsi yako ipotee, basi mkimbilie Yesu haraka maadamu muda upo, Lakini tukikataa kuyasikia maneno yake basi yeye naye atatuacha, na kutuona tu kama sio watu tuliochaguliwa na Baba yake soma..

8:46 “Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki?

47 Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu”.

Natumaini wewe leo utayasikia maneno yake.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

RABI, UNAKAA WAPI?

NENO HILI NI GUMU,NI NANI AWEZAYE KULISIKIA?

Yeshuruni ni nani katika biblia?

KUMBUKA, VIVUKO VYA YORDANI VINAKUNGOJA MBELENI.

NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME

UNYAKUO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/18/maneno-aliyoweza-kutamka-yesu-tu-peke-yake/