RABI, UNAKAA WAPI?

RABI, UNAKAA WAPI?

Swali muhimu kwa Bwana wetu (Rabi unakaa wapi)?.

Yohana 1:35 “Tena siku ya pili yake Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake.

36 Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!

37 Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu.

38 Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?

39 Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi”.

Kipindi kifupi kabla ya Bwana Yesu kuianza huduma yake duniani, Yohana mbatizaji alitokea kuzishuhudia habari zake, alihubiri karibu kila mahali akieleza habari za ujio wa mwokozi wa ulimwengu. Na alipokuwa akihubiri aliwaeleza kuwa huyo mwokozi tayari yupo katikati ya wayahudi lakini hawamtambui(Yohana 1:26)..Hiyo iliwafanya watu wengi wawe na maswali mwengi, ni nani huyo, na anaishi wapi? ..

Yohana aliwaambia watu wote kuwa hata yeye mwenyewe hamjui lakini Mungu alimweleza kuwa Yule ambaye atamwona Roho Mtakatifu anashuka juu yake kama hua basi huyo ndiye. Hivyo baadhi ya wanafunzi wake wakawa makini sana kusubiria wakati wa kufunuliwa kwa tukio hilo..

Na kweli siku zilipofika, Yesu alipoongozwa na Roho kwenda kubatizwa kwa Yohana, wakati tu akiwa pale majini anabatizwa kama mtu mwingine wa kawaida tu, saa hiyo hiyo Yohana akaonyeshwa yale maono aliyoambiwa kuwa Yule ambaye Roho atashuka juu yake huyo ndiye…Na wakati huo huo Yohana akamtangaza kuwa huyu ndiye mwokozi wa ulimwengu, watu wote waliokuwa pale wakasikia..

Lakini baada ya Yesu kubatizwa aliondoka zake, wala hawakujua alipokwenda..Kwa bahati nzuri siku ya pili yake, Yohana alipokuwa na wawili kati ya wanafunzi wake anawafundisha, ambaye mmojawapo alikuwa ni Andrea, pengine wakiwa wanamuuliza habari za kuja kwa mwokozi ambaye jana alitoa habari zake..mara ghafla, huyo hapo wanamwona Bwana Yesu akipita karibu yao mahali walipokuwepo akiendelea katika safari yake…Yohana alipomuona tena, akawaambia wale wanafunzi…mtazameni! Mwanakondoo wa Mungu!!..

Muda huo huo wanafunzi wale wawili, hawakukawia wakamwacha Yohana na kuanza kumfuata Bwana Yesu kwa nyuma kisiri-siri..Na lengo lao lilikuwa ni moja tu wajue makao yake yalipo, wajue anapoishi hilo tu, na hayo mengine yatafuata baadaye..

Ndipo Yesu alipogundua kuwa kuna watu wanamtafuatilia tokea mbali akageuka na kuwaulizia Mnatafuta nini??

Hili ni swali ambalo hata leo hii..Bwana Yesu anatuuliza sisi tunaodai tunamfuata..Je! tunatafuta nini? Tunataka nini?

Lakini vijana wale wawili, hawakumwambia Rabi, tunaumwa tuombee, wala hawakumwambia tunaomba utuwekee mikono utubariki, wala hawakuomba wakae wafundishwe pale pale barabarabani, wala hawakuomba wafanyiwe miujiza,La! Badala yake walimuuliza Rabi, unakaa wapi?..Tunahitaji kujua unapoishi ili tujue tunakupataje hata ikitokea umepotea machoni petu tujue tunakupatia wapi..Tuna mengi ya kujifunza kwako, tunahitaji tukae chini tuzungumze na wewe, huku barabarani tu hakutoshi kutatuliwa matatizo yetu yote, na kutumiza haja zetu zote…ambapo tukishamaliza mazungumzo ndio basi tena hatutaonana tena.

Ndipo Yesu aliposikia hivyo akawapeleka nyumbani kwake.wakapaona..Hilo liliwafanya wale wanafunzi wawe na amani kuanzia huo wakati na muda si mrefu labda baada ya siku moja, Andrea ambaye alikuwa ni mmojawapo wa wale wanafunzi akaenda kumuita ndugu yake ambaye ndio Petro aje kwa Yesu..

Sasa embu fikiria kama asingeyafahamu makao ya Yesu, angemwelekezaji ndugu yake sehemu ya kumpata Yesu.?

Hata sasa, watu wengi wanamfuata Yesu, lakini hawaulizii anakaa wapi.. Nataka nikuambie ukimfuata Yesu, tambua kuwa atakuuliza nawe hili swali kama aliowauliza mitume wake, UNATAFUTA NINI?..Ukisema ninatafuta uponyaji, basi atakupa uponyaji wako na habari yenu itakuwa imeishia hapo hapo..Ukisema ninatafuta nyumba na magari atakupa nyumba na magari lakini habari yako na yeye itakuwa imeishia hapo njiani, ukisema ninatafuta mchumba atakupa mchumba lakini mkataba wenu utakuwa umeishia hapo…Lakini ukisema BWANA UNAKAA, WAPI? Hapo ndipo atakapokupeleka na kukukaribisha na kupaona anapokaa..

Anapokaa utapata kila kitu, zaidi ya yote ukimuhitaji muda wowote, unajua ni wapi utamkuta, hata mtu mwingine akihitaji kumjua huyo Yesu unayemfuata itakuwa ni rahisi kumwelekeza ni wapi alipo kwasababu anapajua nyumbani kwake….Na nyumbani kwake si pengine zaidi ya kwenye NENO LAKE.

Watu wengi wasasa wanalikimbia Neno la Mungu, wanatafuta njia za mkato za kumfikia Kristo..Na ndio maana Bwana hawawi wa kudumu ndani yao kwasababu wanakutana naye njiani tu kama habati, akikunja kona tu basi hawamuoni tena..na wala wao hawana habari naye tena..kwasababu wameshapata haja ya mioyo yao.

Unapolikimbia Neno la Mungu, hutaki kumjua Kristo katika Neno lake halafu unamtafuta katika maombezi, au maji upako, au miujiza hapo ni sawa na unamkimbia Kristo, kwasababu yeye mwenyewe ni NENO. Mhubiri yeyote anayekuletea habari njema za Yesu Kristo ni mfano wa Yohana mbatizaji..anakuelekeza kwa Kristo, hivyo ni jukumu lako wewe mwenyewe kujua unapomfuata una malengo gani na yeye.. Kama ni wa muda tu, wa kukutimizia mahitaji yako kisha basi, au kwamba ni wa kudumu..Kama ni wa kudumu basi taka kujua anapoishi…

Neno la Kristo likikaa kwa wingi ndani yako, basi ujue upo karibu sana na Yesu kuliko mtu mwingine yoyote kama ilivyokuwa kwa mitume, ambao walikuwa ni zaidi ya makutano mengi yaliyokuwa yanamfuata Kristo..walizijua siri nyingi kumhusu Yesu ambazo makutano wengine walikuwa hawazifahamu…Ikiwa utaishikilia tu dini yako, au dhehebu lako, ukadhani Kristo yupo huko na huku huna habari ya biblia, Hujawahi kutenga muda kukisoma angalau kitabu kimoja cha injili chote peke yako pasipo kusubiri kusimuliwa na mtu au mhubiri fulani…nataka nikuambie bado hujampata Yesu.

Na wakati mwingine anakuwa anapita akitembea huko na huko na kukutana na wewe katika safari yako ya Maisha…kama wale watu wa Emau, waliokuwa wanatembea na ghafla njiani Yesu akaungana nao pasipo wenyewe kujua kama ni Yesu…na kama ukisoma pale kwa makini utaona baada ya Yesu kuzungumza nao wakiwa kule kule njiani, akataka kama kuendelea mbele na safari yake..mpaka wale watu wawili walipomshurutisha aingie ndani kwao ale nao..na alipoingia ndani kwao na kula nao ghafla macho yao yakafumbuliwa na kumtambua ni Yesu, na akatoweka mbele yao.(Luka 24:13-32)

Hali kadhalika leo hii unapoisikia injili kama hii ambayo inakufikia hapo ulipo bure, ni Yesu anapita karibu na wewe hakikisha unamkaribisha nyumbani mwako (yaani aingie moyoni mwako kama wale watu wa Emau)..na kisha akishaingia kwako usikubali aondoke bila na yeye kukupeleka kwake (yaani katika Neno lake) kama wale wanafunzi wawili wa Yesu walivyofanya.

Ni maombi yangu kuwa Leo, usimwache Yesu akawa MPITAJI NJIANI TU KWAKO, anza kuchukua hatua ya kudumu kwenda nyumbani kwake (kwenye Neno lake), upate pumziko la kweli..na yeye aingie kwako…Penda kulitafakari Neno la Mungu kwa kadiri uwezavyo, na Yesu Kristo atakuwa na wewe kila wakati…Atakuita RAFIKI kama alivyowaita MITUME.  Mwulize leo unakaa wapi? Na atakufunulia mambo ambayo hata wanadamu wengine hawajui kwasababu upo sikuzote nyumbani kwake na yeye yupo nyumbani mwako.

Ubarikiwe sana. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!

UMUHIMU WA YESU KWETU.

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI.

IMANI NI NINI?

NENO LA MUNGU NI DAWA ILIYO TOFAUTI NA DAWA NYINGINE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Peter Jeremia
Peter Jeremia
2 years ago

amina