MAJONZI YA MTUME PAULO KWA NDUGU ZAKE.

by Admin | 19 July 2020 08:46 pm07

Ukisoma kitabu cha Warumi sura ya 9, ya 10, na ya 11..utaona mambo mazito sana mtume Paulo aliyokuwa akiyazungumza juu ya ndugu zake wayahudi. Akieleza jinsi neema ya Mungu ilivyoondolewa kwao, kiasi kwamba hata wangehubiriwa vipi injili wasingeweza kuipokea.

Chukua muda kwa wakati wako, pitia sura hizo kwa utulivu sana, ukisoma juu juu hutaona chochote, lakini ukisoma kwa utulivu huku ukimwomba Roho Mtakatifu akusaidie, nakuambia hutaichezea hata kidogo hii neema tuliyopewa sisi watu wa mataifa.

Mtume Paulo alipewa kulijua hilo mpaka akawa anasema, anayo huzuni nyingi, na maumivu yasiyokoma moyoni mwake kwa ajili ya ndugu zake (yaani wayahudi), maumivu ya kila siku, akijua kuwa wokovu umeondolewa kwao..

Kiasi kwamba alitamani hata kama ingewezekana yeye  mwenyewe aupoteze wokovu wake, atengwe na Kristo ili kusudi kwamba ndugu zake wote wapone, basi angefanya hivyo..soma..

Warumi 9:1  “Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu,

2  ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu.

 3  Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe NIHARIMISHWE NA KUTENGWA NA KRISTO kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili”;

Kauli hiyo si rahisi kuizungumza, lakini kwa huruma ya watu wengine, na huzuni unayoisikia moyoni mwako inakulazimu uitamke, si kwamba unatamani iwe hivyo, lakini kama ingewezekana.. Ni sawa leo umuone mtoto wako mchanga, kapata ajali halafu kakatika mikono, halafu anatapata tapa pale chini kwa maumivu,akilia, ni wazi kuwa utatamani ungeyapitia wewe yale maumivu yake..Kuliko kumuona anaendelea kuteseka katika ile hali.

Ndivyo ilivyokuwa kwa mtume Paulo, alitamani kama ingekuwa inawezekana yeye kuharamishwa, (kufanywa kuwa mwana-haramu,atengwe na Kristo) kusudi kwamba ndugu zake wayahudi waiamini Injili waokolewe.. Lakini ilikuwa haiwezekani.

Ndugu kama hufahamu wakati ule wa kanisa la kwanza ni wayahudi wachache sana, waliiamini Injili, japokuwa ilikuwa ni mamilioni waliokuwa wanaisikia, na ndio maana ukisoma mbele kidogo mtume Paulo anasema.

Warumi 9.27  “..Hesabu ya wana wa Israeli,ijapokuwa ni kama mchanga wa bahari,ni mabaki yao tu watakaookolewa”

Waliokolewa wachache sana, mpaka akasema, kama Mungu asingewaachia mabaki basi wangefananishwa na Sodoma na Gomora,(yaani akiwa na maana asingeokoka myahudi hata mmoja wakati wao)..

Na hiyo yote ilikuwa ni kwasababu waliikataa neema ya wokovu iliyoletwa na Yesu Kristo, alipokuwa duniani, na kuendelea na njia zao za kumtafuta Mungu, huku wamemweka Kristo pembeni. Ikapelekea mlango wa neema kufungwa juu yao. Na ndio maana utaona haijalishi walikuwa na bidii kiasi gani kwa Mungu lakini hawakuweza kuuona mlango wa neema hata kidogo kwasababu tu walimkataa Kristo (kasome Luka 13:34-35). Mtume Paulo alisema hivyo katika ile sura ya 10

Warumi 10:1  “Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.

2  Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa”.

Hilo jambo linaendelea mpaka sasa, takribani miaka 2000 imepita, lakini  bado mlango wa neema haujafunuliwa kwao. Na hiyo yote ni ili mimi na wewe (watu wa mataifa), tuipokee neema.

Lakini mwisho kabisa mtume Paulo alipewa siri na Mungu, na siri hiyo aliiweka wazi akataka sisi nasi tuijue (yaani mimi na wewe), kwamba utafika wakati ambao Mungu atawarehemu tena..Na kikisha fika hicho kipindi basi sisi tufahamu Habari yote ndio imeishia hapo, kama mtu yeyote wa mataifa atakuwa hajaingia ndani ya Kristo, ndio basi tena..Soma

Warumi 11:25  “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.

26  Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake”.

Jiulize wayahudi kwa miaka 2000 wanautafuta uso wa Mungu lakini hawaupati, unadhani siku hiyo neema ikiondolewa kwetu, sisi tutaipatia wapi? Na dalili zote zinaonyesha wakati wao upo karibuni sana…Tayari taifa hili lilishachipuka tangu mwaka 1948, unadhani ni nini kinachosubiriwa hawa watu Mungu asiwageukie? Usiku na mchana wapo pale kwenye “ukuta wa maombolezo wa Nehemia” wanamlilia Mungu awaokoe (hayo yalikuwa ni majonzi ya mtume Paulo)..Lakini Bwana anakawia kidogo kwa ajili yangu mimi na wewe.

Moja ya hizi siku, Mungu atakisikia kilio chao,.mlango wa neema utafunguliwa kwao, na kwetu utafungwa,. Huo ndio ule wakati wa mwenye nyumba kusimama na kuufunga mlango, na watu watakuwa wakisimama nje na kugonga wafunguliwe lakini Bwana atawaambia siwajui mtokako.(Luka 13:25-28)…Duniani kutakuwa na kilio na kusaga meno.

Hivyo tunaposikia maneno haya, tujitathimini Je! Ni kweli bado tupo ndani ya Kristo? Au tupo vuguvugu. Kama wewe unaisikia injili na bado unasua sua basi uingie sasa kwa nia yote acha kusitasita kwenye mawazo mawili muda unazidi kwenda, kwasababu siku hizi ni za mwisho. Lango hili likishafungwa, halitafunguliwa kamwe.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.

MADHARA YA KUTOA MIMBA.

TABIA YAKO NI YA MNYAMA GANI?

MAHALI UNAPOPASWA USIMVUMILIE SHETANI HATA KIDOGO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/19/majonzi-ya-mtume-paulo-kwa-ndugu-zake/