MJUMBE ASIYEKUWA NA UJUMBE.

by Admin | 21 July 2020 08:46 pm07

Mjumbe asiyekuwa na ujumbe:

Ukisoma katika biblia utakumbuka habari ile ya Daudi na mwanawe Absalomu, jinsi walivyoingia katika mapambano makali,.mpaka kuepelekea vita vizito kupiganwa kule msituni..Kama wengi wetu tunavyofahamu, katika vita vile Daudi hakuwepo bali alimtuma amiri jeshi wake mkuu aliyeitwa Yoabu, kupigana nao. Lakini kabla ya kuanza vita Daudi alimwagiza Yoabu, kuwa ahakikishe kijana hawamuui bali wanamleta mikononi mwake akiwa mzima.

Lakini Yoabu alipomkamata Absalomu, alimuua, na kisha akamtupa kwenye shimo refu sana. Na Israeli walipoona kiongozi wao Absalomu amekufa, vita vikaishia pale pale, watu wote wakatawanyika na kwenda makwao.

Sasa kilichokuwa kimebakia, ni kumpelekea Daudi taarifa za vita, Lakini ni nani wa kumpelekea Daudi Habari ya kifo cha mwanawe. Hapo ndipo wakatokea wajumbe wawili mmoja aliitwa, Ahimaasi, mwana wa Sadoki na mwingine, alikuwa ni mkushi.

Sasa huyu Ahimaasi, akamwomba Yoabu, akimbie ampelekee ujumbe Mfalme Daudi kuhusu vita, lakini Yoabu alimwambia, kwasasa wewe huwezi kupeleka ujumbe, na sababu ya kutopeleka ujumbe ni kwasababu zile sio Habari njema apelekazo..

Ndipo Yoabu akamwita kijana mwingine mkushi akamtuma badala yake akamwambia nenda ukamwambie mfalme uliyoyaona..

2Samweli 18:21 “Ndipo Yoabu akamwambia Mkushi mmoja, Nenda ukamwambie mfalme hayo uliyoyaona. Na huyo Mkushi akajiinamisha mbele ya Yoabu, akaenda zake mbio.”

Ndipo huyu mkushi akatii akaondoka mbio mara moja..Lakini yule Ahimaasi, alipoona mwenzake katumwa halafu yeye bado kabaki, akaendelea kumsisitiza Yoabu na yeye aende..Tusome.

2Samweli 18:22 “Ndipo Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akamwambia Yoabu mara ya pili, Haidhuru, tafadhali nipe ruhusa, nipige mbio na mimi nyuma ya huyo Mkushi. Naye Yoabu akasema, Mbona wewe unataka kupiga mbio, mwanangu, kwa maana hutapata kitu kwa habari hizo unazopeleka?

23 Akasema, Haidhuru, nitapiga mbio. Akamwambia, Haya, piga mbio. Ndipo Ahimaasi akapiga mbio, akishika njia ya uwandani, akampita yule Mkushi”.

Hivyo wote wawili wakaanza safari, lakini tofauti ya mjumbe wa kwanza na yule wa pili ni kuwa yule mkushi, alikuwa na ujumbe wa kupeleka kwa yale aliyoyaona vitani jinsi Absalomu alivyouliwa, lakini yule mwingine hakuona chochote, alisikia tu..

Sasa biblia inatuambia yule wa pili alipiga mbio Zaidi ya yule wa kwanza na kufika kwa mfalme, (hatujui alipiga short-cut au vipi), lakini alifikia wa kwanza kuliko yule mwingine.

Akafika mpaka malangoni mwa mfalme, akaulizwa, umeleta ujumbe gani? Akasema, Mungu ashukuruwe kwa kuwa maadui zako wametawanyishwa.

Lakini Daudi alipomuuliza Habari za kijana? … sikiliza majibu yake.

2Samweli 18:29 “Mfalme akauliza, Je! Yule kijana, Absalomu, yu salama? Ahimaasi akajibu, Yoabu aliponituma mimi mtumishi wa mfalme, mimi mtumishi wako, NALIONA KISHINDO KIKUBWA, LAKINI SIKUJUA SABABU YAKE”.

Daudi aliposikia hivyo akamwambia simama pembeni, akamngojea yule mwingine afike.. Ndipo alipofika yule mwingine na kuulizwa..naye akajibu, “wote wainukao ili kukudhuru, na wawe kama alivyo yule kijana”(akimaanisha kuwa Absalomu Amekufa).

Ndipo Daudi aliposikia vile alienda kulia sana, akimwombolezea mwanawe..

NI NINI BWANA ANATAKA TUJIFUNZE?.

Kama haujafikiria, kuwa mhubiri, au mchungaji, au nabii au mwinjilisti au mtume, au mjumbe yoyote wa Mungu, kwa njia yoyote ile,iwe katika uimbaji, au uandishi n.k. ni vizuri kwanza ukafahamu na kuuelewa vizuri ni ujumbe gani unakabidhiwa kuupeleka..

Ujumbe/ Agizo kuu tulilopewa na Bwana Yesu kwa mtu yeyote anayetaka kuifanya kazi ya Mungu ni hili..

Mathayo 28:19 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;

20 na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi;..”

Sasa jiulize, Je, katika kujibidiisha kwako kuwahubiria watu, Je! Lengo lako ni kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa Kristo?, Je! Ni kuwafundisha kuyashika yale yote Yesu aliyotuamuru au mambo ya kidunia tu?..

Wengine wakiulizwa kwanini auhubiri injili kama ile ya mitume injjili kamilifu na ya utakatifu, watakwambia, mimi sikuitwa kuhubiri injili hiyo! Mimi nimeitwa kuwa mfariji tu!! ..Nataka nikuambie ndugu hapo ni sawa na unakimbia bure bila ujumbe wowote kama yule Ahimaasi. Kumbuka hapo kwenye Mathayo 28, agizo hilo lilipewa kwa watu wote kiujumla, hapo Bwana alikuwa hazungumzi na Petro peke yake, au Mathayo peke yake, au Filipo…alikuwa anazungumza na wote waliokuwepo pale Pamoja na sisi wote tunaosoma.

Ikiwa mafundisho yako, hayalengi kuwavuta watu wa Kristo, kinyume chake, ni kuwahubiria tu jinsi ya kufanikiwa hapa duniani..Basi ujue wewe ni mjumbe usiyekuwa na ujumbe.. Na kazi yako haina faida yoyote, haijalishi utakuwa unawakusanya maelfu ya watu kiasi gani kukusikiliza, au wanakusifia kiasi gani.

Ujumbe tuliopewa ni mmoja tu, nao ni kuwafanya “mataifa yote kuwa wanafunzi wake”. Na unamfanyaje mtu kuwa mwanafunzi, Bwana Yesu alishasema katika Luka 14:27

Hivyo chochote tukihubiricho hakipaswi kwenda mbali na kiini hicho cha agizo..Hata kama tutahubiri hayo mengine lakini kiini hicho kionekane, na hiyo ni kwa faida yetu wenyewe ili kazi yetu isiwe bure mbele za Mungu.

Bwana akabariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je! hizi roho saba za Mungu ni zipi? na je zinatofautiana na Roho Mtakatifu?

SADAKA YA MALIMBUKO.

KUOTA UNACHEZA MPIRA.

MAMBO MENGINE HAYATOKI ISIPOKUWA KWA KUFUNGA.

WAKATI WA KRISTO KUSIMAMA,UMEKARIBIA SANA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/21/mjumbe-asiyekuwa-na-ujumbe/