KIAMA KINATISHA.

by Admin | 27 July 2020 08:46 pm07

Ikiwa leo hii Unyakuo utapita, na wewe ukabaki, basi fahamu dunia itakuwa na miaka 7 tu mbele yako kabla haijaisha, yaani kama leo ni mwaka 2020, basi haitapita mwaka 2027, kabla ya kila kitu unachokiona leo hii kuwa jivu.. Miaka hiyo saba imepatikana kutoka katika ule Unabii wa Danieli wa yale majuma 70, (Danieli 9:24) ambapo mpaka sasa limebakia juma moja tu, lenye miaka 7 kuanza.

Sasa katika hicho kipindi cha miaka 7 dunia haitakuwa tu umestarehe ikisubiria mwisho ufike hapana.. Kutaanza kuwa na mabadiliko ya haraka na ya ghafla sana duniani, jambo ambalo litawashitusha wengi, hapo ndipo ule unabii wa Bwana Yesu unaosema siku hiyo itawajilia kwa ghafla utakapotimia (Luka 21:34-35), kama tu unavyoona huu ugonjwa wa Corona ulivyoijilia hii duniani kwa ghafla bila taarifa, ndivyo itakavyokuwa hicho kipindi.

Miaka hii 7 inajulikana kama miaka ya dhiki, na imegawanyika katika vipengele vikuu viwili, Kipengele cha kwanza, ni cha miaka 3 na nusu, ya kwanza, na cha pili ni miaka 3 na nusu ya mwisho.

Sasa katika hiyo miaka mitatu na nusu ya kwanza, kitakuwa ni kipindi cha mpinga-kristo, kujiimarisha, na kuingia agano na watu(mataifa mengi),Danieli 9:27, ikiwemo taifa la Israeli,.na wakati wa watu kupokea chapa. Lakini wakati huo huo Wale manabii wawili (Mashahidi 2), tunaowasoma katika ufunuo 11, watasimama kuihubiria Israeli, kwa muda huo wa miaka mitatu na nusu ya kwanza,.Injili yao haitakuwa ya maneno matupu tu, bali itafuatana na mapigo kadha wa kadha mwishoni mwishoni karibia na kumaliza ushuhuda wao, soma Ufunuo 11, mapigo hayo yatakuwa ni makali na ya kutesa kiasi kwamba siku mpinga-Kristo atakapowaua, dunia nzima itafurahia tukio hilo na kuepelekeana zawadi wao kwa wao.

Sasa hiyo miaka 3 na nusu ya mwanzo itakapokwisha, Mpinga-Kristo atakuwa ameshapata nguvu za kutosha, wakati huo, ndio atanyanyuka sasa, kuleta dhiki kuu juu ya wale wote ambao hawatakuwa na chapa/Utambulisho wake (666).. Hapa hatanusurika mwanadamu yeyote ulimwenguni aliyeikwepa chapa hiyo, kutakuwa na mawili aidha upokee chapa, au ufe.. Na kifo sio cha kupigwa risasi au kunyongwa…Ni heri ingekuwa hivyo!…lakini kifo watakachokufa wale walioikataa chapa kitakuwa ni cha kuteswa mda mrefu sana…Watu watateswa hata kwa mwaka mmoja au miwili bila kuruhusiwa wafe…Ni mateso ya kuwekwa kwenye kambi maalumu za mateso..yale ya kale ambayo unatolewa macho, unavuliwa nguo, wakati wa baridi..halafu unafanyishwa kazi ngumu, huku unapewa mlo mmoja kwa wiki,(na mlo wenyewe ni supu tu) na huku unachapwa na viboko, yatakuwa ni mateso madogo sana…Watu watatamani wafe huko lakini hawatakufa..watateseka katika hiyo hali hata kwa miaka miwili ndio uje wafe!…

Bwana Yesu alisema dhiki hiyo ambayo itakuja kutokea haijawahi kutokea tangu dunia iumbwe na wala haitakaa itokee tena baada ya hapo.. Kiasi kwamba watakaowezi kuyastahimili hayo watakuwa ni watu wachache sana, wengine wote wataipokea chapa ya mnyama. Na jambo hilo litaendelea kwa muda wote wa miaka mitatu na nusu ya mwisho.

Hapo katika kutakuwa ni mapigo mengine mengi sana, mapigo ya baragumu saba yataendelea..na mapigo ya vitasa saba vya Mungu nayo pia yatafuata, mwishoni mwa miaka mitatu na nusu, kwa urefu wa somo hili fungua hapa >> SIKU YA BWANA INAYOTISHA YAJA!..hatuwezi kueleza yote hapa sehemu moja.

Sasa mwisho kabisa ya dhiki hizo kupita, unaweza kudhani, mambo ndio yamekwisha?, Wale waliopokea chapa, basi wamepona,? Hapana, ndugu kinyume chake huo ndio mwanzo wa ukurusa mwingine ujulikanao kama SIKU YA BWANA.

Hii siku ya Bwana, itakuwa ni kipindi cha siku 30 nyingine juu ya ile miaka saba kupita…Watu watadhani kuipokea chapa ndio kupona, lakini ni sawa na mtu aliyemkimbia Simba akakutana na dubu biblia inasema hivyo..ni heri wangekufa kwenye dhiki kuu ya mpinga-Kristo.

Amosi 5:18 “Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya Bwana; kwani kuitamani siku ya Bwana? Ni giza, wala si nuru.

19 Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma”.

Hichi kipindi watakaokuwepo duniani hawataamini macho yao, watashikwa na butwaa la ajabu, kwasababu, watashuhudia hii dunia ikigeuzwa na kuwa kama mojawapo ya sayari Fulani huko angani isiyokaliwa na watu, Kwasababu hili jua tunaloliona litazimwa lote, (kutakuwa na giza kubwa) mwezi utakuwa mwekundu kama damu, nyota zote zitaondoka huko mbinguni kutakuwa na giza tororo ambalo halijawahi kutokea duniani…

Amosi 5:20” Je! Siku ya Bwana haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga”.

Lengo la siku hiyo ya Bwana, ni kuifanya dunia kuwa ukiwa kama tulivyoikuta siku ile ya uumbaji..Mwanzo 1:1 “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. NAYO NCHI ILIKUWA UKIWA, TENA UTUPU, NA GIZA lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji”

Hivyo dunia itafanywa ukiwa tena..

Isaya 13:9 “Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ILI IIFANYE NCHI KUWA UKIWA, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.

10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.

11 Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;

12 nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri”.

Siku hii itaambatana na tetemeko kubwa la Ardhi ambalo halijawahi kutokea tangu dunia iumbwe, visiwa vitahama,..

Ufunuo 16:18 “Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo.

19 Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake.

20 Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena.

21 Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno”.

Unaona, tutakayokuwa yanaendelea kwenye hii dunia wakati huo?? Ndugu kuna vifungu vingi sana vya kuandika hapa,vinavyoilezea hii siku ya kuogofya ya Bwana, lakini hatuwezi kuviorodhesha vyote, kwa muda wako pitia vifungu hivi (Yoeli 1:15, Yoeli 2:1, 2:11, Yoeli 3:14),

Sasa baada ya hayo kupita, Ndipo Kristo atatokea mawinguni, Na kila jicho litamwona, naye atawaua waliosalia na majeshi yao, na kumaliza kila kitu, wale waovu waliosalia (Mathayo 24:29-30, Ufunuo 19:11-21)..

Na baada ya hapo kutakuwa ni siku nyingine 45, juu ya zile siku 30, ambapo ndani ya siku hizo, wafu watafufuliwa watawale pamoja na yeye, pamoja na ile hukumu ya mataifa ya kuwatenga kondoo na mbuzi, na katika kipindi hicho hicho Kristo ataitengeneza tena hii dunia upya, Nayo itakuwa nzuri zaidi ya Edeni, nasi tutawala naye kwa kipindi kingine cha amani cha miaka 1000, wakati huo hakuna mwovu yoyote, ayatakayenusuruka..

Sasa hapa tumefupisha tu, unaweza kudhani kama hizi ni hadithi tu, au mambo hayo bado sana, yatachukua mamia ya miaka huko mbeleni, Lakini fahamu kuwa hivyo ndivyo shetani anavyotaka ujue ili siku ile ikujie kwa ghafla..Lakini maandiko yanakuambia hivi..

Sefania 1:14 “Hiyo siku ya Bwana iliyo kuu i karibu; I karibu, nayo inafanya haraka sana; Naam, sauti ya siku ya Bwana; Shujaa hulia kwa uchungu mwingi huko!

15 Siku ile ni siku ya ghadhabu, Siku ya fadhaa na dhiki, Siku ya uharibifu na ukiwa, Siku ya giza na utusitusi, Siku ya mawingu na giza kuu,

16 Siku ya tarumbeta na ya kamsa, Juu ya miji yenye maboma, Juu ya buruji zilizo ndefu sana.

17 Nami nitawaletea wanadamu dhiki, hata watakwenda kama vipofu, kwa sababu wamemtenda Bwana dhambi; na damu yao itamwagwa kama mavumbi, na nyama yao kama mavi.

18 Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku ile ya ghadhabu ya Bwana; bali nchi yote pia itateketezwa kwa moto wa wivu wake; maana atawakomesha watu wote wakaao katika nchi hii, naam, ukomo wa kutisha”.

Tusiwe na mengi ya kusema, ila ombi langu ni kuwa kama hujampa Kristo maisha yako, basi fanya uamuzi huu haraka, Kumbuka anakupenda sana, anakujali sana, anakuthamini, na anatamani sana uyarithi aliyokwenda kukuandalia miaka 2000 iliyopita kule juu mbinguni..Kwa muda wote huo! Ni lazima ni mambo mengi na mazuri aliyotuandalia….Wokovu wake ni bure, tena unapatikana sehemu yoyote, bila malipo. Fanya hivyo naye atajifunua kwako. (kiama kinatisha!)

Bwana akubariki, Bwana atubariki sote.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Kwanini Mungu anasema “Afanyaye malaika zake kuwa pepo”?

NA NENO LA BWANA LILIKUWA ADIMU SIKU ZILE.

IKIMBIE DHAMBI KWA GHARAMA ZOZOTE ZILE!

NA NENO LA BWANA LILIKUWA ADIMU SIKU ZILE.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/27/kiama-kinatisha/