Ikimbie dhambi.
Shalom.
Karibu tujifunze biblia, na kujikumbusha yale ambayo tumeshajifunza. Kitu pekee ambacho watu wa Mungu tunapaswa tukiogope kuliko vyote kwa nyakati zetu hizi sasa ni dhambi…Wala hatupaswi kuogopa mapepo wala wachawi wala shetani mwenyewe. Tunachopaswa kukiogopa cha kwanza ni dhambi.
Kwasababu dhambi ndio mlango wa mambo hayo mengine yote.
Hivyo kwa nguvu zote na kwa jitihada zote tunapaswa tujiepushe na dhambi..Na tunajiepusha na dhambi kwa kuikimbia dhambi..maana yake unaiacha kwa gharama zozote zile..Roho Mtakatifu biblia inamwita MSAIDIZI, (Yohana 14:16), unaelewa maana ya msaidizi?..Msaidizi ni mtu anayekusaidia wewe kufanya jambo Fulani ambalo tayari umeshachukua hatua ya kulifanya…yeye sio mfanyaji..bali ni mwongezeaji nguvu kile ambacho umeshaanza kukifanya…
Hivyo tunapookoka na kumpokea Roho Mtakatifu ndani yetu…kazi yake sio KUTUZUIA KWA NGUVU TUSIFANYE DHAMBI!..Hapana hiyo sio kazi yake hata kidogo…Kazi yake ni kutusaidia namna ya kuishinda dhambi!..anatupa mashauri, anatupa kila sababu kwanini sasa hatupaswi kufanya jambo hili baya na tufanye hili jema..Hivyo tunapomtii mashauri yake ndani yetu ile kiu ya kufanya dhambi inakufa ghafla, ndipo hapo tunajikuta tunakaa bila kutenda dhambi. Na kwa jinsi unavyozidi kujizoeza kumtii ndani yako ndivyo zile dhambi zinazidi kufa ndani yako. Ni kawaida kitu usipokifanyia mazoezi muda mrefu unakisahau na unapoteza uzoefu wa hicho kitu (kitendo cha kupoteza uzoefu wa kile ulichokuwa unakifanya ndio kufa katika hicho kitu)…kadhalika unapopoteza uzoefu katika kutenda dhambi ambazo ulikuwa unazitenda hapo kwanza, unapomtii Roho Mtakatifu ndani yako..ule uzoefu unapungua na hatimaye unaisha kabisa na unakuwa UMEKUFA KWA HABARI YA DHAMBI!…Unakuwa hata iweje huwezi kufanya uasherati, huwezi kutukana, huwezi kuiba, huwezi kula rushwa, huwezi kumchukia mtu n.k
Sasa tatizo kubwa linalokuja kwa wengi wetu ni kutoelewa kazi ya Roho Mtakatifu ndani yetu, na hivyo tunadhani Roho anapokuja ndani yetu kama dikteta, ambaye ataziharibu na kutuzia kwa nguvu tusifanye dhambi. Na kutokana na watu kufikiria hivyo wanajikuta wanapopokea Roho na kujiachia ndipo wanajikuta wanashindwa na dhambi na hivyo kuendelea na maisha ya dhambi..na kujiuliza wengine wanawezaje na wao wanashindwa.
Nataka nikuambie ukishaamua kumfuata Bwana Yesu kwa kutubu dhambi zako, ambazo Roho kakushuhudia ndani yako kwamba umepotea kwa hizo na hivyo uziache..Hatua inayofuata baada ya hapo ni kumtii. Na humtii kwa kusema maneno tu mdomoni kwamba “NIMEKUTII BWANA”. Hapana huo ni mwanzo tu wa kutii..Unapaswa umtii kwa VITENDO. Maana yake ni kwamba kama ulikuwa unafanya dhambi Fulani UNAIACHA kwa lazima!…Hutafuti ushauri kwa yeyote Yule, unaiacha kwa kutumia akili zako zote, nguvu zako zote, na roho yako yote. Wala hapo huhitaji kuombewa..
Kwamfano tuchukue mfano mmoja namna ya kuiacha dhambi ya uasherati kisha tutahitimisha. Dhambi ya uasherati ambayo ndani yake inajumuisha uzinzi, ulawiti, ufiraji, na usagaji na hata utazamaji wa picha cha ngono na kujichua, na masturbation…Dhambi hii haimtoki mtu kwa Kuombewa!!..Usimfuate mtumishi wa Mungu na kumwambia niombee niache dhambi hii au dhambi ile..Hakuna maombi ya namna hiyo!..Nakuambia hivyo kwasababu na sisi wengine tulikuwa namna hiyo hiyo..tukadhani kuombewa ndio suluhisho..tukafunga muda mrefu na kujiombea na hakuna kilichobadilika ndani yetu, mpaka tulipoyasoma maandiko, tukaifahamu kweli nayo hiyo kweli ikatuweka huru. Hivyo ndugu mpendwa usipoteze muda kufanya utafiti ambao tayari umeshasaidiwa kuufanya utazunguka na kuzunguka na mwisho wa siku utarudi pale pale.
Suluhisho la kuacha dhambi ya uasherati ni KUUKIMBIA!..Kuukimbia maana yake ni kuondoka bila HIARI ya huo uasherati. Maana yake ni kwamba kama ulikuwa unaishi na mwanamke/mwanamume ambaye mnafanya naye uasherati ni KUMKIMBIA GHAFLA! Na Kukata mazoea!…Akikutafuta kwenye simu mwambie mara moja tu kwamba umeokoka na hivyo tunapaswa tutubu kwa yote tuliyokuwa tunayatenda na kumrudia Mungu. Ukiona hakuelewi wewe jiokoe nafsi yako usitazame nyuma wala usiwe na huruma, usipokee simu zake, …Usianze kushauriana naye huku bado mnakutana kutana na kuzungumza zungumza, akikutafuta kwenye simu usijibu meseji yake hata moja, hata akilia kwa machozi ya damu kwamba mrudiane usiwe na huruma jiokoe nafsi yako na yake, kwa kuukimbia uasherati ikiwezekana block hiyo namba …Usizungumze naye hata kidogo. Mfano wa Yusufu. Mke wa Potifa alimtamani na Yusufu baada ya kulijua hilo, aliacha kuongea na mke wa Potifa..
Mwanzo 39:10 “Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye”.
Utasemaje unataka kuacha uzinzi na bado unaongea na unajibu meseji za watu unaozini nao?..utasemaje unataka kuacha uasherati na huku unamazoea zoea na wanawake wa mtaani na wanaume wa mtaani?, na huku bado unafuatilia vitamthilia na vi-movie vya kipepo vyenye maudhui ya kizinzi ndani yake kwenye Tv yako vinavyochochea uzinzi tu na wala si kitu kingine?..utasemaje unataka kuacha kutazama picha za ngono na huku kwenye simu yako bado zipo?, bado umejiunga whatsapp na facebook makundi ya mambo hayo?, utasemaje unatamani kuacha pombe na wakati kuna chupa za bia ndani mwako, na bado unakula meza moja na kampani zako za walevi?. Na dhambi nyingine zote ni hivyo hivyo…dawa ya kuziacha ni KUZIKIMBIA!!…Ondoka! Dhambi nyingine ili uweze kuziepuka zinakugharimu kuhama hata hapo ulipo, hama hata mtaa..hamia mwingine..Hizo ndio gharama za kuacha dhambi!..Hizo ndizo gharama za kumtii Roho Mtakatifu.
Usipotaka kuzikimbia namna hiyo na kutafuta kuombewa, au kuwekewa mikono, kirahisi rahisi tu hivyo…Utajikuta unaombewa na kila mtu na hata kuwekewa maroho mengine mabaya hata kuliko hayo uliyonayo sasa. Hali yako kila siku itazidi kuwa mbaya kwasababu umekosa maarifa ya kutosha!.
Ndugu umeyasikia/umeyasoma haya..hutasema siku ile hukuambiwa…kama hutamtii Roho Mtakatifu leo, basi yeye mwenyewe atahakikisha anakusaidia kuyatimiza maazimio yako..lakini pia kama hutatii uamuzi ni wako. Lakini natumaini utatii, na Bwana akusaidie. Hivyo kama hujaokoka au kama wewe ni vuguvugu, upo hatarini kutapikwa hivyo kabla hujatapikwa hebu fanya mageuzi haraka..Mtii leo Roho Mtakatifu kwa kuacha dhambi kwa Lazima.. baada ya kuziacha, nenda katafute ubatizo sahihi wa kuzama mwili wote katika maji na kwa jina la Bwana Yesu kulingana na Matendo 2:38, na Yule Roho Mtakatifu ambaye aliishaianza kazi njema moyoni mwako atakusaidia kufanya yale ambayo peke yako ilikuwa ni ngumu kuyatimiza, na dhambi kwako itakuwa sio kitu kigumu kukishinda kwasababu Nira ya Kristo siku zote ni laini na utapata furaha, na amani isiyoelezeka, na utaona siku zote ulikuwa wapi kuingia ndani ya Kristo…kwa raha utakayoipata na furaha..wala dhambi haitakuwa ni kitu kinachokusisimua hata kidogo.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
KWANINI AWE PUNDA NA SI MNYAMA MWINGINE?
Nini tofauti kati ya Amri, sheria na Hukumu?
TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.
KWANINI UNAPASWA UJIWEKE TAYARI SASA, KABLA YA ULE WAKATI KUFIKA?.
NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.
MAMBO MANNE,YANAYODHOOFISHA UOMBAJI WAKO.
Rudi Nyumbani:
Print this post