Nimrodi ni nani?

by Admin | 10 August 2020 08:46 pm08

SWALI: Nimrodi ni nani? Na je! Alikuwa ni mtumishi wa Mungu?

Nimrodi ni kitukuu cha Nuhu kwa kupitia  uzao wa Hamu,

Biblia inatuambia alianza kuwa mtu Hodari, na sio Hodari tu, bali alikuwa ni Hodari wa kuwinda mbele za Bwana, Mpaka enzi hizo ukatungwa msemo maarufu kwa jina lake (Soma Mwanzo 10:9),  

Hivyo aliendelea na huo uhodari wake mpaka akafikia hatua ya kuwa na nguvu nyingi za kuanza kujenga miji mikubwa, ikiwemo Babeli na Ninawi.

Mwanzo 10:8 “Kushi akamzaa Nimrodi, akaanza kuwa mtu hodari katika nchi.

9 Alikuwa hodari kuwinda wanyama mbele za Bwana. Kwa hiyo watu hunena, Kama Nimrodi, hodari wa kuwinda wanyama mbele za Bwana.

10 Mwanzo wa ufalme wake ulikuwa Babeli na Ereku, na Akadi, na Kalne, katika nchi ya Shinari.

11 Akatoka katika nchi ile akaenda mpaka Ashuru, akajenga Ninawi, na Rehoboth-iri, na Kala;

12 na Reseni, kati ya Ninawi na Kala, nao ni mji mkubwa”

Lakini japokuwa alikuwa ni Hodari, alikuwa ni mwovu katika fikra zake na matendo yake, nakala nyingi za kale zinaonyesha, hata nia yake ya kutaka kuujenga mnara wa Babeli ilikuwa ni kumlipizia Mungu kisasi, kwamba kwanini aliwaua mababu zake, hivyo akaunyanyua mnara ule juu sana kuelekea mbinguni kiasi kwamba hata Mungu akileta tena mafurukio mengine asiweze kuwaangamiza.

Lakini jitihada zake hazikufika mbali, tunajua kilichotokea ni nini baada ya pale, ni kwamba walichafuliwa lugha zao na semi, ndoto zao zote zikayeyukia palepale, Kwasababu Mungu hadhihakiwi.

 Lakini Pamoja na hayo bado tunakuja kuona Babeli iliendelea kuwepo kwa miaka mingi mbeleni, mpaka ikaja kuwa  kitovu cha machafuko yote duniani, Na ndio  hawa wababiloni baadaye wakaja kulichukua taifa la Israeli utumwani tena. Kama ulikuwa hujui ni kwamba chimbuko la ibada zote za sanamu na miungu, ilianzia huko, Hii miungu ya Rumi ya kuabudu mungu mke na katoto chake (ambayo kwa sasa wameipachika majina ya watakatifu kama Mariamu ) chimbuko lake lilikuwa ni huko,

Na ndio maana Babeli hiyo mpaka siku hizi za mwisho bado inaonekana kuishi, isipokuwa safari hii inatenda kazi  rohoni. Katika kivuli cha dini.

Sasa muhasisi wa hayo yote alikuwa huyu Nimrodi.

Biblia inasema..

Mithali 1:32 “Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza”

Usifurahie mafanikio ya kipumbavu hata kama utasifiwa na ulimwengu mzima, shetani naye alikuwa ni Hodari hivyo hivyo kabla ya kuasi, lakini ulikuwa ni uhodari unaokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

Ezekieli 28:14 “Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto.

 15 Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.

16 Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto.

 17 Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.

18 Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao.

  19 Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele”.

Nasi pia tusiige mifano hiyo, tuwe wanyenyekevu kwa Mungu, tuishi kwa kuyafanya mapenzi yake, Hilo tu linatosha Sio kila jambo linalofanywa na watu Hodari wa mataifa yaliyoendelea na sisi tuigee, Ni heri tubakie na ushamba wetu kuliko tuige utukanaji, ushoga, au upagani, au uvaaji wa mavazi yasiyo na heshima mbele za Mungu na wanadamu.

Imemfaidia nini Nimrodi kuupata ulimwengu mzima, halafu amepata hasara ya roho yake?

Bwana atusaidie.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

YEREMIA

Kuungama ni nini?

Je! msalaba kaburini una umuhimu wowote?

UMEFUMBULIWA MACHO YAKO YA KIROHO?

HERI YULE ATAKAYEKULA MKATE KATIKA UFALME WA MUNGU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/08/10/nimrodi-ni-nani/