DUNIA HII ITAHARIBIWA KABISA.

by Admin | 25 August 2020 08:46 pm08

Isaya 24:3 “Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana Bwana amenena neno hilo.

4 Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika.

5 Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele.

6 Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu”.

Nabii Isaya alipotabiri juu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo na bikira (Isaya 7:14), miaka 700 kabla ya Masihi kuja duniani, wapo watu pengine walioona kuwa hizo ni hadithi tu za kufikirikika… Alipotabiri tena juu ya mateso yake yatakayoompata (Isaya 53), nazo pia zikaonekana pengine ni habari tu, lakini wakati ulipofika, hayo yote kutimia kwa ufasaha wote, ndipo wakajua kuwa Neno la Mungu huwa halipiti.

Isaya huyo huyo aliyetabiri ujio wa Kristo kwa uvuvio wa Roho, ni huyu huyu alioonyeshwa pia hatma ya huu ulimwengu utakavyokuja kuwa siku za mwisho, na habari zake kaziandika sehemu nyingi sana kwenye kitabu hicho chenye sura 66, alionyeshwa jinsi hii dunia itakavyokwenda kuwa utupu, na kuharibiwa kabisa, jinsi jua litakavyotiwa giza, jinsi watu watakavyoadimika kama dhahabu duniani, na kibaya zaidi alionyeshwa fedha ya mtu wakati huo haitafanya kazi yoyote, umaarufu wa mtu utakuwa hauna maana, biashara za mtu zitakuwa ni kama takatakata, elimu ya mtu haitafanya kazi..tajiri na maskini wote watakuwa wakiomboleza sawa.

Na nyakati zenyewe ndio hizi tunazoishi mimi na wewe, kila mtu analijua hilo, hata ukimuuliza mtoto mdogo atakuambia, hizi ni nyakati za mwisho, watu wengi wanaposikia maneno haya wanapuuzia wakidhani hichi ni kama kile kipindi cha mitume..Ndugu hichi sio kipindi cha mitume.. Fuatilia mambo yanayoendelea duniani hata kupitia mitandao ndipo utakapojua kuwa tunaishi nyakati nyingine.

Bwana Yesu alisema hivi..

“Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;

33 nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.

34 Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia” (Mathayo 24:32).

Sasa kama wewe ni msomaji wa Biblia utajua kuwa Mtini unafananishwa na Taifa la Israeli (Yeremia 24), na wakati ule Israeli ilikuwa bado haijachipua (yaani haijawa taifa), ilipitia miaka zaidi ya 2,500 tangu wachukuliwe utumwani Babiloni, na ulipofika mwaka 1948, Israeli ikachipuka tena na kuwa taifa kwa mara ya kwanza,..Na tunajua kabisa agenda ya Mungu ya wokovu itamalizia tena na Israeli pale Yerusalemu.

Hivyo tangu huo wakati Bwana alisema kizazi hiko, (yaani kilichoshuhudia Israeli kuchupuka tena), hakitapita mpaka hayo yote, kutimia,..Mambo yote aliyoyazungumzia katika Mathayo 24, hadi kurudi kwa pili kwake,..Na kizazi huwa hakizidigi miaka 120, sasa piga hesabu hapo, tunaishi katika wakati gani.. (Hatujui siku wala saa lakini tunayajua majira).

Sikuzote, kiwango chako cha maarifa kuhusu Mungu, ndio kinachoelezea maisha ya kiroho unayoishi sasa hivi, kama jicho lako bado halioni kuwa tunaishi katika majira ya unyakuo, na kwamba huu ndio ule wakati ambapo watu watadhanishia mbona ni amani, na salama, na kumbe ule uharibifu unakuja kwa ghafla (1Wathesalonike 5:3)..Kama ilivyokuja Corona kwa ghafulani pasipo ulimwengu kujiandaa…Ndicho kitakachoitokea dunia kipindi sio kirefu.

Sijui kama hilo unalijua ndugu yangu, kanisa hili linaitwa Laodikia, (Sio dhehebu linaloitwa Laodikia! Hapana!..Bali ni hali ya kanisa kwa ujumla inayofananishwa na Kanisa la Laodikia la Nyakati za kwanza, kasome Ufunuo 3:14), na ndio kanisa la mwisho la 7, na hakutakuwa na kanisa lingine baada ya hili, niambie ni dalili ipi ambayo haijatimia Yesu aliyoirodhesha kwenye Mathayo 24.

Internet imeweza kurahisisha mambo, siku hizi haihitaji mtu aende tena kwenye mikutano ya Injili asikie mahubiri, pale pale alipo hata kama ni kijijini akiwa chumbani mwake Injili inamfikia, utasema Injili haijahubiriwa dunia nzima leo?..

Shetani anataka watu waendelee kufikiria hivyo hivyo, kwamba bado sana, anataka watu waangalie upepo wa dunia unavyokwenda, lakini wasiangalie biblia inasema nini kuhusu siku hizi. Usipokuwa mvivu kusoma biblia ndipo utakapojua ni kwa jinsi gani tunaishi katika nyakati za hatari kushinda zote ambazo zilishawahi kupita katika historia.

Hivyo huu ni wakati wa kuamka usingizini..

Waefeso 5:14 “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza”.

Kama bado hujaokoka, au umeokoka lakini bado mguu mmoja nje mwingine ndani, Embu anza, kuyaangalia upya maisha yako ya rohoni ndugu, Je! Yesu amekuokoa kweli kweli? Kama sio, basi huu ndio wakati, na sio kesho, unachopaswa kufanya ni kuamua kutubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha na kutozifanya tena, na kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji tele (Yohana 3:23), na kwa jina la YESU KRISTO sawasawa na Matendo 3:38,8:16 na 10:48 Upate ondoleo la dhambi zako.(Maagizo hayo ni muhimu sana!). Na Roho Mtakatifu atakuongoza katika kuyaelewa maandiko.

Na kuanzia hapo, anza kuishi maisha ya kama mtu unayemngojea Bwana Yesu kwasababu nyakati hizi, sio za kubembeelezewa wokovu tena, ni kubutuka haraka na kuishindania Imani.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

KUOTA UNAKOJOA KITANDANI.

MAMBO MENGINE HAYATOKI ISIPOKUWA KWA KUFUNGA.

NI WAKATI WA KUJIPIMA, WEWE KAMA MTUMISHI WA MUNGU!

NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME

MISTARI YA BIBLIA YA UPONYAJI.

MANA ILIYOSHUSHWA KUTOKA MBINGUNI.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/08/25/dunia-hii-itaharibiwa-kabisa/