Mungu anaposema yeye ndiye achunguzaye “viuno na mioyo” anamaanisha nini?

by Admin | 29 September 2020 08:46 pm09

SWALI: Mungu anaposema yeye ndiye achunguzaye “viuno ya mioyo” anamaanisha nini, Je! hivyo viuno ni vipi? Kama tunavyovisoma katika vifungu vifuatavyo;

Yeremia 11:20 “Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki, ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu”.

Yeremia 17: 10 “Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake”.

Yeremia 20: 12 “Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu”.

Zaburi 7: 9 “Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki”.

Ufunuo 2:22 “Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;

23 nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo.

Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake”.

Ukisoma pia Mithali 23:16 , na Ayubu 31:19 inazungumzia maneno hayo hayo;


JIBU: Mara nyingine biblia inapolitaja Neno viuno haimaanishi tu hivi viuno vya miili yetu tunavyovivalia mikanda, hapana, bali viuno sehemu nyingine linatumika kumaanisha NIA au WAZO, la mtu. Mungu kabla hajambariki mtu au kumuhukumu au kumsamehe huwa anatazama vitu hivyo viwili, cha kwanza ni Moyo na cha pili ni Nia.

Kwamfano, Mungu anaweza kumsamehe mtu dhambi zake bila hata ya kuzungumza maneno yoyote kwenye kinywa chake kuonyesha anaomba msamaha, Yaani ule moyo tu wa kujutia dhambi zake, moyo wa kuugua, moyo wa kusema kosa hili sitakaa nilirudie tena, siku baada ya siku anajutia makosa yake, na hataki kuyatazama wala kuyarudia tena, hiyo tayari ni toba inayozungumza sana mbele za Mungu kuliko sala za toba elfu mtu anazoongozwa kila siku na huku hana majuto na dhambi zake.

Jambo kama hilo utaliona kwa Yule mwanamke kahaba, aliyekwenda kumlilia Yesu, utaona hakuzunguza Neno lolote lakini Bwana Yesu alimwambia umesamehewa dhambi zako. (Luka 7:37-48)

Vilevile Mungu huwa anachunguza Nia, kwa mfano wengi wetu tunamuhukumu Yuda kama ndiye aliyempeleka Yesu msalabani, lakini ukisoma pale utaona Yuda hakuwa na Nia ya Bwana Yesu kufikishwa katika mateso na kusulibiwa na ndio maana akawaomba watakapomchukua wasimtendee dhara lolote (Marko 14:44), kwani yeye lengo lake lilikuwa ni kupata pesa tu..Lakini alipoona wale watu wamevuka mipaka, mpaka kwenda kumsulibisha alijuta kwa kulia sana, hadi ikamfanya aende kujinyonga, kwa madhara aliyosababisha, Hivyo Mungu anayechunguza Nia hatamuhukumu kwasababu alimpeleka Yesu msalabani bali atamuhukumu kwa kosa lingine la kutokuwa na moyo mkamilifu kwake kama ilivyokuwa kwa mitume wenzake.

Huo ni mfano tu,

Hivyo nasi tunapaswa tuwe makini sana, usiende kuzini ukamwambia Mungu nilipitiwa, yeye hashawishiwi kwa maneno , anachunguza moyo na Nia ya mwanadamu zaidi ya fikra zetu. Hivyo tusijidanganye tuna la kujitetea mbele zake, hata Siku ile ya Hukumu (Anachunguza viuno vyetu). Halikadhalika hata ukitenda tendo la haki, huna haja ya kumwambia Mungu, kumbuka hiki kumbuka kile, yeye anajua yote (Mhubiri 5:8).

Bwana atusaidie,

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Malaika wa maji ni yupi na Je kuna aina ngapi za malaika?

JINSI MUNGU ANAVYOIPIGA NA KUIPONYA AFRIKA.

BWANA WA MAJESHI.

JINSI YA KUSOMA BIBLIA.

Nini maana ya Usiwe mwovu kupita kiasi? (Mhubiri 7:17)

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/09/29/mungu-anaposema-yeye-ndiye-achunguzaye-viuno-na-mioyo-anamaanisha-nini/