AKIJUA YA KUWA ANA WAKATI MCHACHE TU”.

by Admin | 4 October 2020 08:46 pm10

Ufunuo 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu”.

Shalom, katika mistari hiyo biblia inatuonyesha kuwa shetani naye anayo kalenda ya muda kichwani pake. Aishi hoe hae tu, kuna kipindi alifanya kazi zake akijua bado kuna muda, lakini kuna wakati ulifikia kwa jinsi mambo yanavyokwenda, na mabadiliko aliyoyaona akajua kabisa kweli  hana  muda tena hapo wa kuchezea, muda aliobakiwa nao ni mchache.

Na sikuzote mtu mwenye majira ya muda kichwani, hata utendaji kazi wake unatofautiana kulingana na majira husika, Kwamfano, wanariadha, pale wanaposikia kengele imelia ya “mzunguko”  wa mwisho, utaona badala wapunguze mwendo kwasababu wamechoka,  kinyume chake utaona ndio wanaongeza kasi, kana kwamba ndio wameanza riadha, kwasababu wanajua hicho ndicho kipindi cha lala salama.

Mwanafunzi ambaye amebakisha wiki moja au mbili mpaka afanye mtihani wake wa kuhitimu, utaona hata usomaje wake katika kipindi hicho unabadilika, ataanza kuzingatia masomo, atakuwa tayari kukesha kila siku kwenye kusoma, mambo ambayo huko nyuma alikuwa hayafanyi kwa nguvu hizo.

Wachezaji mpira, utaona zinapokaribia dakika 5 mpira kuisha, utaona aina ya uchezaji wao nao unabadilika kwa pande zote mbili, ule upande uliofungwa utaona ndio unaongeza mashambulizi zaidi hata Yule kipa ambaye anakaa pale golini muda wote, ataondoka kwenda kuongeza mashambulizi kwa  upande wa pili, ili tu kuhakikisha wanarudisha magoli waliyofungwa.

Halikadhalika, ule upande uliofunga nao, utaacha kupeleka mashambulizi upande wa pili, utaona kwanza kikosi chote kinarudi nyuma, ili kulinda ushindi wao, adui zao wasirudishe magoli. (Sasa huo ni mfano tu, haimaanishi kila kinachofanyika kwenye hiyo michezo kipo sawa).

Ndivyo ilivyo kwa shetani wakati huu wa siku hizi chache alizobakiwa nazo, anaelewa hakuna muda tena wa kuchezea, hivyo kama ni mpira anaucheza kwa nguvu zote, ikiwa umemfunga (yaani umeokoka), atahakikisha mashambulizi atakayokuletea ni mazito, Na kama wewe ni mwenye dhambi,(hapo ni sawa na amekufunga) basi atahakikisha ulinzi atakaoweka ili usiufikie wokovu unakuwa ni mkubwa sana.

Ndugu, vizuizi shetani alivyonavyo leo, watu wasimfikie Mungu ili watubu dhambi zao, sio kama alivyokuwa navyo zamani, na hiyo yote ni kwasababu anajua muda wake ni mchache sana, anajua hivi karibuni mambo yote yanakwenda kuisha, atashikwa na kutupwa katika lile ziwa la moto..Na ndio maana anakusonga uwe busy ni mambo ya kidunia usipate muda wa kumtafakari Mungu,

Anakusonga na Ma-movie na Ma-series kutwa kuchwa uyawaze hayo,  ili muda wako wote uyawaze hayo usipate nafasi ya kuyatafakari maandiko, mwisho ukukute kwa ghafla, ufe uende kuzimu, au uukose unyakuo.

Anakusonga kwenye anasa na starehe, na pombe, na simu, na magroup ya kidunia, ili muda wako mwingi uumalizie huko, usahau kuwa muda uliobakiwa nao ni mchache, kwamba ni wajibu wako sasa kwa muda uliobakiwa nao hapa duniani ni kuhakikisha mbingu huikosi.

Shetani anajua huu ni  muda wa nyongeza tu, dakika 90 zenyewe zilishaisha, lakini sisi tunaishi kama vile ndio tupo dakika za 5 za kwanza, tunasubiria dalili zipi tena ndio tuamini kuwa Yesu yupo mlangoni? Mapigo kama haya ya Corona ndio zile tauni ambazo zilitabiriwa zitaipiga dunia  siku za mwishoni kabisa (Luka 21:11),  na cha kuogopesha zaidi biblia inasema, pale watakaposema mbona kama kuna Amani, ndipo hapo uharibifu utakapowajia kwa ghafla,

Siku moja utaamka asubuhi, utaiona dunia ni nzuri, jua linachomoza kama kawaida, jua linazama, uchumi wa nchi unaimarika, mikataba ya amani inasainiwa, sayansi inazidi kusitawi na kufanya maisha kuwa marahisi zaidi,  una afya njema, una amani, lakini usiku huo huo, kumbe ndio unyakuo unapita..

Hapo ndipo wengi wataanza kujutia muda wao wameutumiaje hapa dunia. Hivyo tunapoina neema ya Kristo inalia ndani yetu leo, tujitahidi tuipokee, kwasababu muda uliobakia kweli ni mchache, Bwana Yesu alisema hivyo, shetani naye anasema hivyo moyoni mwake, na anataka iwe ni siri yake peke yake, ili atushambulie chap chap atumalize aishinde yeye. Lakini sisi tunapaswa tumshinde kwa kuutafuta wokovu kwa bidii.

Hivyo kama wewe  ni mwenye dhambi, leo fanya uamuzi, Tubu dhambi zote kwa kumaanisha kuziacha, kisha, tafuta ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, kisha baada ya hapo utapokea Roho Mtakatifu, ambaye ndio muhuri wa Mungu kwako (Waefeso 4:30), kukulinda, kukuongoza, kukufariji, na kukufundisha, hata siku ya unyakuo itakapofika.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

HERODE NA PILATO, MAADUI WAWILI WAPATANA.

Baradhuli/Mabaradhuli ni nini au ni nani kwenye biblia?

Juya ni nini kwenye biblia? (Mathayo 13:47)

MATUNDA 9 YA ROHO MTAKATIFU

KALAMU YA CHUMA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/04/akijua-ya-kuwa-ana-wakati-mchache-tu/