WAENDEE WANA WA ISAKARI, UWE SALAMA.

by Admin | 14 October 2020 08:46 pm10

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya uzima, na leo tena kwa neema za Bwana tutajikumbusha juu ya mambo ya msingi ya kuzingatia siku hizi za mwisho

Tukisoma biblia tunaona Yakobo alikuwa na wana 12, na kila mmoja alikuwa na tabia yake ya kipekee, Yusufu alikuwa na ya kwake, Yuda alikuwa na ya kwake, Benyamini alikuwa na ya kwake, na wengine wote. Vivyo hivyo na uzao wao mbeleni nao pia ukaja kuwa na tabia zao za kipekee kujitofautisha na kabila lingine, kabila la Yuda lilikuwa na tabia yake, kabila la Lawi lilikuwa na ya kwake n.k.

Sasa leo hatutaangalia tabia za makabila yote, lakini tutaangalia tabia la kabila la Isakari, ni nini walikuwa nacho, Biblia inatuambia ilipofika wakati Mfalme Sauli amekufa, na anatafutwa mrithi wa ufalme wake pale Israeli, kulihitajika hekima katika kuchagua, ikumbukwe kuwa hapo kabla kulikuwa na mvutano Fulani wa makabila hayo hususani, lile la Benyamini ambalo mfalme Sauli alitokea huko, lenyewe lilikuwa linataka warithi waendelee kutokea katika uzao wa Sauli kwasababu Sauli alitokea kwenye kabila hilo, wakati makabila mengine yanamtaka Daudi ayamiliki.

Hivyo katika mazingira kama hayo, kulihitajika watu wenye akili ambao wanaweza kutambua majira na nyakati kwa wakati huo, kwamba ni nani anapaswa awe mfalme. Sasa kwa kuwa Israeli ilikuwa inajua wanapofikia saa kama hiyo wamtafute nani na nani, ndipo wote wakawaendea wana wa Isakari, na kuwasikiliza wanasema nini.

Sasa ili kufahamu habari yote, unaweza kwenda kusoma 1Nyakati 11-12 yote, hapa tutakiweka kile kifungu tu kinalielezea kabila hili la Isakari,

1Nyakati 12:32 “Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili NA NDUGU ZAO WOTE WALIKUWA CHINI YA AMRI YAO”.

Unaona, Israeli kabla hawajafanya uamuzi wowote, waliwafuata kwanza hawa wana wa Isakari, ili kuuliza ni nini wanachopaswa wafanye kwa wakati huo, wasije baadaye kuingia matatizoni, walikuwa wapo tayari kujiweka chini ya amri yao, kama maandiko yanavyotuambia, haijalishi watakachoambiwa kitakuwa ni kinyume na matarajio yao..Na hiyo yote ni kwasababu waliwatambua kuwa Mungu aliwapa akili ya kujua nyakati na majira, kuijua torati, na kuisikia sauti ya Mungu inataka nini.

Ulipokuwa unafika wakati kama huo, makabila yote yaliondoa tofauti zao, wakasikilize ni nini Mungu anawaonya kupitia wana wa Isakari. Sio kwamba makabila mengine yalikuwa madhaifu hapana, biblia inasema kabila la Yuda lilishinda zaidi ya yote, na Nyumba ya Yusufu ilikuwa ni kuu. Lakini kuhusu hatma ya maisha yao, ya wakati ule na mbeleni,  Isakari walihitajika sana. Na hiyo iliisababishia Israeli, ikae katika Nuru wakati wote.

Vivyo hivyo katika agano jipya, hatupaswi kuishi tu, ilimradi tunaishi, sio kusema nimeokoka tu, sio kusema Bwana atanibariki tu, sio kusema twende kanisani tutimize wajibu kama kawaida, hiyo peke yake haitoshi, tunapaswa tutafute  ni nini Mungu anasema juu ya wakati huu na majira haya; Lakini cha kusikitisha ni kuwa Bwana Yesu alisema sisi ndio tulio nyuma kabisa katika kutambua majira tuliyo nayo, na kibaya zaidi, tunafanya hivyo kwa unafiki, na sio kwamba hatufahamu.

Luka 12:54 “Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.

55 Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.

56 Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya”?

Unaona? Watu wa kipindi kile kwasababu waliipuuzia kujifunza juu ya nyakati zao na majira yao, walishindwa hata kujua kuwa wanatembea na Mungu mwenyewe duniani katika umbo la kibinadamu, mpaka sisi tunasema laiti tungekuwa kipindi chao tungelala na kutembea na Bwana Yesu wakati wote..

Lakini na wao pia  huko walipo leo hii wanatuona sisi wa nyakati hizi za mwisho, ni jinsi gani tupo karibu sana na ule mwisho, wanasema laiti na wao wangekuwepo wakati wetu wangeishi maisha ya kama ya wapitaji tu hapa duniani, kwasababu muda tuliobakiwa nao ni mchache, Yesu yupo mlangoni kurudi na unyakuo ni wakati wowote…

Lakini ni kwanini  tunaishi kama tunavyoishi leo hii, ni kwasababu, hatujui majira tuliyopo. Hatujui kuwa tangu kipindi cha Bwana Yesu hadi unyakuo kulitakiwa kupite kipindi cha makanisa saba, na kwamba sita ya kwanza yameshapita, na hili tunaloishi ndilo la mwisho la 7, lijulikanalo kama Laodikia sawasawa na Ufunuo 3:14 na hakutakuwa na kanisa lingine zaidi ya hili, sisi ndio tutakaoshuhudia tukio zima la Unyakuo. Kwamba lile juma la 70 la Danieli lipo karibuni kuanza kuhesabiwa.

Hatujui kuwa hii neema itakwenda kurudi Israeli siku za hivi karibuni, kama unabii wa biblia inavyotabiri, kwasababu tayari limeshakuwa taifa huru, na hivyo kinachosubiriwa ni unyakuo tu, Mungu akawarudie watu wake kama alivyowaahidi katika siku za mwisho.

 Hatujui kuwa, roho ya mpinga-Kristo inafanya  kazi tayari katikati ya madhehebu mengi, na kama hatuna macho ya rohoni, chapa tutaipokea tu pasipo hata sisi wenyewe kujua. Kwa ufupi hakuna dalili ambayo haijatimia  inayozungumzia juu ya nyakati hizi za mwisho tukiachilia mbali kuibuka kwa wimbi la makristo na manabii wa uongo, biblia ilizungumzia Tauni(Corona), mafundisho potofu, na kuachiliwa kwa nguvu ya upotovu, ili watu waendelee kuamini uongo wapotee waende kuzimu n.k.

Embu tujitathimini maisha yetu tena, Je! bado tupo katika mstari au tunayumba yumba, Je! tunafahamu majira na nyakati kama wana wa Isakari?, au tupo tu, tunasubiria mambo hayo yatukute kwa ghafla tu,.tubakie kusema laiti tungejua..Bwana atusaidie tusifike huko wakati wa kujua ndio huu. Tunaishi katika saa ya kurudi kwa pili kwa Kristo, muda tuliopewa ni wa nyiongeza tu.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

UHURU WA ROHO.

NJONI, NUNUENI MLE NA MNYWE.

FAIDA ZA KUFUNGA NA KUOMBA.

ANGALIA UZURI WAKO, USIGEUKE KUWA KITANZI CHAKO.

KWA KUWA TUMEKABIDHIWA MAUSIA NA MUNGU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/14/waendee-wana-wa-isakari-uwe-salama/