KUNA UMUHIMU WA KUWA MTU WA KURIDHIKA.

by Admin | 27 October 2020 08:46 pm10

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Karibu tujifunze biblia,

Neno la Mungu linasema..

1Timotheo 6:7 “Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;

8  ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo”..

Hili ni moja la andiko linalochukiwa na wengi..Hususani watu wenye uchu wa kupata mali. Lakini wanalisahau pia hili neno..

Mhubiri 5:10 “Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili”.

Maana yake ni kwamba kama wewe ni mtu wa kuzipenda fedha mno, usifikiri utafika wakati utasema sasa sizihitaji tena.. Hata upate nyingi kiasi gani, bado utazidi kuzitafuta tu!.. Hekima ndio inasema hivyo..Siku zote mwenye fedha nyingi ndio yupo busy kuzitafuta kuliko yule asiyekuwa nazo. Matajiri wote wakubwa ulimwenguni ndio wapo bize kuliko watu wasio na fedha nyingi.

Ndivyo hekima inavyosema.. Mhubiri 5:12 “Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi”.

Rafiki yangu mmoja mwenye kazi nzuri na mshahara mzuri sana, (ambaye ni kama boss tu huko kazini kwake) siku moja alinifuata huku akiwa amenyong’onyea, isivyo kawaida..Wakati naanza kuzungumza naye tu, akaniambia leo nimejifunza kitu kikubwa sana nikiwa kazini,

Akaniambia kazini, mahali anapofanya kazi kuna watu ambao kazi yao ni kufanya usafi, ambao mishahara yao ni laki moja, aliyezidi sana analipwa laki moja na nusu. Akasema kilichomshangaza zaidi ni kwamba siku hiyo kawakuta wamejikusanya wanasheherekea na kufurahi na kucheka pamoja mwisho wa mwezi, hivyo wamenunua soda na kukata keki, wakifurahi. Nikazidi kumuuliza kwani wao kufanya hivyo kumekuathiri nini wewe?. Akasema alipowaona wanafurahi huku wanamishahara midogo, ambayo kwa kiwango hicho, cha laki moja yeye anaweza kukitumia kwa siku moja tu na kinaweza kisimtoshe…..Akashangaa inakuwaje wao wenye mishahara midogo wana furaha na raha, na yeye hana raha na ana mshahara mkubwa!….. akasema “Hilo jambo kwa kweli limenigusa sana na nahisi kuna kitu natakiwa nijifunze”.

Sasa huyu alikuwa hajui kama hicho anachokisema tayari biblia ilishakise,a miaka mingi sana huko nyuma …. Mhubiri 5:12 “Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi”.

Ndugu hatuna budi kila siku kujifunza kuridhika… Kwa kusema hivi sio kwamba nasema tuwe masikini au nauunga mkono umasikini hapana!..Ni mapenzi ya Mungu tutajirike, lakini hata katika utajiri pia tunaweza kujifunza kuridhika.

Kuridhika katika hali ya utajiri ni huku… “Aidha siku imepata kingi au vichache, kumshukuru kwako Mungu kupo palepale, kumfurahia kuko pale pale, kutenda kwako mema kupo pale pale”..Kwaufupi moyo wako haupo kwenye mali kabisa.. Na hata ukikosa au ukipata, vyote kwako ni sawasawa tu wewe utabaki kuwa yule yule, kama Ayubu.

Ayubu 31:25 “Kama nilifurahi kwa kuwa mali yangu yalikuwa mengi, Na kwa sababu mkono wangu umepata vitu vingi”

ZIFUATAZO NI FAIDA CHACHE ZA KURIDHIKA.

  1. Unapata nafasi ya kumtafakari Mungu:

Hii ni faida ya kwanza ya kuridhika, unaporidhika unakuwa unafungua mlango  mkubwa katika ufahamu wako wa kufanya jambo lingine ambalo linaweza kuwa la muhimu. Na jambo la muhimu kuliko yote ni muda wa kumtafuta Mungu. Lakini unapoingia katika tamaa ya mali zinazotokana na kutokuridhika, kamwe muda wako siku zote unakuwa umebana, hutapata hata nafasi ya kushika biblia, wala kulisoma Neno lake.

  1. Unapata Furaha:

Unaporidhika, na huku Mungu akiwa moyoni mwako, utapata furaha ya kudumu, kwasababu hutaingia kwenye mashindano na Mtu na wala hutaendeshwa na mali, hivyo hutakuwa mtumwa wa vitu hivyo, na hivyo utakuwa ni mtu wa furaha siku zote.

  1. Utajiepusha na Mitego na Vitanzi vya shetani:

Biblia inasema katika hiyo 1Timotheo 6: 9  “Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika MAJARİBU NA TANZİ, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.

Wote wanaojiingiza katika mauaji, ni kwasababu ya tamaa ya mali, inayotokana na kutokuridhika na hali walizonazo, wanaojiingiza katika ukahaba na wizi ni kwasababu ya tamaa ambayo inatokana na kutokuridhika..

  1. Hutafarakana na Imani:

1Timotheo 6: 10  “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo WAMEFARAKANA NA IMANİ, na kujichoma kwa maumivu mengi”.

Ukiridhika na mshahara, hutamdhulumu mtu wala kusaka njia za kando kando kutafuta mali..Na hivyo Imani yako haiwezi kuathirika.

Kumbuka biblia inatuambia kwamba “Hatukuja na kitu wala hatutaondoka na kitu” na pia Bwana Yesu alisema… “itatufaidia nini (au kwa lugha rahisi, tutapata faida gani), tukiupata ulimwengu mzima halafu tukapata hasara ya nafsi zetu”?. Hilo ni swali tumepewa mimi na wewe na Bwana, la kutafakari!..

Bwana akubariki.

Kama hujampokea Yesu lakini upo bize na shughuli za ulimwengu huu, nakushauri, simamisha kwanza shughuli zako, tafuta uhakika wa usalama wa roho yako, ukishaupata rudi endelea na shughuli zako kama zinampendeza Mungu.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

TAFUTA KUWA NA AMANI NA WATU WOTE.

SALA YA ASUBUHI

Jiepushe na tamaa ya Mali/kupenda fedha.

JE! MTUMISHI KUTOKUWA NA FEDHA NI ISHARA KUWA KUNA TATIZO KATIKA IMANI YAKE?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/27/kuna-umuhimu-wa-kuwa-mtu-wa-kuridhika/