USIOMBE MAOMBI YASIYOKUWA NA MAJIBU NA WALA USIMTUKANE MUNGU.

by Admin | 3 November 2020 08:46 pm11

Luka 23:42  “Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi”.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia.

Kama tunavyojua wengi wetu, kwamba Kristo hakusulubiwa peke yake pale Kalvari, bali alisulubiwa pamoja na wanyang’anyi wengine wawili. Na wote walikuwa wametundikwa msalabani kama Bwana, kufunua kuwa na wao pia wapo katika mateso na uchungu. Lakini kilichowashangaza  zaidi ni kuona anayejiita ni mkombozi naye pia yupo katika mateso kama wao. Katika hali ya kawaida ni jambo linalochanganya kidogo. Hivyo kila mmoja akawa na neno la kumwambia Bwana Yesu.

Wa kwanza akatangulia kumwambia Bwana,……

“Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini YESU HAKUMJIBU NENO. (Luka 23.39 )”

Kitendo tu cha kuanza kwa  kumwambia Bwana…wewe si Kristo?..hicho tayari ni kitendo cha kukosa heshima!..na hakujua kama tayari kamtukana Mungu, kwa kusema tu hivyo..

Mfano kamili wa watu wengi wa siku hizi za Mwisho, Wapo katika dimbwi kubwa la matatizo, na shida lakini watasimama mbele za Mungu, na kusema “kama wewe Mungu upo na una nguvu, mbona huniokoi na shida hizi” na pia “mbona baadhi ya watu wako wana shida nyingi, waokoe watu wako kwanza na shida zao na ndio utusaidie sisi”.

Hawajui kwamba tayari wanamtukana Mungu kwa hayo maneno. Sasa watu wa namna hii, kamwe wasitazamie kupokea majibu yoyote kutoka kwa Mungu, kwasababu wamekosa unyenyekevu…

Ndio maana unaona huyo mnyang’anyi alitazamia atajibiwa na Bwana kwa kejeli zake, lakini Kristo hakutoa neno lolote hata la kumwambia atubu!

Lakini tukiendelea na Mtu wa pili, ambaye naye pia alikuwa anaswali kama hilo hilo kichwani?, isipokuwa huyu alituliza akili yake na kufikiri mara mbili, na kujua kuwa yaliyompata amestahili kupokea malipo yake, na kwamba Kristo yaliyompata hakustahili, maana yake ni kwamba amejitoa kusulubiwa kwaajili ya makosa ya watu wengine, na si kwa makosa yake….kwa kutafakari sana..roho ya unyenyekevu ikamwingia, na ya kuomba msaada..

Luka 23:40  “Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?

41  Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.

42  Kisha akasema, EE YESU, NİKUMBUKE UTAKAPOİNGİA KATİKA UFALME WAKO.

43  Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi”

Hebu mtafakari huyu mtu wa pili, Hata hakuomba kushushwa msalabani aendelee na maisha yake, hakumwomba Yesu amshushe arudi akaione familia yake, hakuomba Yesu amwokoe pale msalabani arudi kwenye biashara yake, hakuomba Yesu amwokoe pale msalabani ili asiendelee kuteseka na maumuvi ya misumari…lakini alimwomba Yesu UZIMA BAADA YA KIFO. Alikikubali kifo, lakini aliomba tu uzima baada ya hicho kifo. Alisema nitastahimili shida ninayoipata sasa, nikipata msamaha wa kushushwa hapa msalabani sawa, nisipopata pia ni sawa, nitavumilia mateso, lakini tu, niupate huo UZIMA WA MILELE, baada ya kufa kwangu. Huyo pekee yake ndiye Kristo aliyemjibu!.

Lakini yule wa Kwanza hakujibiwa Neno hata moja. Na matokeo yake alikufa katika mateso yake na akakosa vyote, akakosa maisha ya dunia aliyokuwa bado anayatamani, na vile vile akakosa uzima baada ya kifo.

Ndugu yangu, huu sio wakati wa kumfuata Kristo ili upate MALI, na huku huna uzima wa milele moyoni mwako..Kristo hatakujibu chochote!..Unapitia shida sasa za kidunia, sio wakati wa kulia uondolewe kwenye hizo shida huku shida ya roho yako bado ipo, huku hutaki kusikia hata habari za Neno lake, Ukisikia habari za Yesu kwako ni habari za kupoteza muda tu, comedy zinazolikebehi Neno lake ndizo zinazokuchekesha… hapo usitazamie kujibiwa chochote.

Tafuta uhakika  kwanza wa uzima wa maisha baada ya haya kuisha, Ndio kitu cha muhimu kwa sasa. Ukikimbilia kuomba msaada wa mambo ya kidunia, kuna uwezekano mkubwa usikipate hicho unachokitafuta na ukafa katika shida zako, na ukakosa vyote (ukakosa Uzima wa Milele pamoja na Mali unazozitafuta).

Mathayo 6: 33  “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa”.

Leo umesikia ujumbe huu, pengine ulikuwa unamtukana na kumdhihaki Mungu pasipo kujua..Upo kwenye shida kweli lakini umekuwa mtu wa kulalamika mpaka kufikia kumdhihaki Mungu… ndio maana leo umekutana na ujumbe kama huu ni kwasababu Kristo bado anakupenda, ndio maana bado hujafa..Upo hapo msalabani umening’inia na shida zako, zinakutesa kweli, unatamani kutoka hapo…Usikimbilie kutafuta msaada wa kutoka hapo kwanza, kwasababu kwa dhambi zako umestahili kuwepo hapo ulipo…Unachopaswa kufanya sasa, ni kuanguka chini, kwa unyenyekevu na kutubu na kumwomba Bwana Yesu msamaha kwa dhambi zako, na kumwambia kuanzia leo nakufuata naomba unipe uzima wa milele…Hata kama usiponitoa katika haya mateso ninayopitia sasa, naomba unipe UZİMA WA MİLELE,  hata kama nikifa leo pasipo kupata chochote katika haya maisha naomba Uzima wa milele baada ya kifo..hicho ndio cha kwanza tunachokihitaji sisi.

Ukiomba maombi ya namna hiyo Roho Mtakatifu atashuka ndani yako kukupa jibu la maombi yako, amani ya ajabu itashuka ndani yako, na utaona akili yako imebadilika na kuwa kama ya Bwana Yesu, kiasi kwamba hizo shida zitakuwa sio kitu kwako, kwajinsi hiyo furaha itakavyokuwa kubwa ndani yako.

Lakini kwanza mpokee Kristo katika maisha yako, na tubu…Na pia kama umetubu hakikisha unatafuta ubatizo sahihi, ambao ni wa maji tele (Yohana 3:23) na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38) kukamilisha wokovu wako.

Na pia kama utapenda kushare ujumbe huu na wengine, tunaomba usiondoe chochote, ikiwemo anwani ya www wingulamashahidi org pamoja na namba zetu hizi 0789001312.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

FAIDA ZA MAOMBI.

NAWAAMBIA MAPEMA!

UFUNUO: Mlango wa 1

UNAZO KILA SABABU ZA KUMSHUKURU MUNGU

KUNA UMUHIMU WA KUWA MTU WA KURIDHIKA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/03/usiombe-maombi-yasiyokuwa-na-majibu-na-wala-usimtukane-mungu/