NAWAAMBIA MAPEMA!

NAWAAMBIA MAPEMA!

Jina la Bwana wetu Yesu, libarikiwe.

Yapo mambo mengi ambayo yatawafanya wanadamu wengi wasiurithi uzima wa milele siku ile. Wakidhani wapo sawa na Mungu, na kwamba wanampendeza Mungu lakini itakuwa kama jambo la kuwashangaza kwamba wameukosa uzima wa milele.  Na hilo si lingine zaidi ya kuukosa utakatifu, biblia inasema katika Waebrania 12:14 kuwa…“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”. Maana yake pasipo huo, haijalishi tunaona maono, haijalishi tunahubiri sana, haijalishi tunatoa sadaka sana, haijalishi tunatoa pepo wengi na kufanya miujiza…bado hatutamwona Mungu.

Fadhili za Mungu huwa zinawalewesha wengi.. Ndugu hata kama utalitukana jina la Mungu leo, hiyo haimfanyi Mungu kukunyima chakula au kutokukupa riziki, hata kama ukiwa mchawi haimfanyi Mungu kutokuangazia jua lake kwasababu fadhili zake ni za milele, na yeye hana upendeleo..anawanyeshea mvua waovu na wema, anawaangazia jua lake waovu na wema.. Hata yule mchawi mwovu kuliko wote anampa uzao, na tena hata katikati ya huo uzao wake wanaweza kutokea watumishi wa Mungu. Lakini pamoja na fadhili zote hizo za Mungu haimaanishi ndio tiketi ya kumwona Mungu siku ile..

Unapoumwa na kumwomba Mungu akuponye, na akakuponya hiyo haimaanishi kwamba ndio upo sawa na Mungu na kwamba hata ukifa leo utaingia mbinguni, Kama ni mtumishi unapomwombea mtu na akapona au unapotoa pepo na likatoka, huo sio uthibitisho kwamba Mungu anapendezwa na wewe…

Vile vile unapopitia shida na ukaona mkono wa Mungu umekuokoa katika hiyo shida…huo sio uthibitisho kwamba Mungu anafurahishwa na wewe ndio maana kakuokoa… anachokufanyia wewe ndicho anachowafanyia mamilioni ya watu duniani kote..na wengine hata sio wakristo anawaokoa kwa ushuhuda mkubwa. Kama unafikiri nakudanganya, tafuta mtu yeyote ambaye sio mkristo kabisa, mtu wa makamo mwulize ni tukio gani ambalo hutalisahau katika maisha yako, ambalo unaamini ni Mungu alikutendea..Utasikia shuhuda atakazokupa!…Hapo ndipo utakapojua kuwa Mungu hanaga upendeleo wa kuwapendelea watu wake tu!..

Hivyo fadhili za Mungu, zisitupumbaze na kujiachia katika dhambi, tukijitumainisha kuwa siku ile tutamwona Mungu…

Hebu yatafakari haya maneno ya Bwana..

Mathayo 7:21  “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22  Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23  Ndipo NITAWAAMBIA DHAHIRI, SIKUWAJUA NINYI KAMWE; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”

Hapo anasema atawaambia “DHAHIRI” yaani maana yake wazi pasipo vificho, kwamba siwajui.

Maana yake ni kwamba kama ukiwa mwasherati kwa siri au kwa wazi, haijalishi unaona malaika kila siku katika ndoto, hautaurithi uzima wa milele, kama unaabudu sanamu kama ni mchawi kama ni mlevi na mambo mengine yote yanayofanana na hayo, basi siku ile hautaurithi uzima wa milele.

Na Neno la Mungu ni upanga ukatao kuwili, hivyo linawahusu watu wote, hata mimi pia linanihusu, kama sitakuwa mtakatifu sitaurithi uzima wa milele, haijalishi nafanya nini sasa.

Ndio maana Mtume Paulo kwa uongozo wa Roho akasema mahali fulani maneno haya…

Wagalatia 5:19  “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20  ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21  husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, KATİKA HAYO NAWAAMBİA MAPEMA, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”.

Hapo mstari wa 21, anasema “ANATUAMBIA MAPEMA”..Maana yake ni kwamba siku ile tutakapojikuta tumekataliwa na Kristo kutokana na kuukataa utakatifu…tusije tukasema tulikuwa hatujui!…Ndio maana hapo anatuambia mapema kuwa waasherati, wagomvi, wanaoabudu sanamu n.k hawataurithi uzima wa Milele.

Na pia katika Waefeso ni jambo hilo hilo linajirudia…

Waefeso 5:5  “Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu”.

Ndugu ni vizuri kuzifurahia fadhili za Mungu, tunapoumwa anatuponya, tunapokuwa katika mashaka anatupa faraja, tunapozungukwa na hatari anatuokoa..ni vizuri kuzifurahia hizo, kwasababu ndio uthibitisho kwamba tunaye Baba mbinguni, lakini hizo zisitupumbaze tukambweteka na kufikiri kuwa ndio tayari anapendezwa na sisi,.. ndio tayari tiketi za kutuingiza mbinguni…hapana! bado kuna jambo lingine la muhimu la kufanya, nalo ni utakatifu.

Hivyo ni lazima tuishi maisha masafi na ya utakatifu na ya toba kila siku. Ili tuwe na uhakika wa kumwona Baba siku ile.

Bwana atubariki.

Kama hujaokoka, wokovu unapatikana bure.. Unachopaswa kufanya leo ni kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi, na Roho Mtakatifu atashuka juu yako, na kukusafisha kabisa na kukupa uwezo wa kushinda dhambi, jambo ambalo kwa nguvu zako mwenyewe huwezi!.Na utapata raha ya wokovu

Maran atha!

Tafadhali unapowashirikisha wengine ujumbe huu usipunguze wala kuongeza chochote, wala usiweke anwani au namba yoyote tofauti na hizi zilizopo hapa,

Na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

PALE AHADI ZA MUNGU ZINAPOKUJARIBU.

JIFUNZE NAMNA YA KULITUMIA NENO LA MUNGU.

LAKINI USIKU WA MANANE, PAKAWA NA KELELE.

JINA LAKE KWA KIEBRANIA NI ABADONI, NA KWA KIYUNANI NI APOLIONI.

NAYE HERI AWAYE YOTE ASIYECHUKIZWA NAMI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments