NAYE HERI AWAYE YOTE ASIYECHUKIZWA NAMI.

NAYE HERI AWAYE YOTE ASIYECHUKIZWA NAMI.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima. Karibu tujifunze Maneno ya uzima.

Siku zote tunavyolijua Neno la Mungu ndivyo tunavyozidi kuwa na amani na ujasiri zaidi wa kusonga mbele kwasababu biblia inasema.. Neno lake ni taa ya miguu yetu, Na mwanga wa njia zetu (Zab 119:105).

Leo kwa neema za Bwana tutajifunza tena kisa cha Yohana Mbatizaji,. Kama tunavyoijua habari yake Yohana alikuwa ni mkuu zaidi ya nabii yeyote aliyewahi kutokea kulingana na maneno ya Bwana wetu Yesu, na kwamba tangu wakati wake, kurudi nyuma hakuna nabii yote aliyemzidi kwa ukuu mbinguni, si Eliya, si Isaya, si Yeremia, si Musa wala si mwingine yeyote yule.

Lakini pamoja na ukuu wake wote, kuna wakati alimtilia shaka Bwana Yesu..Japokuwa aliisikia kabisa sauti kutoka mbinguni ikimshuhudia kuwa Yesu ndiye mwana pekee wa Mungu, aliyependezwa naye..Japokuwa alimwona Roho Mtakatifu akishuka juu yake kama hua, kumtia mafuta..Lakini kuna wakati alifikia kumtilia shaka..

Japokuwa aliwashuhudia wanafunzi wake, na watu wengine kuwa Yule kweli ni mwana wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu, mpaka baadhi ya waliokuwa wanafunzi wake wakamwacha, wakafuatana na Yesu, lakini alikuja kumtilia shaka wakati fulani.

Hiyo ilitokea siku moja akiwa gerezani akawatuma wanafunzi wake, kumfuata Yesu ili kumuuliza, je! yeye kweli ni Yule mwokozi wa ulimwengu waliyekuwa wanamsubiria au wamtazamie mwingine..?

Jaribu kutafakari maneno hayo, mtu ambaye maisha yake yote amekuwa akimshuhudia, na ambaye ndiye aliyetiwa mafuta na Mungu kumtengenezea njia leo hii, anauliza tena kana kwamba alikuwa hana uhakika kuwa yeye ndiye..

Mathayo 11:1 “Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake kumi na wawili, alitoka huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

2 Naye Yohana aliposikia huko gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza,

3 Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?

4 Yesu akajibu akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana mnayoyasikia na kuyaona;

5 vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema.

6 NAYE HERI AWAYE YOTE ASIYECHUKIZWA NAMI.

Unadhani ni kwanini Yohana alisema vile? Alisema vile kwasababu “alimtazamia zaidi ya matazamio yenyewe kwa wakati ule”, Pengine alitazamia Bwana Yesu atakwenda kukaa kama mfalme awaokoe Israeli na maadui zao, kama maandiko yanavyosema, lakini akashangaa, mbona havutiwi hata na mambo ya ufalme wa duniani hii!!..Alitazamia atakaa kuwahukumu Israeli kwa mkono wa Mungu kama maandiko yanavyosema!, lakini yeye anamwona ndio kwanza anawahubiria wenye dhambi na maskini habari njema..Alitazamia atakuwa tajiri kwasababu ya ufalme wake, lakini anamsikia analala kwenye milima, hana hata kibanda n.k..

Unaona? Si kwamba matazamio yake yalikuwa ni uongo hapana, yalikuwa ni kweli lakini si katika wakati husika.

Ndipo Yesu aliposikia hivyo, akawatuma wale watu kumrudishia ujumbe juu ya kazi alizokuwa anazifanya..Na mwisho kabisa akamalizia na kuwaambia “Heri awaye yote asiyechukizwa nami”

Au kwa namna nyingine heri mtu Yule asiyekwazwa na haya niyafanyayo sasa..

Ndivyo ilivyo hata leo, mawazo kama hayo yapo miongoni mwetu kanisa la leo, si watumishi, si washirika.. wote.

Tunasema Yesu wewe ni mkuu, ni tajiri, nimempokea siku nyingi, nimesoma shuhuda zake, na mambo yake makuu aliyoyafanya kwenye biblia, na aliyowafanyia watu wengine, lakini mbona sioni akinibadilisha maisha yangu, na uchumi wangu.? Huyu ni Yule kweli wa kwenye biblia, au nimtazamie mwingine?

Bwana anasema.. Heri awaye yote asiyechukizwa nami.

Ndugu yangu, usivunjwe moyo ukamwacha Yesu, kisa tu hajakuponya ugonjwa wako ulionao kwa muda mrefu..

Usichukizwe na Yesu kisa tu hajayajibu maombi yako uliyokuwa unamwomba kwa muda mrefu.. Si kila jambo ni lazima ujue sababu yake leo, wewe endelea kumwamini tu..Anasema heri mtu Yule asiyechukizwa nami.

Hujui kesho kakupangiaje.. Wale walioweza kumvumilia Bwana Yesu mpaka dakika za mwisho ndio waliokuja kumjua yeye vizuri alikuwa ni nani, walijua kuwa kumbe itampasa aje mara mbili, kumbe mara ya kwanza ilikuwa ni kwa lengo la kuwaokoa watu dhambi zao, na mara ya pili ndio itakuwa ni ya kuketi kama Mfalme wa Wafalme na kuwahukumu mataifa, na kutawala pamoja na watakatifu wake..Na kwamba yeye ndiye atakayeshika utajiri wote wa mataifa. Lakini wao waliokuwa wanataka yatokee yote kwa wakati mmoja, hapo ndipo walipokosa shabaha.

Kumbuka upo ufalme Bwana Yesu alikwenda kutuandalia mbinguni, ambapo sisi tutakaoshinda, sisi ambao hatukuchukizwa na yeye tukiwa hapa duniani, tutaurithi huo, nasi tutawala naye kama wafalme na makuhani, wakati huo, ndio tutajua kuwa Mungu alikuwa anatuwazia mawazo mazuri.

Kwahiyo ukiona mambo hayaendi kama ulivyoyatazamia leo, ndio kwanza zidi kumpenda Yesu. Usimtilie shaka, Yesu ni Mungu. Siku zote anatuwazia mawazo mazuri, Na kesho yetu ipo mikononi mwake, tusichukizwe naye hata kidogo, pale ambapo hajibu maombi yetu kama tulivyotazamia..Kila jambo lina majira yake na wakati wake.

Mhubiri 3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.

2 Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa;

3 Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga;

4 Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza;

5 Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia;

6 Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa;

7 Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;

8 Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

UTHABITI WA AGANO LA MUNGU KWA MKRISTO.

WAKATI WA KRISTO KUSIMAMA,UMEKARIBIA SANA.

Nifanye nini ili niishi maisha ya ushindi siku zote?

NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?

UBATIZO NI NINI NA ULIO SAHIHI NI UPI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments