by Admin | 9 November 2020 08:46 pm11
Kwanini Kuhani wa Mungu Eli alikufa kwa kuvunjika shingo, Na sio kwa njia nyingine yoyote salama?
Habari ya Eli ni funzo tosha kwa kanisa la Kristo leo hii. Mungu aliruhusu afe kifo cha aina hiyo, ili kutimiza mstari huu wa biblia;
Mithali 29:1 “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa”.
Kama tunavyoijua habari ya Eli,alikuwa kuhani wa Mungu kwa muda wa miaka 40, na katika ukuhani wake, alifanya kazi hiyo pamoja na wanawe wawili, lakini watoto wake hawa walikuwa waovu kupindukia, kwani waliwakosesha Israeli kwa tabia zao sizizoakisi ukuhani, na habari yao ikavuma kila mahali kuwa hawafai, kwani walikuwa wanaila dhabihu isivyostahili na zaidi ya yote, walikuwa wanalala na wanawake waliokuwa wanatumika mbele ya hema ya kukutania, mfano tu baadhi ya wakristo katika kanisa la Mungu leo hii.
Sasa dhambi hii ilikuwa ni kubwa sana, na Mungu alikuwa amekusudia kuwauwa wale watoto wawili wa Eli, na sio Eli mwenyewe, lakini tabia ya Eli ya kupuuzia na kuwaheshimu watoto wake zaidi kuliko Mungu, hilo lilimfanya Mungu amuue na yeye kwa kifo hicho. Kwasababu alijua kabisa uovu unaofanywa na wanawe lakini hakulitilia mkazo.
Eli alionywa mara tatu, mara ya kwanza alionywa na waisraeli, kuwa watoto wake hawafai na kwamba anapaswa awaondoe katika kazi ya ukuhani lakini hakusikia..
Akaonywa tena mara pili na Mungu kupitia nabii wake, (1Samweli 2:29), lakini bado hakuwaondoa, akawaheshimu wanawe kuliko Mungu.
Akaja tena kuonywa mara ya tatu kupitia mtoto Samweli, akaelezwa mpaka na hukumu itakayowakuta watoto wake, lakini yeye bado akaendelea kuwaacha wafanye machafuko yote hemani pa Bwana.
1Samweli 3:13 “Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia”.
Ndipo siku ya siku ilipofika, Wafilisti waliwavamia Israeli, wakawapiga, wakaliiba na sanduku la Agano, Na yeye akiwa amebaki hemani mwake kusubiria taarifa ya vita, kama tunavyoijua Habari, kijana mmoja alitoka huko akamletea habari, na kumwambia Israeli imepigwa, wanawe wote wawili wamekufa na kibaya zaidi Sanduku la Mungu limechukuliwa na wafilisti. Aliposikia tu habari hiyo akadondoka kwa nyuma, shingo yake ikavunjika na pale pale akafa.
1Samweli 4:13 “Alipofika, tazama, Eli alikuwa ameketi kitini pake kando ya njia, akingojea; maana moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Na yule mtu alipoingia mjini, akatoa habari, mji wote ukalia.
14 Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli.
15 Basi Eli umri wake umepata miaka tisini na minane; na macho yake yamepofuka hata asiweze kuona.
16 Yule mtu akamwambia Eli, Mimi ndimi niliyetoka jeshini, nami leo hivi nimekimbia toka jeshini. Naye akasema, Yalikwendaje, mwanangu?
17 Yeye aliyeleta habari akajibu, akasema, Israeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, tena watu wengi sana wameuawa, hata na wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa pia, na sanduku la Mungu limetwaliwa.
18 Ikawa alipolitaja sanduku la Mungu, Eli akaanguka kitini pake kwa nyuma, kando ya mlango, shingo yake ikavunjika, akafa; maana alikuwa mzee, tena mzito. Naye alikuwa amewaamua Israeli miaka arobaini”.
Hivyo kitendo cha Eli kufa kifo cha kuvunja shingo ni Mungu alikuwa anafundisha jinsi madhara yatakavyowakuta watu wale wanaopuuzia na kudharau maagizo yake.
Tengeneza picha Eli alikuwa ni kuhani lakini alikufa kifo cha ghafla tu kwa kosa la kudharau maneno ya Mungu. Vipi kuhusu sisi ambao kila siku Mungu anatuonya tuache hichi au kile lakini hatutaki kusikia, Mtu anazini na bado anasema ameokoka. Kila siku tunasikia maneno ya Mungu lakini bado hatutaki kuyakabidhi maisha yetu kwake.. Je! Ni kitu gani tunakitazamia siku za usoni?
Hututakufa kifo cha kuvunjika shingo kimwili, lakini rohoni tutavunjika shingo zetu ghafla, na hutakuwa na nafasi tena ya kumrudia Mungu, kwasababu hukumu tayari itakuwa umeshatolewa juu yetu.
Mithali 29:1 “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa”.
Inawezekana na wewe umeshaonywa mara nyingi kwa kupitia mahubiri ya Neno la Mungu, lakini ulikuwa umeshupaza shingo…. Kwanini leo, usimrudie muumba wako? Kwanini usianze maisha mapya na Kristo, uondokane na laana ya dhambi? Maisha ya dhambi yamekupa faida gani mpaka sasa, Ukifa leo ghafla huko utakapokwenda utakuwa ni mgeni wa nani?. Au Kristo akirudi leo wewe utakuwa wapi?. Kwasababu tupo ukingoni kabisa mwa nyakati, Kristo anarudi.
Ulimwengu huu umeshatamkiwa meme, mene, Tekeli na Peresi kitambo sana, Umeshatamkiwa IKABODI, Hakuna cha ziada zaidi ya kuharibiwa tu. Tubu dhambi zako kama bado hujatubu. Na pia tafuta kubatizwa ikiwa bado hujabatizwa. Na Mungu atakupa Roho wake Mtakatifu. Katika wakati huu wa kumalizia.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Kwanini Samweli aliruhusuiwa kuhudumu hekaluni kama vile Walawi wakati yeye ni mu-Efraimu?
Kitabu cha YASHARI kinachozungumziwa katika 2Samweli 1:17-18, ni kitabu gani?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/09/kwanini-kuhani-wa-mungu-eli-alikufa-kwa-kuvunjika-shingo/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.