by Admin | 24 November 2020 08:46 pm11
SWALI: Naomba ufafanuzi kidogo hapa sijaelewa vizuri, kwanini wakati Bwana Yesu anakuja kukamatwa naona kijana waliyemkamata alikuwa na nguo ya kitani ila baadae tunaona anaitupa nguo na kukimbia uchi , Marko 14:51-52
JIBU: Tusome;
Marko 14:50 “Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote.
51 Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata;
52 naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi”.
Biblia haielezi huyu kijana alikuwa ni nani, wengine wanasema alikuwa ni Marko mwenyewe aliyeandika kitabu hicho, au mwanafunzi mwengine mbali na wale
12, kwasababu wale walikuwa yatari wameshakimbia, ukisoma mstari wa 51. Lakini kufahamu kama huyu kijana alikuwa ni miongoni mwa wale 12 au wengineo sio la muhimu sana kwenye habari hiyo . La muhimu ni kujua kwanini tukio kama lile lijitokeze.
Kwanini biblia inasema aina ya vazi alilovaa kwamba ni la kitani?. Kwanini aache vazi akimbie na sio kitu kingine? .Tukiweza kuyatafakari maswali hayo tutapata ujumbe mkubwa sana nyuma ya tukio lile.
Kama tukichunguza asili ya vazi hilo, kwa mazingira yaliyokuwa yanaendelea pale tunaweza kusema ni vazi linalomsitiri mtu mwili wote. Kiasi kwamba likivaliwa halihitaji kuvaliwa na kitu kingine ndani. Kiasi kwamba mtu akilivua ni rahisi kubakiwa uchi.
Pili, ni vazi ambalo ni rahisi kuvulika, halihitaji kufungwa au kushikizwa kwa vitu vingi. Na ndio maana utaona kijana huyo alipokamatwa tu na wale askari, ilikuwa ni rahisi kuwaachia lile vazi na kukimbia. Ingekuwa ni vazi lenye vifungo, au mikandani mingi, isingekuwa rahisi kujikwamua kwa wale askari.
Na jambo lingine unaweza kuona pale, ni kuwa wale askari waliona njia pekee ya kumkamata ni kwa kulishika vazi lake, na sio pengine mikono yake au kitu kingine,. Na ndio maana utaona kijana alitumia njia ya kuacha vazi ili akimbie.
Hiyo ni kutufundisha, kuwa lipo vazi la rohoni (Kitani ya rohoni). Ambalo linauwezo wa kuusitiri uchi wote wa mtu wa rohoni, lakini pia ni jepesi sana mtu kulivua. Na ndio Bwana Yesu alisema..
Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na KUYATUNZA MAVAZI YAKE, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)”
Unaona hapo anasema heri “ayatunzaye” mavazi yake. Ni kuonyesha kuwa mavazi hayo yanapaswa yatunzwe sana..kwasababu ni rahisi kuvulika.. Tutaona mbele kidogo mavazi hayo ni nini..
Na adui yetu shetani, anachokiwinda kwetu, sio miili yetu, sio mionekano yetu, si madhehebu yetu, si dini zetu. Bali ni mavazi yetu ya rohoni..Hayo ndiyo anayokimbilia kuyashika, haya ndiyo anayotaka umuachie, kama alivyofanya kwa yule kijana, Na mavazi yenyewe si mengine zaidi ya “matendo yetu ya haki” (yaani, utakatifu). Biblia inasema hivyo katika.
Ufunuo 19:8 “Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; KWA MAANA KITANI NZURI HIYO NI MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU”.
Unaona? Mavazi ya kitani ni matendo ya haki ya watakatifu. Mpaka hapo utakuwa unapata kufahamu ni picha gani Mungu alikuwa anatuonyesha kwa yaliyokuwa yanaendelea kwa Yule kijana rohoni. Hata sasa ni kawaida watu wanapopitia shida kidogo, au dhiki au wanapokutana na matatizo kuuacha wokovu, wanaacha utakatifu, wanamwacha Mungu, wanaacha kutenda matendo mema tena, wanamwachia adui vazi lao la thawabu.
Hivyo Neno la Mungu linatufundisha, tukutanapo na udhia wowote, au dhiki, tusiwe wepesi wa kuuacha wokovu wetu na utakatifu wetu.
Swali ni je! VAZI hili unalo? Ikiwa huna
Bwana Yesu anakupa shauri katika Ufunuo 3:18 kuwa ukanunue kwake mavazi hayo meupe uvae ili aibu ya uchi wako isionekane.. Hivyo tubu kama bado hujafanya hivyo, ukabatizwe, upokee Roho Mtakatifu. Ukamilishwe kwa vazi hili
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/24/kwanini-yule-kijana-aliitupa-ile-nguo-ya-kitani-chini-na-kukimbia-uchi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.