UFUNUO NI NINI, NA NITAPOKEAJE UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU?

by Admin | 5 December 2020 08:46 pm12

Ufunuo ni kitu kilichofunuliwa.. Maana yake ni kwamba kilikuwa kimefichika/kimefichwa  sasa kimefunuliwa.

Tunaposoma maandiko na kupata kitu kipya ambacho hatukuwa tunakijua hapo kwanza, hapo ni sawa na hicho kitu kimefunuliwa kwetu.

Kwamfano unaposoma biblia kuhusu damu ya Yesu, na ukagundua kitu kipya kuhusu damu hiyo, hicho ulichokipata ndio ufunuo. Sasa hicho ndicho kinachoelezea ukubwa wa Imani yako, Ukipata kujua/kugundua kitu kikubwa zaidi kuhusu damu ya Yesu, ndivyo Imani yako inavyozidi kuwa kubwa. Maana yake ni kwamba kwa ufunuo huo unaweza kutatua matatizo makubwa ya kiroho, au kufanya mambo makubwa, tofauti na yule mtu ambaye bado hajapata ufunuo wowote kuhusu damu ya Yesu.

Na maneno mengine yote ya Mungu ni hivyo hivyo, Ukipata kugundua kitu cha kipekee kumhusu Yesu, ambacho hapo kwanza ulikuwa hukijui.. Hicho ulichokigundua ndicho shetani kinachomwogopesha na ndicho hicho kinachoweza kukupa matokeo makubwa ya rohoni.Na kugundua huko kunaletwa na Roho Mtakatifu mwenyewe ndani ya mtu.

Sasa Ufunuo upo wa uongo, na Pia upo wa ukweli.

Unaweza kusoma neno ukapata kitu au ukagundua kitu ambacho ulikuwa hujakijua hapo kwanza.. Sasa hicho kitu ulichokigundua kama ni cha ukweli (maana yake kama kimetokana na Mungu kupitia Roho wake Mtakatifu) basi kitakubaliana na mistari mingine au habari nyingine za kwenye biblia. 

Lakini kama si cha ukweli basi kitakinzana na mistari mingine ya biblia. Maana yake si cha kukipokea wala kukiamini. 

Sasa ni kwa namna gani tutapokea Ufunuo?. Zipo njia kuu Mbili.

  1. Kwanza ni kwa kulisoma Neno la Mungu:

Wengi hawapendi kulisoma Neno la Mungu wao binafsi, na badala yake wanapenda kufundishwa,  au kutazama filamu fulani tu  za kikristo, Lakini pasipo kujua kuwa kuna hatari kubwa sana ya kudanganywa kama usipojijengea tabia ya kulisoma mwenyewe Neno. 

Kwasababu wanaofundisha uongo ni wengi kuliko wanaofundisha ukweli. Bwana Yesu alisema Njia ni nyembamba, maana yake mimi na wewe hakuna namna tunaweza kuifanya iwe nene, na alisema Manabii wengi wa uongo watatokea watawadanganya hata yamkini walio wateule, hakuna namna tunaweza kuwafanya wawe wachache hawa manabii wa uongo. Kwahiyo Njia itakayobakia kuwa bora siku zote ni ile ya mtu binafsi kutafuta kulisoma Neno yeye binafsi maadamu anao uwezo wa kusoma na kuandika. Na hapo hapo Roho Mtakatifu anapata nafasi ya kumfunulia maandiko.

Na kumbuka tunapozungumzia kusoma Neno hatumaanishi kwenda kuchukua mstari mmoja hapa kwenye Mathayo na kisha kwenda kuruka kutafuta mstari mwingine wa faraja kwenye Isaya, Na kurudi kuunganisha mwingine kwenye Yeremia..na hivyo kujikuta kwa siku umesoma mistari mia, tofauti tofuati kwa masaa mawili na kujipongeza kuwa umelisoma Neno..Nataka nikuambia hapo utakuwa hujasoma biblia bali umeiperuzi biblia, wanaoiperuzi biblia ni wahubiri, na wanafanya hivyo kwa lengo la kufundisha, somo lipate kueleweka kwa muda mfupi. Hivyo wewe usiiperuzi biblia, hutaelewa chochote na wala hutapata kitu cha kudumu cha kukusaidia roho yako.

Kusoma Neno kunakofaa ni huku, kushika kitabu kimoja kimoja…kukisoma chote pasipo kuruka…sio lazima ukisome chote kwa siku moja hapana, Mfano unaweza kuanza kusoma kitabu cha Mwanzo, sura 10 za kwanza na kisha kupata muda mrefu wa kuzitafakari, na hata kuzirudia tena hizo mpaka utakapoona umeelewa vya kutosha kusonga mbele.. lakini ukisoma sura 4, 5 ukafika sehemu inazungumzia vizazi ukaboreka na kisha ukarukia kitabu cha kutoka hutakaa uielewe biblia..

Soma kitabu cha Mwanzo chote kimalize, haijalishi itakuchukua wiki au mwezi, kisha nenda kitabu kinachofuata… Ukifanya hivyo utaielewa biblia sana, na Ndio chanzo kikubwa cha KUPATA UFUNUO WA KWELI wa Neno . Na pia unaposoma biblia, hakikisha unafungua kule nyuma kwenye ramani, uielewe pia ramani kama biblia yako inayo ramani..fuatilia kwenye ramani zile hatua Ibrahimu alizopita, Wana wa Israeli walizopita, miji Bwana Yesu aliyokuwa anatembea n.k.

  1. Njia ya pili ni ile ya Kusikiliza Mahubiri:

Sasa kama tulivyotangulia kusema, Kuna hatari kubwa sana katika kutegemea njia hii kupata ufunuo wa Neno la Mungu. Lakini njia hii ikitumika sahihi pia ni rahisi kupata mengi. 

Sasa njia bora sio kufungulia redio au internet na kwenda kusoma au kusikiliza mahubiri yanayoendelea kila siku, na huku huna habari kabisa na biblia yako, hapo nakuambia utakwenda na maji, haijalishi mhubiri huyo umemwamini kiasi gani.

Njia bora ni ya kupata ufunuo wa Neno la Mungu kupitia watumishi wa Mungu, ni wewe kwenda kusoma Neno kwanza, labda mada fulani katika biblia.. Na kisha ukishaisoma hiyo mada na ukaielewa, isipokuwa kuna vipengele vichache ambavyo hukuvielewa na ungehitaji kuviongezea maarifa, ndipo unamtafuta Mtumishi na kumuuliza kulingana na ile mada uliyoisoma, au unakwenda katika internet na kukitafuta kitu kile, uone maoni ya watumishi mbali mbali kuhusu jambo hilo.

Hiyo ni njia bora ambayo itakusaidia kutokudanganywa kirahisi, kwasababu utakuwa unakwenda kutafuta kujua kitu ambacho tayari una ufahamu nacho angalau kidogo, hivyo ni ngumu kudanganyika…Kamwe usiende kutafuta kuuliza kitu ambacho hata wewe mwenyewe hujui kinapatikana wapi kwenye biblia.

Ni sawa umekwenda kwenye mji uliochanganyikana kama Kariakoo, na kuanza kuuliza uliza, bila ya wewe kuwa na angalau taarifa ndogo ya kile unachokitafuta au unakokwenda, kwasababu kama hujui kabisa ni rahisi kutapeliwa na kupoteza kila kitu ulichonacho..Unaweza kuomba kuelekezwa benki ukaelekezwa kichochoro cha vibaka, ukaibiwa kila kitu hata nauli uliyokuwa umebakiwa nayo.

Ndio maana Bwana Yesu alisema katika Luka..

Luka 8:8 “Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.”

Bwana anatuonya tujiangalie jinsi TUNAVYOSIKIA.  Maana yake ukienda kutafuta kusimuliwa vitu bila wewe mwenyewe kutafuta kusoma kile kitu kwanza, angalau kidogo, kuna hatari kubwa ya wewe kupoteza kila kitu hata kile kidogo kizuri ulichokuwa nacho moyoni mwako. Ni rahisi hata kama kulikuwa na kitu cha ukweli moyoni mwako, ni rahisi kukipoteza hicho, Kwasababu utakayekutana naye kama atakuwa ni mwalimu au nabii wa uongo, atakutoa kabisa kwenye mstari (huko ndio kunyang’anywa hata kile kidogo ulicho nacho).

Kwamfano unakwenda kumuuliza Mwalimu/Nabii (wa uongo) kuhusu habari fulani kwenye biblia ambayo ulisikia tu watu mtaani wakisimuliana, ili hali wewe hujawahi hata kwenda kuifuatilia kwenye biblia inasemaje, yule nabii atakudanganya, na wewe utamwamini..na zaidi ya hayo, kama pia kama ulikuwa unaamini kuwa si sahihi kuoa wake wengi, huyo nabii atakupa maandiko na maandiko pia ya kukuambia ni ruksa kuoa wake wengi, na wewe utamwamini. Pasipo kujua kuwa tayari umeshanyang’anywa hata kile kidogo ulicho nacho.

Roho Mtakatifu anataka kutufundisha mengi, lakini sisi ndio hatutaki kumpa nafasi ya yeye kutufundisha, kwasababu tunakuwa wavivu wa kusoma (Waebrania 5:11). Tujitahidi kumpa nafasi.

Bwana atubariki.

Kama hujampokea Yesu, Basi fahamu kuwa ANARUDI. 

Waebrania 10:37  “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia”.

Hivyo mkaribie leo naye atakukaribia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JIFUNZE NENO LA MUNGU KWA BIDII ZOTE.

Uga ni nini? Na kazi yake ni ipi kibiblia?

MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 10 (Kitabu cha Zaburi).

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/05/ufunuo-ni-nini-na-nitapokeaje-ufunuo-kutoka-kwa-mungu/