JIFUNZE NENO LA MUNGU KWA BIDII ZOTE.

JIFUNZE NENO LA MUNGU KWA BIDII ZOTE.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, libarikiwe!.

Karibu tujifunze Biblia.

Ndege tunazozipanda zinazoruka angani, hazijaundwa na mtu mmoja, kuna jopo kubwa sana la watu wamechangia maarifa katika kuiunda ile.. Utaona aliyegundua injini ya ndege ni mwingine, aliyegundua mfumo wa hewa ndani ya ndege ni mwingine, aliyebuni umbile na mwonekano wa ndege ni mwingine, aliyegundua sayansi ya kuifanya iruke ni mwingine, aliyegundua mfumo wa umeme ndani ya ndege ni mwingine, aliyegundua Mafuta ya ndege ni mwingine, aliyegundua kona ya ndege ni mwingine, aliyebuni matairi ya ndege ni mwingine n.k.

Sasa hao wote kila mmoja akiandika kitabu chake kidogo cha maelezo kuhusu mchango wake huo na vitabu hivyo vikakusanywa Pamoja bila shaka tunaweza kujikuta tuna kitabu kimoja kikubwa kama Biblia au hata Zaidi ya biblia, kilichojaa elimu kuhusu ndege. Maana yake ni kwamba mtu atakayejifunza hicho na kukielewa anaweza naye pia kutengeneza ndege yake.

Hivyo basi kama ilikuwa ni mpango wa Mungu kwamba wanadamu siku moja waruke angani, waende mbali sana kule juu Zaidi ya Tai..kumbe mpango wake haukuwa wa kumpa mtu mmoja maarifa hayo, bali aligawanya ujuzi huo kwa watu tofauti tofauti wanaojulikana kama wanasayansi..ambao katika hao kila mmoja alipochangia ujuzi wake na uvumbuzi wake ndipo kitkapoumbwa kitu kinachoitwa Ndege.

Kama ulikuwa ni mpango wa Mungu siku moja tusafiri kutoka bara moja hadi lingine kwa muda mfupi kwa kutumia ndege, na tena kama ulikuwa ni mpango wa Mungu siku moja turuke mbali sana Zaidi ya mawingi hata kuufikia mwezi kwa kutumia roketi…Basi pia upo mpango mwingine wa Mungu ulio mkubwa Zaidi ya huo, ambao utatufanya tupae Zaidi ya mawingu na mwezi na Zaidi ya nyota… Na huo si mwingine Zaidi ya ule wa kutupeleka mbinguni yeye alipo.

Na kama vile maarifa ya uvumbuzi wa kifaa kinachoitwa ndege au roketi, yalivyogawanyika katikati ya watu tofauti tofauti, vivyo hivyo maarifa ya kwenda mbinguni wamefunuliwa Mitume na Manabii mbalimbali wa kwenye biblia…Wakina Yeremia, Danieli, Musa, Ezekieli,…Wakina Petro, Paulo, Yohana n.k Hao kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu kila mmoja kaandika siri za ufalme wa Mbinguni kwa jinsi alivyojaliwa…ambazo sisi kama wakristo, tunajifunza leo katika kitabu kinachoitwa biblia, na kama tukifuzu kukielewa vyema basi tunaweza kupaa juu Zaidi ya yale mawingu. Tunaweza kutengeneza roketi na kuingia ndani yake na kuruka Zaidi ya yale mawingu, na ndege yetu hiyo au Roketi ni YESU KRISTO.

Yesu ndiye NJIA, KWELI na UZIMA…Mtu hawezi kufika kwa Baba mbinguni isipokuwa kwa Njia yake yeye (Soma Yohana 14:6).

Teknolojia inahubiri injili, ukiona wakati tunaoishi inawezekana kusafiri hewani, basi jua kuna safari kubwa kuliko zote inakaribia. Lakini hayo yote hayaji pasipo maarifa.

Ndugu dada/kaka usiache kusomana kujifunza kamwe biblia, Hakuna sehemu yoyote utaweza kupata maarifa ya kumjua Yesu nje ya biblia. Usiposoma biblia kwa kujifunza utachukuliwa na kila aina ya upepo wa uongo. 

Usipende kusubiria tu kufundishwa biblia, Jifunze kuisoma mwenyewe!.. Hata mwanafunzi anayefanikiwa masomoni ni yule kwanza anayependa kujisomea mwenyewe…Na anapokutana na maswali magumu ndipo anapokwenda kuuliza kwa mwalimu wake!..Lakini mwanafunzi anayependa kufundishwa tu! Na wala hana muda wa kujisomea yeye mwenyewe..kamwe hawezi kufanya vizuri..Na ndivyo hivyo hata sisi, Mungu anataka tuisome biblia wenyewe!.

Kumbuka pia hajayarekodi maneno yake kwa njia ya Audio, kayaweka kwenye kitabu…Ukiona kitu kimewekwa kwenye kitabu maana yake anayekisoma anahitaji kuketi chini mahali pasipo na usumbufu, akiwa na kalamu yake na daftari..Biblia hatuisomi kama gazeti, tunajifunza na ndivyo Roho Mtakatifu anataka tuwe hivyo ili aweze kutufunulia siri zake..

Je unataka kwenda mbinguni?..Mimi nataka sijui wewe?..kama wewe nawe unataka basi Ni lazima tuifahamu biblia sana.

Bwana akubariki

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

WAKAKAA KWAKE SIKU ILE. NAYO ILIKUWA YAPATA SAA KUMI.

ACHENI MJUE YA KUWA MIMI NI MUNGU.

MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.

USIRUHUSU MUNGU AWEKE UADUI KATI YAKO NA WATU WAKO.

Yuko azuiaye sasa hata atakapoondolewa! ni nani huyo?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Moses Mohamed
Moses Mohamed
3 years ago

Nimeyapenda masomo yenu, naomba mnionganishe.