USIRUHUSU MUNGU AWEKE UADUI KATI YAKO NA WATU WAKO.

USIRUHUSU MUNGU AWEKE UADUI KATI YAKO NA WATU WAKO.

Bwana Yesu Kristo asifiwe.

Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu, ambalo ndio mwanga wa njia yetu na taa iongozayo miguu yetu.

Ili tufanikiwe na tuwe na maisha mazuri siku zote ni lazima tujifunze kulitii na kulishika Neno la Mungu. Kinyume na hapo tutasumbuka sana bila sababu.

Watu wengi wanatafuta kutengeneza urafiki na undugu na watu wengi…wakitegemea marafiki hao wakati wa tabu watawafariji, au wakati wa shida watawasaidia, lakini wengi wanaishia kuumizwa na hao hao marafiki au ndugu, na kupata vile wasivyovitegemea. Unakuta urafiki utaanza vyema lakini utaishia kuwa uadui. Wengine wanatafuta wanawake/wanaume wakitazamia hao ndio watakaokuja kuwa waume zao au wake zao..lakini mwisho wanaishia kuumizana na kuharibiana maisha.

Ipo sababu ya mambo hayo kuwa hivyo…Na sababu hiyo ilianzia tangu Edeni. Hivyo kama tutalielewa somo vizuri kilichotokea Edeni basi, hatutarudia makosa ambayo tayari yalishafanywa na tukaona madhara yake.

Sasa hebu tuwatafakari hawa marafiki wawili ambao hapo kwanza walikuwa na mahusiano mazuri lakini yakaishia kuwa mabaya tena ya uadui. Na marafiki hao si wengine zaidi ya HAWA NA NYOKA. Wote hawa walikuwa wapo katika uwepo wa Mungu, na walikuwa wanakaribiana sana…lakini baada ya kuyaasi maagizo ya Mungu, Mungu akaweka uadui mkubwa katikati yao…Kiasi kwamba mpaka leo Nyoka na mwanadamu ni maadui wakubwa sana…Ukiuliza ni kiumbe gani wa kwanza anayeogopwa na wanawake wengi nadhari asilimi zaidi ya 90 watamtaja nyoka..Hiyo ni kutokana na uadui ambao Mungu aliuweka mwenyewe katikati yake yeye na nyoka.

Mwanzo 3: 14 “Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako;

15 NAMI NITAWEKA UADUI KATI YAKO NA HUYO MWANAMKE, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino”.

Umesoma hapo mstari wa 15?…Watu wengi hawajui kuwa UADUI ambao unatokea ghafla kati yao na ndugu zao, au marafiki zao mwingi unawekwa na MUNGU mwenyewe na wala si shetani, na huo ni kutokana na kuacha kulitii na kulishika Neno lake.

Kwamfano utakuta mwanamke… anakutana na mtu ambaye anahisi atakuwa mume wake, na moyoni anajua kabisa hapaswi kukutana kimwili na yoyote Yule mpaka atakapoolewa(kanisani ameshafundishwa sana na yeye mwenyewe anayajua maandiko)…lakini kwa kulikaidi Neno la Mungu anaamua amridhishe Yule mwanaume na kwenda kufanya naye uasherati, akidhani baada ya kitendo hicho ndio atapendwa zaidi…kumbe kinyume chake ni kuchukiwa, baada ya hapo anashangaa Yule aliyemtegemea ampende ndio hana muda na yeye tena..na mwisho wa siku anajiona kama sio mwenye bahati.

Hivyo mwanamke hupaswi kumsogelea kabisa mwanaume, katika kipindi cha uchumba…kipindi cha uchumba sio kipindi cha kutembeleana nyumbani na huku mko wawili tu, si kipindi cha kupikiana pikiana, sio kipindi cha kukutana kutana nyumbani na huku mpo wawili tu!…kwasababu hicho ndio kipindi maalumu cha shetani kupanga kuvuruga mambo…Kama umeandaa chakula mwite mtu zaidi ya mmoja kwako pamoja na huyo mnayekaribiana kuoana lakini si nyinyi wawili tu peke yenu..na pia kumbuka huruhusiwi kabisa pia kumbusu mtu ambaye bado hamjafunga ndoa.

Mambo madogo kama hayo yanadharauliwa na wengi lakini ndio yanayovuruga mipango yote…Na kamwe usifikiri ukimheshimu Mungu, utachukiwa na Yule anayetaka kukuoa au unayetaka kumuoa…Kama ndiye Bwana aliyekusudia awe wako, hawezi kukuchukia zaidi ya yote ndio atakupenda.. Lakini mkivuka mipaka na kwenda kufanya uasherati kabla ya ndoa..hapo ndio basi tena!…kuna nafasi ndogo sana, au isiwepo kabisa ya nyinyi kuoana..mtaishia kuchukiana kwa chuki ya ajabu baada ya kipindi kifupi…mpaka mtashangaa wenyewe ni nini kimetokea…Mungu atawaweka uadui katikati yenu. Kwasababu Mungu hawezi kuunganisha wazinzi pamoja, maana lengo la Mungu kuwakutanisha kwenye ndoa ni ili awabariki…sasa hawezi kuunganisha wazinzi wawili na tena kuwabariki…atakachokifanya ni kuwaweka mbali mbali, au kuwaacha muendelee na uzinzi wenu na yeye asiwe na nyinyi (warumi 1:28).

Kama wewe ni msomi wa biblia utakuwa umewahi kusoma kisa cha Yule mototo wa Daudi aliyemtamani dada yake, na kumlazimisha alale naye…na baada tu ya kulala naye biblia inasema alimchukia kwa chuki isiyokuwa ya kawaida.

2 Samweli 13:13 “Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa.

14 Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye.

15 Kisha Amnoni AKAMCHUKIA MACHUKIO MAKUU SANA; KWA KUWA MACHUKIO ALIYOMCHUKIA YAKAWA MAKUU KULIKO YALE MAPENZI ALIYOKUWA AMEMPENDA KWANZA. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako.

16 Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza.

17 Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake”.

Ukianzia kusoma kuanzia mstariwa kwanza utaona, Kisa hicho ingawa mwanamke ndiye aliyelazimishwa kwa nguvu…lakini matokeo yake yalikuwa ni yale yale “CHUKI BAADA YA TUKIO”.

Kuna nguvu Fulani ya uadui inashuka kwa watu wanaovunja amri za Mungu..

Mnakubaliana kwenda kuiba au kula rushwa, mwisho wa siku ni lazima tu muishie kugombana…Mnakubaliana kufanya kazi haramu mwisho wa siku ni lazima muishie tu kuwa maadui, mnakubaliana kwenda kufanya utapeli/uuaji lazima mtaishia tu kugombana na kuchukiana na kuwa maadui, mtaanza vizuri lakini itafika kipindi mtatofautiana tu!!… fanya utafiti watu wawili wanaokaa kitako kumsengenya mwingine…huwa wanaishia na wao kugombana au kuchukiana, badala ya kuzidi kuwa pamoja..

Unakumbuka Mnara wa Babeli walianza pamoja lakini nia yao ilipokuwa katika kuujenga mji na mnara wa kisheatani, ili waabudu miungu, Mungu aliwasambaratisha, wakawa hawaelewani, huyu akisema hivi mwingine anasema hivi, wakagombana na mwisho wa siku hata lugha zikazalika nyingine…kazi ngumu waliyokuwa wameianza ikaishia pale pale.

Lakini kinyume chake kama ukiyashika maagizo ya Mungu na amri zake, na kumheshimu…Bwana anasema atakupa amani hata na maadui zako…

Mithali 16: 7 “Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye”.

Hivyo zishike amri za Mungu, na mambo yatakunyookea…ukitaka uwe na amani na ndugu zako, fomula ni hiyo hiyo.. “lishike Neno la Mungu”..usiwe kama Hawa mama yetu..aliyedhani kuuimarisha urafiki na nyoka ni kula lile tunda…kinyume chake ndio aliimarisha uadui kati yake na huyo nyoka, na hiyo roho imeendelea mpaka kwa vizazi vyake hadi leo.

Bwana atusaidie

Kama hujampa Yesu maisha yako, hapo jitenge binafsi, piga magoti tubu kwa dhati kabisa na kisha acha yote uliyokuwa unayafanya yasiyompendeza Mungu, na baada ya hapo tafuta kanisa lililopo karibu nawe la kweli, dumu hapo ujifunze Neno na pia upate kubatizwa..Na Roho mtakatifu atakuwa na wewe kukuongoza katika kweli yote.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

NAO WAKADHANI YA KUWA YUMO KATIKA MSAFARA;

VITA VYA IMANI NI VITA ENDELEVU.

VITA VYA IMANI NI VITA ENDELEVU.

KILA MMOJA WENU AJUE KUUWEZA MWILI WAKE.

KILA MMOJA WENU AJUE KUUWEZA MWILI WAKE.

DAMU YA YESU INANENAJE MEMA KULIKO YA HABILI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments