Je mtu anayeua anabeba dhambi zote za yule aliyemuua?

by Admin | 18 December 2020 08:46 pm12

Jibu: Si kweli kwamba mtu anayeua anakuwa anazibeba dhambi zote za yule aliyemuua, na kwamba yule aliyeuawa yupo huru, (anakuwa hana dhambi tena huko anakokwenda).

Kama mtu atamkataa Mungu na ghafla akafa katika dhambi zake, kwa kifo cha aina yeyote ile, iwe kwa kuuawa, au labda kwa kugongwa na gari, au kupewa sumu, au kupigwa mpaka kufa.. Mtu huyo dhambi zake anazibeba mwenyewe, na anakwenda nazo huko anakokwenda, hakuna yeyote atakayezuchukua. Yule aliyemuua atabeba dhambi ya mauaji, kwa alilolifanya lakini si dhambi za yule aliyemuua.

Wagalatia 6: 5  “Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe”.

Ni kitu kimoja tu ambacho Mungu atamdai mtu yule ambaye hatamwonya mwingine aiache njia yake mbaya. Na hicho si kingine zaidi ya Damu ya huyo mtu.

Ezekieli 3:18 “Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako”.

Sasa nini maana ya kuwa hatia na damu ya mtu?.

Kuwa na hatia ya damu ya mtu, si kuzichukua dhambi zake na kuzibeba.. La!..Bali maana yake ni kuwa na kila sababu za kuwajibishwa kwa kumsababishia mwingine madhara. Maana yake ni kwamba kama hujamwonya mtu aache njia mbaya, na ilihali ulikuwa na nafasi ya kufanya hivyo, na yule mtu akafa bila kusikia maonyo yoyote, basi wewe ambaye ulipaswa umwonye, kuna adhabu itakayokuja juu yako. Na adhabu hiyo inaweza kuwa laana au wakati mwingine hata kifo.

Ili tuelewe vizuri tafakari tu, mtu aliyemuua mwenzako…katika sheria za nchi, yule aliyeua hachukui madeni ya yule aliyemuua.. Maana yake ni kwamba, kama yule aliyeuawa alikuwa na madeni ya benki, au madeni mengine yoyote, madeni hayo hatayarithi yule aliyemuua. Yule aliyemuua atahukumiwa kwa kosa la mauaji (ambayo adhabu yake ndio hiyo ambayo inaweza kuwa hata kifo), lakini hatatwikwa madeni yote ya yule aliyemuua kwamba benki imfuate imwambie alipe deni la marehemu . Ndio hivyo hivyo pia kwa mtu aliyemuua mwingine, hatabeba dhambi za aliyekufa.

Hivyo tunachojifunza ni kwamba tuwe makini, hususani kama umeshaokolewa, ni wajibu wako kuwapelekea wengine injili, ili damu yao isiwe juu yako, kama Mtume Paulo alivyosema mahali fulani..

Matendo 20:25  “Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena.

26  Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote.

27  Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu”

Na kuipeleka injili sio tu kwenda kuhubiri, bali kuchangia hata kuichangia kazi ya Mungu, pia ni kuipeleka injili.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Aina za dhambi

Je! Kuna dhambi kubwa na ndogo, na kama hakuna je! Mtu aliyeua na aliyetukana je watapata adhabu sawa?

DHAMBI YA MAUTI

Je! Ni dhambi kumpiga au kumuua mnyama bila sababu yoyote?

6# SWALI : Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/18/je-mtu-anayeua-anabeba-dhambi-zote-za-yule-aliyemuua/