Kwanini ndugu wanaokaa pamoja wawe kama mafuta ya Haruni?

by Admin | 24 May 2021 08:46 pm05

SWALI: Naomba ufananuzi wa mstari huu, ni kwanini ndugu wanaokaa pamoja wafananishwe kama na mafuta mazuri yashukayo ndevuni mwa Haruni?

Zaburi 133:1 “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.

2 Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake”.


JIBU: Tunapaswa tujiulize ni kwanini awe ni Haruni na sio mtu mwingine kama vile Daudi, au Samweli au Eliya?. Haruni alikuwa ni kuhani mkuu. Na ukuhani wake ulikuwa na matokeo pale alipotiwa mafuta na Mungu (Kutoka 30:30, Walawi 8:12).

Hivyo kitendo cha ndugu kukaa pamoja katika Kristo, tena kwa umoja, wakinia mamoja, kwa upendo wote.. Rohoni kitendo hicho kinachukua umbile la kuhani mkuu anayetiwa mafuta mengi sana ambayo hayaishii tu kwenye kichwa au ndevu zake, bali yanatiririka kabisa mpaka kwenye pindo za mavazi yake.

Na kama tunavyojua leo hii, kuhani mkuu tunaye mmoja tu, ambaye ndiye Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo tunapokaa pamoja kwa umoja sisi kama kanisa la Kristo, msingi wetu ukiwa ni Biblia, basi rohoni tunachukua lile umbile la Kristo alipokuwa anatiwa mafuta na Mungu hapa duniani.  Biblia inasema mafuta aliyotiwa yalikuwa ni mengi kuliko  kuhani au mtakatifu yoyote aliyewahi kuishi hapa duniani.

Waebrania 1:8 “Lakini kwa habari za Mwana asema, Kiti chako cha enzi,Mungu,ni cha milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.

9 Umependa haki, umechukia maasi; KWA HIYO MUNGU, MUNGU WAKO, AMEKUTIA MAFUTA, MAFUTA YA SHANGWE KUPITA WENZIO.

Unaona, Na matokeo ya mafuta yale, ilikuwa si kingine zaidi ya kuwamulikia watu injili ya kweli, kutenda miujiza, kufungua, kukomboa, kuponya n.k.

Luka 4:18 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,

19 Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa”.

Ipo siri kubwa sana katika hilo. Leo hii hatuuoni uhai wa Kristo ndani ya kanisa, kwasababu moja tu, hatuna upendo, wala hatunii mamoja, kila mtu anafikiria mambo yake mwenyewe, na sio ya Kristo. Bwana atusaidie tuufikie umoja wa imani, kama lilivyokuwa katika kanisa la kwanza la mitume. Ambalo kwa kupitia kanuni hiyo waliweza kuupindua ulimwengu kwa kipindi kifupi sana. Kwasababu Mafuta ya Kristo yaliyokuwa yanamiminika katikati yao, yalikuwa ni yale yenyewe kabisa. kwa ule umoja tu na mshikamano waliokuwa nao.

Fikiria ni watu ambao walifikia hatua ya kusema, vitu walivyonavyo sio mali zao binafsi bali za shirika. Je na sisi tunaweza kufikia huko?

Bwana atusaidie sana.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UPAKO NI NINI?

Ukoma wa nyumba ulifunua nini zamani?

Kwanini Kuhani wa Mungu Eli alikufa kwa kuvunjika shingo?

BADO UPO YERUSALEMU TU..GALILAYA HUTAKI KWENDA?

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/24/kwanini-ndugu-wanaokaa-pamoja-wawe-kama-mafuta-ya-haruni/