MUNGU ATAKUUA UKIWA MBAYA MACHONI PAKE.

by Admin | 4 June 2021 08:46 am06

Mwanzo 38:6 “Yuda akamwoza mke Eri, mzaliwa wake wa kwanza, na jina lake huyo mke ni Tamari.

7 Naye Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mbaya machoni pa Bwana; na Bwana akamwua”.

Lazima tukumbuke kuwa Mungu anatazama matendo ya kila mmoja wetu katika hii dunia, Na pale yanapovuka mipaka yake aliyoiweka tujue kuwa tunayahatarisha maisha yetu sisi wenyewe.

Vifuatavyo ni vitu ambavyo, havimpendezi Mungu, na kama vipo ndani yako, basi hakikisha vinaondoka mapema sana. Tulishajifunza huko nyuma lakini ni vizuri tujikumbushe tena, ili visiondoke mioyoni mwetu. Tunavisoma katika..

Mithali 6:16 “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake.

17 Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;

18 Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;

19 Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.

MACHO YA KIBURI:

Kiburi ni kujiona wewe ni bora kuliko wengine, upo juu wa wengine wote, hivyo unawadharau , hutaki kurekebishwa, hutaki kuonywa, hutaki kuwasaidia wengine. watu wa namna hii, ni machukizo mbele za Mungu, katika biblia kulikuwa na mtu aliyeitwa Nabali, ni mfano wa mtu aliyekuwa na kiburi, japokuwa alisaidiwa na Daudi kuangaliwa mifugo yake, lakini bado alimdharau na kumtukana, kisa tu ana mali, na mafanikio, na mwisho wa siku Mungu akamuua. (1Samweli 25:1-38)

Kiburi pia kinachozungumziwa hapo ni kiburi cha uzima. Kisa una afya, ni mzuri, una nguvu, una mafanikio, basi ukielezwa habari za Mungu, wewe ni kudharau, na kudhihaki, na kukebehi, unasema watu wanaomtafuta Mungu ni watu wajinga, wavivu, hawana akili. Kama wewe ni mmoja wapo wa hili kundi la watu, jirekebishe mapema sana, upo hatiani kuuliwa na Mungu.

ULIMI WA UONGO: 

Kilichomfanya shetani apewe adhabu ya kutupwa katika ziwa la moto, ni pamoja na uongo aliokuwa nao tangu mwanzo. Bwana Yesu alisema..

Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; KWA SABABU YEYE NI MWONGO, NA BABA WA HUO”.

Embu fikiria na wewe pale unapokuwa mwongo mwongo kwa kila jambo, unadhani Mungu atapendezwa na wewe? Hawezi kinyume chake unajitafutia kifo tu na hukumu. Uongo unaharibu mahusiano ya mtu na Mungu kwa kiasi kikubwa sana. Tuziponye ndimi zetu.

MIKONO IMWAGAYO DAMU ISIYO NA HATIA:

Kundi lingine ambalo Mungu halipendi kabisa, ni la wauaji. Wengi wanadhani kuwa muuaji ni mpaka utimilize  tendo lenyewe. Hapana, kitendo tu cha kusema nashika silaha,nashika kisu, panga, n.k. na kwenda kuvamia kuiba, tayari wewe ni muuaji, kwasababu hiyo silaha uliyobeba tayari ulishawaza kichwani mwako, endapo ikitokea shida utaitumia kujihamu, ikiwezekana hata kuua. Mambo kama hayo, yanavuta kifo chako cha kiroho na kimwili kwa haraka sana.(Mathayo 5:21-22). Acha matendo yenye harufu za uuaji nyuma yake. Zitakupunguzia maisha yako hapa duniani.

MOYO UWAZAO MAWAZO MABAYA:

Ni moyo ambao hauna fikra chanya kwa Mungu, au katika kuuendeleza ufalme wa Mungu. Badala yake ni moyo ambao unawaza uzinzi wakati wote, unafikiria mbinu ambazo unaweza kupata pesa ukatumie katika anasa. Moyo ambao unaamka asubuhi unafikiri ukafanye kazi ile baadaye ukamalizie siku yote baa.

Moyo ambao unafikiria utapeli, uporaji, dhulma, hauna nafasi hata mara moja kufikiria hatma ya maisha yake ya baadaye, haumfikirii muumba wake, haufikirii kumtolea Mungu, haufikirii kuifanya kazi ya Mungu. Watu kama hawa Mungu anawaua mapema sana, aidha rohoni au mwilini.

MIGUU ILIYO MYEPESI KUKIMBILIA MAOVU;

Kwa kawaida mwanadamu yoyote ni lazima aone ugumu Fulani, katika kutekeleza jambo ambalo sio la haki, ni lazima ashtuke pale anapoletewa habari ya kwenda kuzini na mke wa mtu, anapoambiwa tule rushwa n.k. Lakini kama wewe ni mwepesi wa kukimbilia maovu, mtu anakwambia twende Disko na wewe unakurupuka kuongozana naye, twende tukaibe, unakurupuka kuenda, twende tukazini mume wangu kasafiri, na wewe unaenda, Ujue mwisho wako utakuwa ni mbaya sana, kwasababu miguu hiyo ni mepesi kukimbilia maovu. (Mithali 1:16 , 7:5-27)

SHAHIDI WA UONGO ASEMAYE UONGO;

Huyu ni zaidi ya mtu anayesema uongo. Huyu anaushuhudia kabisa uongo  kuwa ni kweli. Kipindi kile Yezebeli aliajiri watu wamshuhudie uongo Nabothi kwamba amemkufuru Mungu, ili watu wampige mawe afe ili arithi kiwanja chake 1Wafalme 21:1-16

Hata leo hii, wapo watu ni hodari wa kushuhudia uongo, wanafundishwa kusema uongo ili wasitiri dhambi zao, au za wengine, hilo ni jambo baya sana, ambalo linamchukiza Mungu. Bwana atusaidie tusifanyike mashahidi wa uongo.

NAYE APANDAYE MBEGU ZA FITINA KATI YA NDUGU:

La mwisho ndio hili, unatunga uchonganishi katikati ya ndugu wanaomwamini Mungu, ili wachukiane, wagombane, wasiongee, unavunja umoja wao na upendo wao, ambao Bwana Yesu aliwaombea wawe nao katika Yohana 17. Lakini wewe furaha yako ni kuona hivyo. Jambo hilo linamchukiza sana Mungu.

Wakati Mungu anasema,Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Wewe unakuwa mchonganishi..kinyume chake ni kuwa utaitwa mwana wa Ibilisi.

Hivyo tunapoishi hapa duniani tuwe watu wenye Hofu kwa Mungu. Tusiishi kana kwamba Mungu hatuoni.. Anatuona, na tunavyozidi kuwa wabaya ndivyo tunavyoyaweka maisha yetu hatarini. Ni wazi kuwa mtoto wa Yuda, alifanya mojawapo ya dhambi hizo na ndio maana Mungu akamuua. Vivyo hivyo na sisi tujichunguze kama mambo hayo yapo basi tuyaweke mbali na sisi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

TABIA KUU TATU ZA WAHUBIRI WALIORUDI NYUMA NA KUMWACHA MUNGU.

VIKAANGUKA MACHONI PAKE VITU KAMA MAGAMBA.

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/04/mungu-atakuua-ukiwa-mbaya-machoni-pake/