Muhubiri/ Mtumishi yeyote aliyerudi nyuma na kusahau kusudi lake tayari anageuka kuwa nabii wa uongo, kumbuka pia, biblia inapotaja nabii wa uongo, haimaanishi tu mtu Yule mwenye karama ya kinabii, hapana! Bali neno hilo ni neno la kiujumla linaloweza kumaanisha aidha Mwalimu wa uongo, au mchungaji wa uongo, au mtume wa uongo, au muinjilisti wa uongo, au hata muimbaji wa uongo, wote hao ni manabii wa uongo kibiblia.
Leo tutajifunza tabia kuu tatu za wahubiri waliorudi nyuma. Ambapo tukizijua tabia hizo zitatusaidia kujihadhari na upotevu wao.
1. Tabia ya kwanza, huwa hawahubiri na wala hawapendi kuhubiri kuwa hizi ni siku za Mwisho,
2. Tabia ya pili, wanashambulia watumishi wanaohubiri kuhusu siku za mwisho.
3. Tabia ya tatu, ni watu wa kupenda anasa, aidha kwa siri au kwa wazi.
Hizo ndio tabia kuu tatu za manabii, waalimu, wainjilisti, au wachungaji waliorudi nyuma na kugeuka kuwa wa uongo! ambapo kitambo sana walishaliacha kusudi la Mungu na kufuata mambo yao.
Sasa hebu tusome mfano ufuatao ambao Bwana Yesu aliutoa, kuhusu watumishi waliorudi nyuma.
Mathayo 24:44 “Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja. 45 Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? 46 Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. 47 Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote. 48 Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; 49 akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; 50 bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, 51 atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”
Mathayo 24:44 “Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.
45 Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?
46 Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.
47 Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote.
48 Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia;
49 akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi;
50 bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua,
51 atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”
Bwana alitoa mfano huo kwa wanafunzi wake tu!..na kwa makutano yote.. Akimaanisha kuwa unawahusu mitume tu! Na wote ambao wameitwa katika kuifanya kazi ya kulisha kondoo wa Mungu. Huu ni tofauti na ule mfano wa mpanzi, ambao Bwana aliwaambia watu wote, (yaani makutano pamoja na wanafunzi), lakini mfano huu aliwatenga wanafunzi wake na kuwaambia wao peke yao. Na katika mfano huo alilinganisha utumishi aliowapa wa kwenda kuhubiri na utumishi wa mtu aliyeajiri wafanyakazi katika nyumba yake. Ambapo hiyo nyumba inaonekana ni kubwa mfano wa kasri ambayo ina watu wengi (wageni pamoja na wenyeji) vile vile ina wafanyakazi wengi tofauti tofauti, wapo wapishi, wapo wanaofua nguo, wapo walinzi, wapo wanaofanya usafi n.k
Lakini katika huo mfano tunaona mwenye nyumba ni kama alisafiri, na akawaachia majukumu kila mfanyakazi, na hakuwaambia ni lini atarudi, Hivyo kila mfanyakazi kwa nafasi yake alipaswa afanye kwa uaminifu, kwasababu hajui ni lini Bwana wake atakuja. Lakini akatokea mtumwa mmoja miongoni mwao, ambaye kazi yake ilikuwa ni ya upishi, ambapo aliachiwa posho ya kutosha ya kununua chakula apikie watu wa ile nyumba wale kila siku washibe, lakini kinyume chake alipoona Bwana wake anachelewa, alikengeuka na kuanza kuwazuilia chakula watu wa pale nyumbani, lakini haikuishia hapo akaanza kuwapiga wajoli wake, Neno mjoli maana yake ni “mfanyakazi-mwenza”.. yaani mtu anayefanya kazi pamoja na wewe anaitwa “mjoli wako”.
Kwahiyo huyu mpishi akaanza kuwapiga wale wafanyakazi wengine, pengine wale waliokuwa walinzi, au wanaofanya usafi n.k. Na mpaka mtu afikie hatua ya kuwapiga wafanyakazi wenzake maana yake ni kwamba tayari kuna vitu wale wenzake wanafanya ambavyo hakubaliani navyo. Maana yake wenzake ni waaminifu katika kazi zao lakini yeye si mwaminifu ndio maana anagombana nao, na hata kufikia kuwapiga.
Maana yake ni nini mfano huo?
Ukiona mtumishi kasahau Ono la Msingi la kwamba BWANA WAKE ANARUDI SIKU YOYOTE, na kugeukia mambo mengine. Tambua kwamba hiyo ndio dalili ya kwanza ya Mtumishi aliyerudi nyuma.
> Ukiona hakubaliani na kwamba Kristo wakati wowote anarudi, badala yake anahubiri na kuishi maisha kana kwamba Kristo atarudi miaka elfu5 mbele…Jitenge naye! Kwasababu Kitambo sana kashaliacha kusudi lake, na hivyo atakupoteza.
> Ukiona hakukumbushi kwamba siku yoyote kuanzia muda huu parapanda italia, kimbia! Jiokoe nafsi yako.
> Ukiona anakuhubiria vitu vya kidunia tu!..njoo upate mke, njoo upate nyumba, gari, mali.. na wala hakwambii kuwa hizi ni nyakati za mwisho, na dalili zote za kurudi kwake zimetimia.. Jiokoe nafsi yako ndugu!
2. Tabia ya pili: Ukiona anawapiga wajoli wake (yaani wale watumishi wanaosimamia kweli) jihadhari naye. Utauliza anawapigaje?..Anawapiga kwa kuwarushia maneno!!, na kuwadharau. Na ni kwanini anafanya hivyo?.. ni kwasababu ameona wamekuwa waaminifu katika nafasi zao na yeye kashatoka kwenye mstari kitambo, hivyo atakapoona wengine wanahubiri kwa nguvu kwamba Kristo yupo mlangoni, atakwenda kinyume nao kwa nguvu!.. kwasababu yeye bado anatamani udunia. Hiyo ni dalili ya pili.
> Hivyo ukiona anashambulia sana mahubiri au wahubiri wanaohubiri kuhusu kurudi kwa Yesu. Jihadhari na huyo mtumishi. Ukiona anakuambia Yesu harudi leo wala kesho, hivyo endelea na maisha yako kama kawaida, jiokoe nafsi yako!.
3. Na tabia ya tatu na ya mwisho: Ni watu wa kupenda anasa. Katika huo mfano utaona anasema “anaacha kwenda kugawa chakula, anakula na kunywa na walevi”
> Ukiona mhubiri anapenda kusifia sifia vitu vya kiulimwengu kama magari, nyumba, mavazi, umaarufu, mwonekano, hiyo ni dalili mojawapo ya kwamba ni mtu wa anasa. Anaweza asikiri kwa kinywa lakini maisha yake ya siri ni ya anasa. Na mahubiri yake yatakuwa ni ya kutukuza mambo hayo hayo tu!.. Atakuwa anafanya juu chini ili awe maarufu, ili awe na mali nyingi, atabadilisha mpaka mtindo wa mahubiri ilimradi tu akusanye fedha, na umaarufu kutoka kwa watu. Ukiona hiyo dalili, jihadhari kwasababu tayari kasharudi nyuma. Kashaliacha kusudi aliloitiwa.
Lakini Bwana alisema maneno haya..
Mathayo 24:50 “bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, 51 atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”
Mathayo 24:50 “bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua,
Hapo Bwana anaanza kwa kusema “atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua”. Ndugu hao manabii na watumishi wanaokuhubiria kuwa Kristo harudi, wala haji leo wala kesho!!.. Kristo kasema mwenyewe atakuja siku wasiyoidhania… wakati wanadhani ndio wakati wa kujiongezea mali, ghafla Kristo atatokea, na atawakata vipande viwili. Je! Wewe unayewategemea hao utakuwa wapi siku hiyo???. Geuka! Mtazame Kristo yupo mlangoni kurudi, achana na wahubiri hao waliorudi nyuma, hawana tumaini lolote, siku yao itakuja ghafla na Kristo atawahukumu.
Na tena anasema atawakata vipande viwili: Kwanini viwili na si kumi?..na kwasababu wanajifanya kutumika upande wa Bwana na wakati huo huo wanazitumikia tamaa zao (wanatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja), hivyo zamani, adhabu ya mtu anayekamatwa anatumikia falme mbili kwa wakati mmoja ilikuwa ni kukatwa vipande viwili, kwasababu ni mnafiki na msaliti. Hivyo na Bwana atawakata vipande viwili watumishi wote wanaotumikia tumbo na huku wanasimama kuhubiri, atawakata vipande viwili wahubiri wote wanaodharau ujio wake.
Ndugu hizi ni nyakati za mwisho, Yesu anarudi, kizazi tunachoishi ni kizazi cha hatari kuliko vyote, kwasababu dalili zote za kurudi kwake zimeshatimia, Ugonjwa uliosambaa sasa ujulikanao kama corona ni mojawapo ya Tauni zilizotabiriwa kutokea kipindi kifupi kabla ya kurudi kwa Yesu mara ya pili (Soma Luka 21:11), na zaidi ya yote, Israeli imeshakuwa Taifa, wakati wowote unyakuo wa kanisa utatokea.
Luka 12:35 “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; 36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. 37 Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia”
Luka 12:35 “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;
36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.
37 Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia”
Kama hujampokea Yesu, wakati wako ndio sasa na si kesho, hapo ulipo piga magoti, kisha omba rehema kwa Bwana Yesu, naye atakusamehe..na pia acha maovu yote uliyokuwa unayafanya kwa vitendo, kama ulikuwa unatazama filamu za kidunia unaacha na kuzifuta kwenye kifaa chako, kama ulikuwa unazini na kufanya uasherati unaacha kwa vitendo, kama ni binti ulikuwa unavaa vibaya, ikiwemo nguo zinazobana na suruali, na kama ulikuwa unapaka wanja, na kuvaa wigi, hereni, na kujichubua,na mambo mengine yote yanayofanana na hayo ya kidunia unayaacha, na unabeba msalaba wako unamfuata Yesu. Na baada ya hapo, bila kukawia tafuta ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Yesu, kwaajili ya ondoleo la dhambi zako (Matendo 2:38).
Na kama ukifanya hayo yote kwa Imani, Roho Mtakatifu atakuthibitisha kwa kukupa amani, na furaha isiyoelezeka, na pia atakupa uwezo wa kuushinda ulimwengu, na atakuongoza katika kuyaelewa maandiko.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali. Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
MPINGA-KRISTO
THAWABU ZA SIRI, ZA WATAKATIFU MBINGUNI.
NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE
Kikoto ni nini?(Yohana 2:15)
JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.
Rudi nyumbani
Print this post