Waoga ambao hawataurithi uzima wa milele ni watu wa namna gani?(Ufunuo 21:8).

by Admin | 15 June 2021 08:46 pm06

 Ufunuo 21:8 “BALI WAOGA, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Mwoga ni mtu mwenye “hofu”. Na hofu inatokana na kutokuwa na uhakika wa jambo…Mtu anayekatiza mahali Fulani usiku, na hana uhakika kwamba ataimaliza hiyo njia anayoipita salama, kitakachomtawala baada ya hapo katika nafsi yake ni hofu na wala hakuna kingine, kadhalika mtu ambaye hana uhakika kwamba kesho atakula au atapata jambo Fulani, basi kinachofuata kwake ni kuingiwa na hofu vile vile mtu ambaye hana uhakika akifa atakwenda wapi, kitakachofuata kwake ni kuingiwa na hofu na mashaka… hata kama hajijui kama anayo hofu!, lakini tayari anayo.

Hivyo hofu inakuja kutokana na kukosa uhakika wa maisha,… na uhakika huo hauletwi na mwingine zaidi ya mmoja tu, ambaye ni YESU. Kwa kupitia yeye pekee ndiye anayetoa mashaka na hofu yote ndani ya mtu, anaondoa hofu ya maisha yake ya hapa duniani na ya maisha yanayokuja…kiasi kwamba mtu anakuwa hana hofu kabisa na maisha na vile vile hana hofu  ya mauti..

Waebrania 2:15  “awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa HOFU YA MAUTI walikuwa katika hali ya utumwa”.

Hivyo mtu aliye nje ya Kristo anayo hofu!.. hana uhakika kwamba kesho atakula!, hana uhakika kwamba mwezi ujao atakuwa salama, akisikia ugonjwa Fulani umezuka anaishiwa nguvu, akiumwa kidogo anapoteza tumaini lote, kila taarifa inayomjia kwake ni ya mshtuko tu!..kwaufupi kesho yake yote yamejaa mashaka!..

Na hiyo yote ni kwasababu yupo nje ya Kristo!.. na Kristo hayupo ndani yake!.. Kwasababu kama akizama kisawasawa hawezi kuwa na hofu yoyote ile!..anakuwa ni jasiri muda wote.

1Yohana 4:18  “Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo”.

Na kwasababu anakuwa hayupo ndani ya Kristo, basi ni lazima na mambo mengine maovu yatakuwa yanaambatana naye, kama ulevi, uashetari, uzinzi, usengenyaji, tama mbaya, kuupenda ulimwengu n.k … na hivyo hawezi kuurithi uzima wa milele, kwa tabia hizo.

Ufunuo 21: 7  “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8  BALI WAOGA, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Je! Wewe ni mwoga?. Jipime kama una hofu ya kifo!, au una mashaka baada ya kifo utaenda wapi, basi! Kuna uwezekano bado hujakamilishwa katika pendo la Mungu.. Unamhitaji Kristo aingie katika maisha yako ili akupe uhakika wa uzima wa milele.. Uhakika huo utaitupa nje hofu yote.. hutaogopa kufa hata ukiambiwa leo ndio safari yako ya maisha imefika ukingoni, hata ukisikia kuna ugonjwa fulani hatari umezuka, hata ukisikia taarifa zozote za kuogopesha, wewe siku zote utabaki kuwa jasiri, zikija tufani, dhiki, tabu wewe unabaki yule Yule…huogopi ogopi.. Vile vile kama unaogopa wachawi, majini au kulogwa, bado Kristo hajaingia maishani mwako.

Marko 4.39  Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.

40  Akawaambia, MBONA MMEKUWA WAOGA? Hamna imani bado?

41  Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Nasi tukiwa ndani ya Yesu na Yesu akiwa ndani yetu, hofu yote inaondoka!..

 2Timotheo 1: 7 “ Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi”.

Kumbuka tena WAOGA, wote hawataurithi uzima wa milele. (1Yohana 4:18).Hivyo woga pia ni kipimo tosha cha kujijua kama kweli tupo kwenye mstari wa Imani au la!.

Bwana atusaidie na kutubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

Kicho ni nini? (Waefeso 5:21, 2Samweli 23:3)

CHUKI ULIZO NAZO KWA MAADUI ZAKO, SIZO ALIZONAZO MUNGU JUU YAO.

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/15/waoga-ambao-hawataurithi-uzima-wa-milele-ni-watu-wa-namna-ganiufunuo-218/