AOGOPACHO MTU ASIYE HAKI NDICHO KITAKACHOMJILIA.

AOGOPACHO MTU ASIYE HAKI NDICHO KITAKACHOMJILIA.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Silaha moja kubwa ya adui ni Hofu.  Na biblia inatuambia Hofu ina adhabu (1Yohana 4:18).. Leo hii tutaona adhabu kuu ya hofu ni nini..

Tukisoma Mithali Mithali 10:24  Inatuambia..

“Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia;..”

Leo hii kiini cha ukristo hakipo tena katika mafundisho ya wokovu na ufalme wa mbinguni, bali kipo katika elimu za uchawi na uganga. Kiasi kwamba mtu hajui ubatizo wa Roho Mtakatifu ni nini, lakini ukimuuliza kuhusu habari za wachawi anajua A-Z. Hilo jambo ni hatari sana, mimi sipingi uchawi, lakini tuangalie  katika biblia, je! uchawi umepewa uzito gani katika maisha yetu ya wokovu ya kila siku?

Kwanini mitume au Bwana Yesu hakutufundisha au kutusisitiza  sana juu ya siri za wachawi? .Unadhani hawakuwepo? Walikuwepo wengi, lakini waliijua nguvu nyingine iliyo kubwa zaidi ya wao, na ndio hiyo walijikita kuwahubiria watu waiamini, kwasababu walijua hiyo wakishaipata, ni ulinzi tosha, dhidi ya nguvu zote za Yule adui.

Hofu ya uchawi imewashika watu wengi, na kibaya zaidi imewakamata na wakristo waliookoka pia, wao ambao ndio wangepaswa kuwa wakwanza kuzidharau.

Sasa hizi ni baadhi ya hofu za hofu zinazowakamata wengi leo hii;

Kwamfano kama utaona mjusi ndani kwako, na kusema ile ni roho , ujue kuwa hofu hiyo imeshakuvaa.

Kama utaona panya ndani,  au mende, au sisimizi, au konokono, au nzi vitu ambavyo vingehitaji  usafi tu kuviondoa, na ukasema hizo ni roho, ujue kuwa hofu hiyo ipo ndani yako.

Kama utaona paka, na ukahisi ni wachawi wamekutembelea, basi ujue hofu hiyo ipo ndani yako.

Kama utaona, mtu fulani na ukahisi ni mchawi na atakudhuru kwa nguvu za giza, basi ujue hofu hiyo ipo ndani yako. N.k.

Sasa kama biblia inavyotuambia, hofu ina adhabu.. basi ujue adhabu yenyewe ndio hii “Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia;..” hiyo ndio adhabu!!

Ukiona roho ndani ya konokono, ujue kuwa shetani anaumbika nyuma ya konokono huyo, na inakuwa roho hai kweli, na madhara yatakukuta kupitia konokono huyo, kwasababu pepo la hofu ya uchawi umeliruhusul ifanye kazi ndani ya konokono, na hivyo madhara yote yatokanayo na pepo hilo utayapata tu.

Ukiamini, kuwa miti fulani ni ya kichawi, ukweli ni kwamba hilo jambo litaaumbika kwako na madhara hayo utayapata ya kutosha, kama ni kifo utakipata, lakini wakati huo huo  utaona jirani yako anao mti kama huo, na wala hakuna lolote baya linalompata.

Kwasababu hofu yoyote ina adhabu..

Ukiamini panya ndani kwako ndio wanaokusababishia umaskini na usisonge mbele, basi umaskini wako utakujia kwa njia ya hao hao panya, utafunga usiku kucha kuomba, na kukemea, bado hali itakuwa ngumu kwako, panya mwingine atakapokatiza ndani kwako,.. kwasababu umeshafungua mlango wa hofu kwa kupita viumbe hao, lakini jirani yako ataona panya, atakachofanya ni kukumbuka kuwa mazingira yake hayapo safi, hivyo atayaweka sawa kwa kufanya usafi na kutafuta namna ya kuwaua , akaendelea kuishi maisha yake ya furaha.

Hiyo ndio adhabu ya hofu ndugu.. Ukikutana na bundi ukaamini katumwa kukuletea msiba, basi msiba huo utakujia tu kwa mlango wowote,

Kwasababu Biblia inasema Imani ni kuwa na uhakika, wa mambo yatarajiwayo..Ukiwa na uhakika kwamba utapata msiba kutokana na bundi uliyemwona, basi ni kweli utakuja kwa njia hiyo hiyo uliyoamini.

kumbe bundi alikuwa anapita tu katika safari yake usiku na kwa bahati nzuri au mbaya akakutana na wewe, lakini kwasababu wewe umelipa nafasi pepo la hofu ya mauti na uchawi, nalo likapata nafasi kupitia ndege Yule huyo mrembo. Na siku si nyingi unasikia msiba,, na wewe unadhani unabii umetimia, kumbe ni hofu imekuzalia matunda yake, uliyokuwa unayatarajia.

Ndugu ukiwa ndani ya Kristo huhitaji kuishi maisha ya kuogopa ogopa kila kitu, hata kama kweli ni nguvu za giza, zipo ndani yao, lakini Bwana Yesu alituambia..

Luka 16.18 “watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa;..”

Utatumiwa uchawi, lakini hautakudhuru ikiwa upo ndani ya Kristo, utatengewa chakula cha kichawi, kilichotoka kuzimu kabisa, lakini hakitakuwa na madhara yoyote ndani yako, kwasababu nguvu iliyo ndani yako NI KUBWA kuliko yao. Lakini ukianza kuhangaika huko na huko, unafuta kila njia ya kujilinda mwenyewe dhidi ya kila kitu unachokiona, utapata shida nyingi sana hapa duniani, na wala hutaufurahia wokovu wako, hata kidogo.

Kwasababu maisha yako yatakuwa ni ya vita kila siku, visivyokuwa na sababu.

Hivyo  Ikiwa wewe ni mmojawapo wa walioathirika na mafundisho hayo manyonge, ambayo yanahubiriwa kila mahali, nataka nikuambie leo hii anza upya na Kristo, toka kwenye hicho kifungo, kisha jibidiishe katika kusoma biblia, kuliko kusikiliza hadithi hizo za kimila, na za wachawi, na kidogo kidogo utaanza kupata amani moyoni mwako, kama vile biblia inavyosema;

Yohana 8:32 “tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru”.

Shalom!.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312/+255 693036618


Mada Nyinginezo:

JE! PAKA KULIA USIKU NI ISHARA YA UCHAWI?

Ni kosa gani Daudi alilolifanya katika kuwahesabu watu, mpaka kupelekea vifo vya waisraeli wengi?

USIWE NA HOFU, USHUKAPO CHINI.

USIKATE TAMAA UNAPOPITIA MAGONJWA.

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments