PATANA NA MSHITAKI WAKO KWANZA.

PATANA NA MSHITAKI WAKO KWANZA.

Shalom, Biblia inasema;

Luka 12:58 “Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani.

59 Nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho”.

Hapo mwanzoni nilidhani mshitaki wetu ni shetani tu peke yake kama tunavyosoma katika 1Petro 5:8, na Ufunuo 12:10, lakini biblia inatuonyesha kuwa wapo washitaki wengine ambao watatushitaki sisi huko tunapokwenda, ambao sisi hatuwajui..

Ukiuchunguza huo mstari kwa makini, unaposema patanishwa  na mshitaki wako, kabla ya kufika kwa mwamuzi, utajiuliza shetani atapatanishwaje na sisi? sisi hatuwezi kupatanishwa  na yeye kwa lolote kwasababu yeye sikuzote ni mpingamizi na ni adui.. Hivyo wapo washitaki wengine wanaozungumziwa, ambao Bwana Yesu aliwamaanisha hapo,.. Na hao si washitaki, wa kidunia labda wa mahakamani,hapana ni kweli ukisoma hapo alitumia mfano wa washitaki wa kidunia, lakini alikuwa anamaanisha washitaki wengine wa rohoni.

Je washitaki hao ni wakina nani?

Tukirudi nyuma katika mazingira ya Kristo aliyokuwepo, waisraeli wengi walikataa kumsikiliza kwa kisingizio kuwa wanaye Musa, (Wakiwa na maana wanaifuata torati yake, na sio maneno ya tu mwingine yeyote). Lakini kiuhalisia torati yenyewe walikuwa hawaishiki, na kwa mantiki hiyo Bwana Yesu kuna mahali akawaambia maneno haya;

Yohana 5:45 “Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi.

46 Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu”.

Wana wa Israeli hawakujua kuwa Musa wanayemwamini ndiye atakayekuwa mshitaki wao siku ile ya mwisho kwanini hawakuyashika alichowaagiza.. Na ndio maana Bwana Yesu akatumia mfano huo, na kuwaambia patana kwanza na mshitaki wako, Patana kwanza na Musa, patana kwanza na torati, kabla hamjafika kwa kadhi, Kadhi hapo anamaanishi Mungu, katika siku ile ya Hukumu.

Kwasababu ukishajikuta mbele ya kadhi (yaani Mungu) siku ile , kitakachofuata si kingine zaidi ya Hukumu, na ukishahukumiwa utawekwa mikononi mwa mwenye kulipiza,(Askari), ambao ni malaika watakatifu, kisha hao watakukamata, na kwenda kukutupa kwenye ziwa la moto.

Anamalizia kwa kusema..

Ukishafikia hatua hiyo, hutoki huko mpaka utakapolipa senti ya mwisho, maana yake ni kwamba Ukishashushwa kuzimu, habari yako ndio imeisha hapo rafiki, hakuna cha msamaha, hakuna cha dhamana, hakuna cha kulipa kidogo kidogo ukiwa nje..Utaishia huko milele na milele.

JE! NA SISI PIA TUNAO WASHITAKI?

Waisraeli walijifanya kuwa ni watoto wa Musa, hivyo Musa akawa mshitaki wao, vivyo hivyo na sisi, washitaki wetu ni mitume na manabii.. Tunasema sisi ni wakristo, tunayoiamini biblia, tunasema tumejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii  lakini walichokisema mitume baba zetu hatukifanyi katika maisha yetu.. Hao ndio watakaokuwa washitaki wetu. Hizo Injili zao ndizo zitakazotushitaki siku ile..

Na ndio maana biblia inatusisitiza sana, tuhakikishe tunapatanishwa  nao, angali tukiwa hapa katikati njiani, Maana yake ni angali tukiwa angali hapa duniani,hatujafa  bado,  tunayo nafasi ndogo, kabla hatujamaliza mwendo, tuhakikishe, wokovu tunaupata, tuhakikishe tunalizingatia lile andiko linalosema, tafuteni kwa bidii, kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu ambao hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao (Waebrania 12:14). Tuhakikishe hayo tunayo, tuhakikishe tumebatizwa kweli kwa Roho Mtakatifu. Tumetiwa muhuri.

Kwasababu hawa ndio watakaosimama siku ile kutushitaki, kuwa walituambia lakini sisi tulikataa.

Paulo alisema..

Warumi 2:16 “katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu”.

Bwana atusaidie tuitii injili.

Je umeokoka? Je, unaouhakika wa maisha yako ya milele kwamba hata ukifa leo utakwenda mbinguni? Kama sivyo, basi leo tubu, mkabidhi Yesu maisha yako ayasafishe, kwasababu hizi ni siku za mwisho, wote tunalijua hilo, tunaishi katika dakika za nyiongeza tu, dakika za majeruhi, Unyakuo ni wakati wowote, Hivyo sote kwa pamoja tuamke, tumgeukie Muumba wetu.  Ni wakati wa kujitwika msalaba wako wewe kama wewe, na kumfuata  Kristo, ni wakati wa kuchagua lililo la msingi kwanza, na hayo mengine ndio yafuate baadaye kama yanayoulazima. Hii mizigo ya duniani tuipe pumziko kidogo tufanya lililo la kwanza, ili tuwe mahali salama.

Tupatanishwe na washitaki wetu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

NI NINI TUNAJIFUNZA JUU YA MT. DENIS WA UFARANSA?

NYAYO TUNAZOPASWA KUZIFUATA.

WAPE WATU WANGU RUHUSA ILI WAPATE KUNITUMIKIA.

USITAFUTE KUKANWA NA BWANA SIKU ILE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments