Barazani pa Mungu ni wapi? Kama tunavyosoma katika Yeremia 23:18?

by Admin | 1 July 2021 08:46 am07

Jibu: Tusome,

Yeremia 23:18 “Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la Bwana, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia”

Ili tuweze kuelewa vizuri,  hebu tuendelee kidogo kusoma hadi mstari wa 22

“19 Tazama, tufani ya Bwana, yaani, ghadhabu yake, imetokea; ni dhoruba ya kisulisuli; itapasuka, na kuwaangukia waovu vichwani.

 20 Hasira ya Bwana haitarudi, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtalifahamu neno hili kabisa.

21 MIMI SIKUWATUMA MANABII HAO, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.

22 Lakini kama wangalisimama katika BARAZA YANGU, ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya, na uovu wa matendo yao.”

Katika mistari hiyo, Bwana alikuwa anazungumza juu ya manabii wa uongo, ambao hawakuketi kusikia kutoka kwa Mungu bali walijitungia nabii zao na kuwapa watu…na nabii  hizo walizowapa watu hazikuwa zinawafanya watu waache dhambi zao, bali zilikuwa zinawafanya watu wazidi kustarehe katika dhambi, manabii hao wa uongo walikuwa wanawatabiria watu kuwa kuna amani na shwari na Bwana hajawakasirikia ilihali hakuna amani yoyote, na Bwana amewakunjia uso, kutokana na maasi yao.

Sasa ndio Bwana anawaambia wana wa Israeli kupitia kinywa cha Yeremia kuwa.. manabii hao wanaowatabiria uongo, hawakuketi barazani pa Mungu na kusikia Mungu anasema nini, bali wamejituma wenyewe…

Hivyo Barazani pa Mungu panapozungumziwa hapo ni “mahali ambapo Mungu anakutana na watu wake katika roho na kuwapa ujumbe”.

Mfano wa watu walioketi barazani pa Bwana, na kupokea ujumbe ni nabii Isaya..

Isaya 6:1 “ Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.

 2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka…………….

6 Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu;

 7 akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa”.

8 Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.

 9 Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione”

Mfano mwingine ni Nabii Ezekieli, Nabii Danieli na Nabii Musa. Sehemu nyingi, Bwana amemketisha Musa barazani kwake na kumpa ujumbe kwa wana wa Israeli.

Pamoja na hayo, Mungu pia anaketi katika baraza na malaika wake mbinguni, na kuzungumza nao na kuwatuma.. na pia shetani na mapepo wake wanaweza kuhudhuria barazani mwa Mungu kuwashitaki wateule..

Nyakati 2:18 “Mikaya akasema, Sikieni basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto.

 19 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

 20 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani?

21 Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo”

Hivyo katika agano la kale, barazani pa Mungu palifikiwa na wanadamu wachache tu!… yaani manabii wa Bwana!, hao ndio Bwana aliowaita barazani pake na kuwapa ujumbe kwa wana wa Israeli. Lakini katika zamani hizi za agano jipya, Wote waliompokea Roho Mtakatifu wanapakaribia barazani pa Bwana, na kuisikia sauti yake anataka nini pamoja na mashauri yake.  Hatuhitaji tena Nabii Fulani anyakuliwe mbinguni akasikie ni nini Bwana anasema juu yetu, kisha aje kutuambia… Kwasababu tayari Roho Mtakatifu aliye ndani yetu, anatwaa yale yaliyo ya Kristo, katika baraza lake lililo mbinguni na kutupasha habari..

Yohana 16:13  “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

14  Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari”.

Hivyo Baraza la Mungu leo ni Roho Mtakatifu!.. Tukimpata huyo basi, tutajua yote Mungu anayotaka tuyajue, hatutahitaji kunyakuliwa mbinguni tukayasikie..la!, wala hatuhitaji kumshusha Kristo chini aje atuambie! tukiwa hapa hapa duniani tutayajua na kuyasikia..kwasababu Roho Mtakatifu aliye ndani yetu, atatupasha habari..

Warumi 10:6  “Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini), …….

8  Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo”

Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kumpokea Roho Mtakatifu, kwasababu yeye ndio baraza la Mungu. Kwake yeye tunapokea mashauri na maonyo na mafunzo. Na biblia inasema katika Warumi 8:9 kuwa wote wasio na Roho Mtakatifu hao si wake.. ikimaanisha kuwa pasipo Roho Mtakatifu haiwezekani kumwona Mungu.

Na Roho Mtakatifu anafanya kazi kamili kwa aliyemwamini Bwana Yesu, na kuoshwa dhambi zake kwa damu yake. Na aliyebatizwa katika ubatizo sahihi, wa maji mengi na kwa jina la Yesu kulingana na Matendo 2:38.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

Nini maana ya “heri mtu asiyekaa barazani pa wenye mizaha?”

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

ESTA: Mlango wa 4

NINI TUNAJIFUNZA KWA MWANA MPOTEVU NA NDUGUYE?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/01/barazani-pa-mungu-ni-wapi-kama-tunavyosoma-katika-yeremia-2318/