Nini maana ya “heri mtu asiyekaa barazani pa wenye mizaha?”

Nini maana ya “heri mtu asiyekaa barazani pa wenye mizaha?”

 SWALI: Zaburi 1:1 inasema ..“heri mtu asiyekaa barazani pa wenye mizaha”. Je, ni mizaha gani inaongelewa hapo na kuna tofauti gani kati ya Utani na mizaha, na Kama hamna tofauti je hata kutaniana na mtu ni dhambi pia?


JIBU: Kuna mambo ya msingi tunatakiwa tujifunze katika vifungu hivyo, Embu tuvisome tena vizuri..Anasema;

Zaburi 1:1 “Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha”.

Ukitazama hapo utaona vitu vitatu; KWENDA, KUSIMAMA, na KUKETI.

Vyote hivyo tumezuiwa tusivifanya. Hapo inaposema ‘kwenda’ maana yake ni ‘kutembea’. Hivyo kwa namna ya kawaida, tukizungumzia katika Nyanja ya dhambi, Kutembea kuna heri kidogo kuliko kusimama kwenye dhambi, na kusimama kuna heri pia kidogo kuliko kuketi chini. Kwasababu mpaka unaketi ni wazi kuwa unaonyesha ndio umefika, yaani umetia nanga, hapo ndio panakuvutia. Lakini vyote hivyo biblia imetukataza tusivifanye kwa makundi hayo matatu ya watu.

Kundi la kwanza ni la watu wasio haki

Watu wasio haki ni watu ambao hawana habari na Mungu, watu ambao hawana hofu ya Mungu hata kidogo, wapo tayari kutenda mambo maovu bila kujali kuwa ni machukizo mbele za Mungu au la. Hawa tumeonywa tusitembee katika mashauri yao.

Kundi la pili ni wakosaji.

Hawa ni watu wanaovunja amri za Mungu kwa makusudi, wanaweza wakasema wao ni wakristo, au wana hofu ya Mungu, lakini matendo yao, yanawathibitisha wao ni wakosaji utakuta (ni wazinzi, wafiraji, washirikina, wezi, warushi, n.k.) hao nao tumeambiwa tusisimame karibu nao.

Kundi la tatu ni Watu wenye MIZAHA.

Hawa ndio wabaya zaidi kwani sio tu ni waovu, na wakosaji, bali wamevuka hiyo mipaka hadi kufikia hatua ya kuleta mizaha mpaka kwenye mambo matukufu ya Mungu, kudhihaki, kukejeli, kukashfu Neno la Mungu, na wokovu kwa ujumla kwao ni jambo la kawaida.. Biblia inasema..

2Petro 3:3 “Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,

4 na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa”.

Hawa tumeonywa tusiketi nao kabisa, kwasababu wapo mabarazani (maana yake kwenye majukwaa, au sehemu yenye mkusanyiko wa watu).

Ni mara ngapi utaona  watu wanaifanyia biblia comedy kwenye majukwaa na watu wamelipa kiingilio, wameketi pale chini wanacheka na kufurahia, huku wakimtaja Bwana Yesu, au mmojawapo wa manabii wa kwenye biblia, na kuwatolea mifano kana kwamba Yule biblia ni kitabu cha story za vichekesho? Ni mara ngapi umewaona kwenye tv au umewatazama youtube?. Hao tumeambiwa tujitenge nao. Hata tusisikilize vichekesho vyao, kwasababu ni machukizo makubwa mbele za Mungu.

Hivyo tukirudi kwenye swali? Je kuna tofauti gani kati ya utani na mzaha,?

Mzaha ndio unaopelekea utani, hivyo ni vitu vinavyoshadidiana. Na pia sisi kama wakristo, hatupaswi kuwa na mizaha kwenye mambo yanayohusiana na imani zetu, au yanayovuka mipaka ya maadili yetu. Vinginevyo tutakuwa tunatenda dhambi. Biblia inasema hivi;

1Wakorintho 15:33 “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.”

Kitu kimoja kinachoharibu tabia ya Mkristo, ni mizaha… Mtu anayejizoeza mizaha, ndivyo anavyopalilia tabia nyingine mbaya ndani yake kama uzinzi, na uongo..Siku zote uzinzi unaanzia kwenye mizaha na utani uliopitiliza, vile vile tabia ya uongo inafunikwa na kivuli cha utani..

Mithali 26:19 “Ndivyo alivyo amdanganyaye mwenzake, Na kusema, JE! SIKUFANYA MZAHA TU?”

Hivyo tunapaswa tuwe na kiasi kama Mtume Paulo alivyomwonya  Timotheo

2Timotheo 4:5 “Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote,….”

Bali tufurahishwe na sheria za Bwana.

Mithali 19:29 “Hukumu zimewekwa tayari KWA WENYE MZAHA; Na mapigo kwa mgongo wa wapumbavu”

Tukifanya hivyo. Shetani hatatuweza.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

VICHEKESHO NA UTANI MADHABAHUNI

UVUMILIVU WA MUNGU ULIPOKUWA UKINGOJA.

CHEMBE YA NGANO ISIPOANGUKA KATIKA NCHI, IKAFA,

KUNA UMUHIMU WA KUWA MTU WA KURIDHIKA.

Je! ile habari ya watu wawili wenye pepo inajichanganya?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments