APENDAYE FEDHA HASHIBI FEDHA.

by Admin | 8 July 2021 08:46 am07

Mbu ni mdudu ambaye endapo akitua juu ya mwili wa mtu, kama hatasumbuliwa kwa namna yoyote ile, basi atanyonya damu na mwisho wa siku tumbo lake litajaa sana mpaka kupasuka akiwa pale pale ananyonya!..na hapo ndio unakuwa mwisho wa maisha yake!.

Utafiti unaonyesha, kuwa wakati mbu ananyonya damu, mfumo wa taarifa wa tumbo lake na ufahamu wake unakatika, hivyo hajijui kuwa kama hapa kashiba au bado, yeye ile njaa ya kwanza ipo pale pale, anaendeleo kunyonya tu, mpaka anafia pale pale..

Biblia inasema pia katika Mhubiri 5:10 kuwa..

Mhubiri 5:10 “APENDAYE FEDHA HATASHIBA FEDHA, Wala apendaye wingi hatashiba nyongeza. Hayo pia ni ubatili.

 11 Mali yakiongezeka, hao walao nao waongezeka na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu?”

Sio vibaya kutafuta fedha, ni jambo la muhimu, lakini lisiwe jambo linalotawala maisha kiasi kwamba, unapoangalia kushoto, au kulia unaona fedha, au unawaza fedha!. Ukiwa katika hali kama hiyo, nataka nikuambie “kupenda fedha kupo ndani yako hata kama hutakiri kwa kinywa”.

Hekima ya ulimwengu huu inatuambia na kutufundisha, kuwa muda wote tuwaze fedha, tufikiri fedha, tuziishi fedha, tuzitafute lakini hekima ya Mungu haisemi hivyo.. hekima ya kiMungu inasema hivi…

Waebrania 13:5  “MSIWE NA TABIA YA KUPENDA FEDHA; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa”.

Hekima hii kwa ulimwengu inaonekana ni upumbavu!, lakini kwa watu wa Mungu ni nguvu ya Mungu.

Hekima ya kiMungu pia inasema, shina moja la mabaya yote ni kupenda fedha!

1Timotheo 6:10 “Maana SHINA MOJA LA MABAYA YA KILA NAMNA NI KUPENDA FEDHA; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”.

Mtu anayependa fedha anakuwa hashibi fedha siku zote, akipata elfu hashukuru wala haridhiki, atatamani tena laki, akipata laki hali yake ni ile ile, atataka milioni, akipata milioni atataka milioni 100, wala hutaona badiliko lolote kwake, hashukuru wala hatosheki..ni kama mbu anayenyonya damu, pasipo kujijua kuwa tayari tumbo lake limeshajaa na linakaribia kupasuka, yeye anaendelea tu!, mwisho wa siku anapasuka matumbo!.

Ndicho kilichomtokea Yuda, alianza kupenda fedha kidogo kidogo, na kwasababu kupenda fedha ni roho!, ikampelekea asitosheke kuiba fedha iliyokuwa inapatikana katika mfuko wa Bwana!, akapiga hatua nyingine ya kutamani hata apate fedha nyingi zaidi, kwa kumsaliti Bwana Yesu! Pasipo kujua kuwa tayari tumbo lake limejaa na linakaribia kupasuka!, yeye aliendelea kuzisaka fedha kwa nguvu, na ulipofika wakati matumbo yake yalipasuka kama maandiko yanavyosema…

Matendo 1:18  “(Basi mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka.

19  Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata konde lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, konde la damu.)”

Biblia inatuonya tusiwe na tabia ya kupenda fedha.., haijatukataza kufanya kazi!, bali tusiwe watu wa kupenda fedha!…unaweza kuipenda kazi unayoifanya lakini usiwe na tamaa ya kupenda fedha katika hiyo!, kiasi kwamba upate kingi au kidogo!, moyo wako hauutaabiki!!, maadamu umetoa huduma iliyo bora, furaha yako inakuwa ni ule uaminifu katika kazi yako, yaani siku ukiona hujafanya kazi kwa uaminifu ndio moyo wako unauma, na sio siku umeona hujapata faida nyingi!… Na wengi wanaoipenda kazi zao kuliko faida na fedha, ndio wanaofanikiwa kuliko wale ambao kipaumbele chao ni fedha tu!.. Hao wapo tayari mwingine alie ili wao wapate faida, au mwingine adhurike wao wapate fedha, kama Yuda!, wapo radhi wakuuzie hata sumu, au wafanye biashara haramu ilimdari tu matumbo yao yajae…

Ndio maana wanafananishwa na mbu anayenyonya damu!.. mbu ananyonya uhai wa mtu, ambayo ni damu yake..ndio maana mwisho wake unakuwa ni kupasuka matumbo!..

Bwana atusaidie, tuwe watu wa kumpenda yeye zaidi ya kupenda fedha!.

Mathayo 6:33  “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa”

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

KUNA UMUHIMU WA KUWA MTU WA KURIDHIKA.

ONDOA TAKATAKA KATIKA FEDHA, NA CHOMBO KITATOKEA KWA MTAKASAJI.

BWANA AYAGANGE NA MACHO YETU PIA.

MAMA UNALILIA NINI?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/08/apendandaye-fedha-hashibi-fedha/