ONDOA TAKATAKA KATIKA FEDHA, NA CHOMBO KITATOKEA KWA MTAKASAJI.

ONDOA TAKATAKA KATIKA FEDHA, NA CHOMBO KITATOKEA KWA MTAKASAJI.

Shalom, karibu tujifunze Neno la Mungu. Biblia inatuambia..

 “Ondoa takataka katika fedha, Na chombo kitatokea kwa mtakasaji; (Mithali 25:4)

Tunapoiona dhahabu au madini mengine yote, yanang’aa sana, mpaka kufikia kiwango cha kuuzwa kwa thamani kubwa sana, hatupaswi kudhani, huko chini yanapochimbwa yanatoka kama yalivyo. Hapana, mengi ya hayo yanakuwa yamechanganyikana na mawe mengine au uchafu mwingi tofauti tofauti, kiasi kwamba unaweza kukutana na mwamba mkubwa sana, na ndani yake kukawa na kiwango kidogo sana cha dhahabu au fedha.

Hivyo, ili kuitapata dhahabu yenyewe safi, inawagharimu wafuaji wafanye kazi ya ziada, na kazi yenyewe ndio hiyo ya kutenganisha madini hayo kutoka katika hizo takataka nyingine, Zipo takataka ambazo unaweza kuziondoka kwa kuzichuja tu au kupepeta, lakini zipo ambazo itakuhijitaji utumie moto ili kuzitenganisha, kwasababu inakuwa zzimechanganyikana na dini lenyewe hadi ndani.

Hivyo wanachokifanya ni kwenda kuyachoma mawe hayo, kwa joto kali sana mpaka yayeyuke, na yakishayeyuka na kuwa kama uji uji,  ndipo sasa uchafu unajitenga na dhahabu yenyewe.  Kwa kupanda juu, hapo ndipo yule mfuaji anapoondoa uchafu ule,  na atarudia tena hizo hizo hatua kwa jinsi atakavyoweza, na kwa jinsi anatakavyozidi kuondoa takatakata hizo zote hata zile ndogo, ndivyo, mnga’o wa fedha hiyo unavyozidi kuja.. hatimaye, inatokea ikiwa nzuri sana yenye kunapendeza, tayari kwa matumizi yenye thamani.

Mithali 25:4 “Ondoa takataka katika fedha, Na chombo kitatokea kwa mtakasaji;”.

Hivyo na sisi pia kama wakristo, tunapookoka tunakuwa hatuna tofauti na fedha/dhahabu iliyochimbwa katikati ya miamba, tumetolewa huko tukiwa na mambo mengi ya kidunia  ambayo yameshikamana sana na sisi,

Sasa tunapookoka, kanuni ni ile ile inatugharimu tuingizwe katika moto, ili tuwe safi kabisa, Na moto huo anayetuingiza Mungu, na pia tunajiingiza sisi wenyewe.

Hapo ndipo utaona pale tunapokuwa wakristo tu, Mungu anaruhusu tupitishwe katika majaribu mbali mbali ya moto ili tuwekwe safi. Ndio maana biblia inasema;

1Petro 1:6 “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;

7 ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo”.

Yakobo 1:2 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;

3 mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi”.

Unaona, ni jambo la kawaida Mungu, kuwapitisha watoto wake katika majaribu ya namna mbalimbali, lengo sio kuwaangamiza, bali kuwaimarisha Zaidi.

Pia Neno la Mungu linatuambia na sisi wenyewe, tunapaswa tuondoe takataka katikati ya kila kitu tunachokifanya katika maisha yetu ya ukristo ili Mungu aweze kutufanya kama vile anavyotaka, iwe ni katika  huduma zetu, au  shughuli zetu n.k..

Tukitaka tumwone Mungu katikati ya Maisha yetu, tuondoe mambo ambayo hayampendezi, tuondoke uzinzi, tuondoe usengenyaji, tuondoke kuchat chati kusikokuwa na maana mitandaoni, na kutazama muvi muvi zisizotujenga, tuondoe mizaha, tuondoe unafki, tuondoe rushwa, tuondoe uvaaji mbovu,  n.k. Mambo kama haya tukiyazingatia basi Mungu, atatuletea ule mng’ao tunaostahili kuwa nao sisi kama wakristo, na tutakuwa wa thamani nyingi mbele zake na mbele za ulimwengu.

2Wakorintho 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu”.

Kumbuka mambo kama haya kuyaondoa, haihitaji kuwa mlegevu legevu, inahitaji kujiingiza wewe mwenyewe katika moto wako, (kujinyima, kukataa na kuepuka) kila kitu ambacho unaona hakimpendezi Mungu. Hata kama nafsi yako inakitamani vipi, unakipinga. Unakubali kuonekana wa ajabu, lakini moyo wako uwe salama, na faida yake utaiona baadaye.

Vilevile hata katika Maisha yetu ya huduma, ili Kristo atende kazi vema, na ukuu wake uthibitike tunapaswa tuondoe mambo yote  maovu katikati ya kanisa, tusiwe radhi na wazinzi na wapotoshaji katikati yetu, na Mungu atajifunua miongoni mwetu.

Mithali 25:4 “Ondoa takataka katika fedha, Na chombo kitatokea kwa mtakasaji;

5 Mwondoe asiye haki mbele ya mfalme, Na kiti chake cha enzi kitathibitika katika haki”.

Bwana atusaidie sote, Na atubariki.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KUNA UMUHIMU WA KUWA MTU WA KURIDHIKA.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Santuri ni nini? (Danieli 3:5,10)

Fuawe ni nini? Kama tunavyosoma katika Isaya 41:7

NYAYO TUNAZOPASWA KUZIFUATA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments