KWANINI MITUME WAMUULIZE BWANA FARAGHANI?

by Admin | 23 August 2021 08:46 pm08

Yapo mambo mengi ambayo, mitume waliyasikia yakizungumzwa na Bwana, na wakati huo huo wakamuuliza maana yake na wakapewa majibu yake,. Lakini yapo majira ambayo walipoyasikia maneno ya Bwana, hawakuwa na haraka ya kuuliza maswali yao muda huo huo, Bali walimtafuta Bwana faraghani(yaani akiwa peke yake) katika utulivu, ndipo wakawasilisha maswali yao.

Unaweza kujiuliza ni kwanini iwe faragha? Ni kwasababu, walihitaji umakini sana wa kupokea majibu ya maswali yao yaliyowasumbua vichwa.. Na leo tutaona baadhi ya maswali hayo, ambayo na sisi kama wakristo, tunahitaji sana faragha na Bwana ili tuweze kuyaelewa majibu yake, vinginevyo hatutakaa tuelewe kama tutakuwa ni watu wa kuchukulia tu kila kitu juu juu.

Maswali yenyewe tunayasoma katika kile kitabu cha Mathayo 24 Tusome;

Mathayo 24:1 “Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu.

2 Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.

3 Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia”?

Kama unavyoweza kusoma  hapo kwenye huo  mstari wa tatu, biblia inasema walimfuata Bwana kwa faragha, wakiwa wenyewe, muda ambao hakuna masumbufu ya makutano, au ndugu au shughuli yoyote ile.

Wakati ambao mazingira ni tulivu kuna shwari kuu, na Bwana hayupo katika shughuli yoyote ya kihuduma, ndipo kwa pamoja wakamfuata, wakamuuliza hayo maswali makuu matatu yanayohusiana na mwisho wa dunia.

Sasa yafuatilie kwa makini maswali haya, kwasababu kumbuka iliwagharimu mitume “faragha”, kuyaelewa majibu yake. Na ndio maana hawakuyumbishwa na mafundisho ya uongo, yanayohusiana na siku za mwisho, kama ilivyo leo wakristo wengi wanavyoyumbishwa na vitu ambavyo hata havipo katika maandiko, hiyo yote ni kwasababu hatutaki kuwa katika utulivu rohoni kusikia Kristo anasema nini katika Neno lake.

Maswali yenyewe yalikuwa ni haya;

1)Mambo hayo yatakuwa lini?

2) Nayo ni nini dalili ya kuja kwako

3) na ya mwisho wa dunia

1) Tukianzana na swali la kwanza, Mambo hayo yatakuwa lini?

Swali hilo lililenga moja kwa moja, juu ya siku, tarehe, na mwaka, wanafunzi walikuwa wanataka kujua ni “LINI” atarudi, ni lini atakuja kulichukua kanisa lake, tarehe ngapi, mwaka gani na mwezi gani. Ndipo Bwana Yesu akawajibu moja kwa moja swali lao katika ule mstari wa 36-44 na kuwaambia..

Mathayo 24:36 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.

37 Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

38 Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,

39 wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

40 Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;

41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.

43 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.

44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja”.

Unaona hapo? Aliwaeleza wazi kuwa siku hiyo atakayorudi hakuna aijuaye, ni siri ya Mungu, lakini hakuwaacha tu hivyo hivyo hewani waishie kujua hivyo, bali aliendelea kuwaeleza mwonekano wa siku hiyo jinsi utakavyokuwa, kwamba wasidhani siku hiyo kutakuwa na mabadiliko yoyote ya kimwonekano duniani, hapana, itakuwa ni siku kama siku nyingine, watu watakuwa wakila na kunywa, wakipanda na kuvuna, wakiwekeza, uchumi wa taifa ukiimarika, wakioa na kuolewa, kama ilivyokuwa siku za Nuhu na Lutu, lakini ghafla tu, kufumba na kufumbua, Yesu amerudi ameshachukua watakatifu wake amekwenda nao mbinguni.

Kama tu ilivyo leo ndugu yangu,Kristo akirudi leo, huwezi amini, kwasababu, ungetazamia labda, uone ishara Fulani kubwa mbinguni, au watu wengi wakienda kanisani?,Lakini hamna, itakuwa siku kama ya leo, ambayo unaona serikali ikiweka mipango yake, na wanadamu wakijishughulisha na kazi zao za kila siku, ndio hapo wengine watakuwa shambani, wengine vitandani kama alivyosema. Ni siku ya kitofauti sana ambayo Itakuwa nje kabisa na matazamio ya watu wengi.

2) Swali la pili lilikuwa ni nini dalili ya kuja kwako;

Walitamani kufahamu sasa, dalili zitakazoonyesha yupo karibuni kufika. Hapo ndipo utaona akieleza dalili hizo kuanzia mstari ule wa 4-28, kwamba kutatokea manabii wa uongo, matetemeko ya nchi, vita, magonjwa(Corona), kuchipuka kwa Israeli, kuongezeka kwa maasi, akawaambia mkiyaona hayo yote basi mjue nipo mlangoni kurudi.

Mambo ambayo sisi tunaoishi sasa hivi tumeshayashuhudia yote, na wala hakuna hata moja ambalo halijatimia. Hivyo, hiyo ni kutuonyesha kuwa siku yoyote, tutamwona Kristo. Kama vile wanavyosema dalili ya mvua ni mawingu, nasi dalili zote zimeshatimia hakuna asiyejua ni paraparanda tu kulia.

3) Na swali la tatu na la mwisho, lilikuwa ni kuhusiana na mwisho wa dunia.

Walitamani kujua pia, mwisho wa dunia utakuwaje, tukiachia mbali siku ya kurudi kwake, kiama kitakuwaje? Je! Kutakuwa ni gharika kama ilivyokuwa kwa Nuhu, au ulimwengu utaendelea kudumu hivyo hivyo mpaka milele. Lakini tunasoma Bwana Yesu aliwajibu swali hilo katika mistari hii;

“29 Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;

30 ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.”

Siku hii ni mbaya sana, kwasababu jua litakuwa giza, na mwezi kuwa mwekundu, kutakuwa na tetemeko kubwa la ardhi, ambalo litapelekea mpaka visiwa kuhama, hadi watu watatamani milima iwaangukie,wafe, ili tu waikwepe  hiyo ghadhabu ya Mungu.

Siku ya kiama inatisha ndugu yangu. Mpaka Mungu mwenyewe anauliza kwanini mwaitamani siku hiyo? Ni siku mbaya sana ambayo haijawahi kutokea katika historia ya dunia.

Itoshe tu kusema hayo, lakini mambo haya unapaswa uyajue, kuwa siku isiyokuwa na dalili Kristo anarudi, swali ni je! Umejiwekaje ndugu?  Je! Bado upo nje ya Kristo? Kama sivyo basi tubu leo umepokee Kristo, ayabadilishe maisha yako, kisha uwe tayari kubatizwa kwa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako. Ikiwa upo tayari leo kutubu, basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi 0693036618, tuombe pamoja, na vilevile ikiwa unahitaji ubatizo basi fanya hivyo hivyo tutakusaidia.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Mafundisho

MUUNGANO WA DINI NA MADHEHEBU YOTE, UMEKARIBIA.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 10 (Kitabu cha Zaburi).

Je ni lazima kupitia mafundisho ya muda mrefu kabla ya kubatizwa?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/08/23/kwanini-mitume-wamuulize-bwana-faraghani/