Je ni lazima kupitia mafundisho ya muda mrefu kabla ya kubatizwa?

Je ni lazima kupitia mafundisho ya muda mrefu kabla ya kubatizwa?

Jibu: Ubatizo ni tendo linalopaswa lifanyike, haraka sana baada ya mtu kuamini. Tunaposema kuamini tunamaanisha  kumwamini Bwana Yesu kuwa ndiye mkombozi wa ulimwengu, na kumkiri kwa kinywa na kisha kuungama dhambi zote mbele zake.

Hivyo mtu anapoamini tu namna hiyo, hapaswi kwenda kupitia mafunzo Fulani ya ubatizo, la!.. Bali moja kwa moja anapaswa akabatizwe, ikiwezekana siku hiyo hiyo alipoamini, ndivyo maandiko yanavyosema..

Sasa Ili kulithibitisha hilo tunaweza kujifunza mifano kadha katika biblia…

Mfano wa kwanza ni kuhusu habari ya Yule Mkushi-Towashi aliyekutana na Filipo. Maandiko yanasema Mkushi Yule alipoamini, saa ile ile baada ya kuamini alibatizwa..

Matendo 8:34  “Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?

35  Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu. 36  Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37  Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]

38  Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza”.

Umeona hapo?.. Filipo hakumwambia huyu Mkushi, asubiri apitia mafunzo Fulani kwanza ya ubatizo, ya wiki kadhaa, au miezi kadhaa, ndipo akidhi vigezo vya kubatizwa!.. La! Hakumwambia hayo hata kidogo.. Bali alimbatiza pale pale alipoona kuwa tayari kushamwamini Bwana, na yeye mwenyewe yupo tayari..

Mfano wa pili ambao unaweza kuzidi kututhibitishia, ni ule unaomhusu Kornelio na familia yake. Kwani Kornelio aliyekuwa akida wa jeshi la kirumi, aliposikia tu habari za Yesu na kuamini, zilizohubiriwa na Mtume Petro aliamini, na Roho Mtakatifu aliwashukia na baada ya hapo wakabatizwa siku ile ile.. hawakungoja siku nyingine, wala Petro hakuwaambia wakae kwanza chini ya mafundisho ndipo wabatizwe!.. bali tunaona ni siku ile ile walibatizwa..

Matendo 10:44 “ Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.

45  Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.

46  Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,

47  Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?

48  Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha”.

Sehemu nyingine ya mwisho katika biblia inayoweza kututhibitishia kuwa ubatizo unapaswa ufanyike punde tu mtu anapoamini ni katika habari za Yule Askari wa gereza aliyewekwa kuwalinda Paulo na Sila.

Maandiko yanatuambia, mara baada ya Yule askari kuona ishara ile kubwa ya nchi kutetemeka na milango kufunguka, alitaka kujiua, lakini Mungu alimwepusha na hilo na kinyume chake akamwamini Yesu usiku ule ule, na katika usiku ule ule alioamini, alikwenda kubatizwa yeye na familia yake yote!, wala Paulo hakusubiri kupambazuke ndipo akambatize!, bali usiku ule ule alikwenda kuwabatiza.

Matendo 16:25 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.

26  Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.

27  Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia.

28  Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.

29  Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila;

30  kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?

31  Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.

32  Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.

33  Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, KISHA AKABATIZWA, YEYE NA WATU WAKE WOTE WAKATI UO HUO.

34  Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu”

Hapo katika mstari wa 33, maandiko yanasema “KISHA AKABATIZWA, YEYE NA WATU WAKE WOTE WAKATI UO HUO”.. Na sio kesho yake, au asubuhi yake!, bali “wakati huo huo” baada ya kuamini tu!.

Na kama biblia ndio mwongozo wetu na Taa yetu, basi hatuna budi na sisi kufanya kama Mitume walivyofanya.. kwamba mtu anapoamini, hapo hapo anapaswa akabatizwe!, na hapaswi kungojeshwa sana!.

Kadhalika na sisi tulioamini ambao bado hatujabatizwa!.. Ni lazima tuutafute ubatizo haraka sana kwasababu ni tendo la muhimu sana, na lenye madhara makubwa katika ufalme wa giza, ndio maana shetani hataki watu wabatizwe haraka pale tu baada ya kuamini, kwasababu anajua mtu akishabatizwa bali uhalali wa kummiliki Yule mtu unakuwa unapotea.. na yeye, shetani hawezi kuwa tayari kuona anampoteza mtu kirahisi hivyo.

Swali ni je umebatizwa baada tu ya wewe kuamini?.. kumbuka siku zote ubatizo sahihi ni ule wa maji tele, na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na maandiko (Matendo 2:38), na si wa kunyunyiziwa, na vile vile watoto wadogo!, hawabatizwi kwasababu bado hata hawajajitambua na hawajaamua kumpokea Yesu na kutubu!.

Hivyo kama bado hujabatizwa!, ni vyema ukatafuta kubatizwa haraka iwezekanavyo, popote pale unapoweza kuupata!, au kama hujui mahali utakapoweza kuupata ubatizo sahihi kwa haraka, basi unaweza kuwasiliana nasi kwa namba hizi 0693036618/0789001312.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

TOFAUTISHA KATI YA MAFUNDISHO YA YESU, NA YA WAANDISHI.

Nini maana ya kuabudu malaika? (Wakolosai 2:18)

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

Nini maana ya Dirii, Chepeo na Utayari?

Mlima wa Mizeituni  unaumuhimu gani kwetu?

Nini maana ya “Roho za manabii huwatii manabii?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments