REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

by Admin | 1 November 2021 08:46 pm11

Jina la Bwana Yesu libarikiwe, karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu.
Leo tutajifunza, mambo Matatu ambayo, kama Mkristo ukiyarekebisha hayo basi uchumi wako utaimarika zaidi.

1. KUWA MWAMINIFU KWA MUNGU WAKO.

Dawa ya kwanza ya mafanikio yoyote yale, yawe ya kimwili au kiroho, ni kuwa MWAMINIFU KWA BWANA.

Mithali 3:7
“ Usiwe mwenye hekima machoni pako;
Mche BWANA, ukajiepushe na uovu.

8 Itakuwa afya mwilini pako,
Na mafuta mifupani mwako.

Kumcha Bwana ni kuishi maisha matakatifu na yanayompendeza yeye, ambayo Nuru yako inakuwa inaangaza kila mahali.
Jambo moja kubwa wakristo wengi wasilolijua ni kwamba, tumewekwa ulimwenguni ili tuhubiri injili, licha ya kwamba Mungu anataka sisi tupate faida katika mambo yetu kutoka kwake, lakini pia Mbingu inategemea kupata faida kutoka kwetu.. Na faida yenyewe ni sisi kuwavuta wengine waingie katika ufalme.

Kwahiyo maana yake ni kwamba kama wewe unafanya biashara, au kazi yoyote ya kuajiriwa au kujiajiri.. Mungu anategemea maisha yako yawe sababu ya kuwavuta wengine.

Hivyo Bwana akikuamini, atakuvutia watu wengi kwako, kama ni wateja au watu wa fursa wakujie, lengo si tu waje kununua bidhaa zako, au kukupa wewe fursa, bali Mungu anawasogeza kwako ili wapate kuiona nuru yako na wamgeukie Mungu na kutubu..Hivyo wewe unafanyika daraja la wao kumfikia Mungu zaidi.

Lakini kama wewe maisha yako hayana ushuhuda wowote,maana yake ni maisha ya uzinzi, ya wizi, ya ulevi, utukanaji, umbea, usengenyaji n.k.

maana yake Mungu akikuletea watu, ni sawa na kampelekea shetani kondoo..Hivyo ili awalinde watu wake wasizidi kupotea, anazuia wateja wasije kwako, kwasababu utawaharibu kwa tabia zako..na Mungu hapendi watu wake wapotee.

Atawazuia wasije kwako, na atawapeleka kwa watu wengine wenye staha zaidi..Huku nyuma wewe utabaki kufikiri umelogwa, kumbe ni wewe mwenyewe umejiharibu kwa kutokuwa mwaminifu kwa Mungu wako.

Mathayo 5:14
“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.

15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.

16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”.

Angaza Nuru yako ili milango ifunguke.

2. KUWA MWAMINIFU KATIKA KAZI UNAYOIFANYA.

Hili ni jambo la pili ambalo, ni muhimu kulijua.

Wengi wetu hatujui kuwa Mungu si Mungu wa kuwadhuru watu, bali wa kuwapatia watu mema.. Mteja yeyote Mungu anayemleta kwako, ni kwasababu Mungu anataka apate huduma bora ya viwango, ili aweze kumshukuru Mungu baada ya hapo, na Mungu apokee shukrani zake..

lakini hawezi kumleta kwako wewe unayeuza kitu kilichoisha muda wake wa matumizi (kime-expire). Hapo Mungu atakuwa muuaji na mkatili na si Mungu mwenye fadhili..

Alisema..

Mathayo 7:9
“9 Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe?

10 Au akiomba samaki, atampa nyoka?

11 Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”

Hiyo ndio maana watu wateja hawawezi kuja kwako, kwasababu Mungu hawezi kuwaongoza watoto wake kwenda kula sumu, au vitu vilivyo chini ya ubora..vinginevyo atakuwa mwongo hapo aliposema.. “Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”.

Hebu tengeneza picha wewe umeamka asubuhi, na kumwomba Baba akulinde na yule mwovu na pia akupe riziki njema..halafu unatoka hapo Mungu anakuongoza kwenda kununua Soda iliyo-expire! Kwenye duka la mtu fulani…huyoo Mungu si atakuwa mkatili sana?..

Hivyo ili Mungu kumpa mtoto wake kipawa chema sawasawa na Neno lake hilo, atamwepusha kuja kwenye duka lako, au kukupa wewe ajira..badala yake anampeleka kwenye duka lingine au kumpa mtu mwingine ajira ambaye atatoa huduma iliyo bora na kuleta faida katika ufalme wa mbinguni.

Hiyo ndio sababu wakristo wengi Mungu anaifunga milango ya riziki katika biashara zao, au katika mambo yao mengine na kuishia kudhani wamelogwa, na kuzunguka huku na huko kutafuta maombezi kumbe ni kwasababu wao wenyewe sio waaminifu katika kazi zao na hawatoi huduma iliyo bora!.

Na vile vile kuwa mwaminifu katika kumtolea Mungu, maandiko yanasema wote wasiomtolea Mungu zaka ni wezi, wanamwibia Mungu..hivyo Mungu hawezi kuwabariki wezi.

Malaki 3:8 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.

9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote”

Mithali 3:9 “Mheshimu BWANA kwa mali yako,Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.

10 Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya”.

3. IMARISHA KAZI YAKO, AU UJUZI WAKO.

Hili ni jambo lingine pia la muhimu kujua.
Wengi wetu hatupendi kuziimarisha kazi zetu, au ni walegevu katika kuziimarisha, wakati mwingine tukidhani si mpango wa Mungu.

Lakini leo nataka nikuambie kuwa kuiimarisha kazi yako, ni jambo la muhimu sana na la kimaandiko.

Kila siku buni na tafuta mbinu mpya na ongeza ujuzi katika shughuli unayojishughulisha nayo au unayoifanya..hayo ni mapenzi ya Mungu pia!

Bwana Mungu baada ya kuimaliza kazi yake ya uumbaji pale Edeni, alipumzika, lakini baada ya kipindi fulani alinyanyuka tena na kusema..”Si vyema mtu huyu awe peke yake nitamfanyizia msaidizi wa kufanana naye”.Ndipo akamletea Hawa kama msaidizi.

Kadhalika na sisi hatuna budi kusema siku zote “si vyema kazi hii ikabaki yenyewe, basi niongeze nyingine kama hii, na nyingine na nyingine”.

Si vyema kazi hii iwe kama ilivyokuwepo mwaka jana, basi nitaiimarisha hivi na hivi..si vyema ujuzi huu nilionao nikaendelea nao, basi nitauongeza tena na tena..

Kwa kufanya hivyo, Bwana atakubariki kwasababu na yeye pia anafanya matengenez kila siku katika maisha yetu.
Haya ndiyo mambo makuu matatu yanayozuia uchumi wetu kusonga mbele.

Na yaliyo ya muhimu zadi ni hayo mawili ya kwanza.

Tofauti na wengi wanaofikiri kwamba matatizo mengi yanasababishwa na uchawi.

Uchawi wa kwanza shetani anaologa nao mtu sio kuifanya biashara yake isifanikiwe..anachokifanya cha kwanza, na tena anakifanya kwa bidii ni kumfanya MTU AWE MTENDA DHAMBI!.

Kwasababu anajua Dhambi ndio mzizi na chanzo chaatatizo yote na shida na dhiki.

Mtu aliyejitenga na dhambi kamwe shetani hamwezi, na wala hakuna uchawi mwingine wowote utakaoweza kufanya kazi juu yake.

Lakini kama mtu hajajitenga na dhambi, basi uchawi mwingine wowote utafanya kazi juu yake na kumletea madhara.

Swali ni je?

WEWE NI MWAMINIFU KWA MUNGU?…NA JE! NI MWAMINIFU KATIKA KAZI YAKO?..NA JE UMEJITENGA NA DHAMBI?

Kumbuka hakuna mtu yeyote kwa nguvu zake anaweza kuishinda dhambi, Bali tunaishinda dhambi kwa Kumwamini kwanza Bwana Yesu, kwamba yeye ni Bwana na Mwokozi na anaweza kutusamehe dhambi zetu na kutuosha..

Kwa kumwamini huko, na kubatizwa basi yeye mwenyewe anaingia ndani yetu, na kutupa huo UWEZO WA KIPEKEE WA KUSHINDA DHAMBI, ambao unatufanya kuwa Wana wa Mungu.

Yohana 1:12 “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”.

Uwezo huo unatufanya tuwe watu wengine tofauti na tulivyokuwa hapo kwanza..Ndio hapo zile pombe tulizokuwa hatuwezi kuziacha ghafla tunajikuta tunaweza kuziacha, ule uasherati tuliokuwa tunaona ni mgumu kuuacha tunajikuta tunaushinda, yale matusi ambayo tulikuwa tunaona ni mepesi kuyatamka ulimini mwetu tunajikuta hatuyatoi tena vinywani mwetu n.k.

Bwana atubariki.

Maran atha!

Group la whatsapp Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Tafadhali washirikishe na wengine habari

hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/11/01/rekebisha-yafuatayo-ili-uchumi-wako-ukae-sawa/