Biblia inamaana gani inaposema “Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?”

by Admin | 3 January 2022 08:46 pm01

SWALI: Naomba kufahamu Bibliainaposema “Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?” inamaana gani? Kuteka mahekalu ndio kukoje?

Warumi 2:21 “basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?

22 Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?


JIBU: Maneno hayo aliyasema mtume Paulo kwa uweza wa Roho Mtakatifu, lakini hakutoa maelezo marefu, ni kwa namna gani wayahudi walikuwa wanateka mahekalu.

Lakini kulingana na maneno yake, ni kuwa kulikuwa ni desturi mbaya kwa baadhi ya wayahudi waliokuwa wanaishi kwenye mataifa ya wapagani, ya kuvamia mahekalu yao, kisha kuiba miungu yao, ambayo haswaa ilikuwa inatengenezwa kwa vito vya thamani kubwa kama vile fedha, au dhahabu.

Hivyo wenyewe walikuwa wanaviiba  na kwenda kuviuza kama vilivyo , au wanaviyeyusha na kuviuza kama VITO kinyume chake,. Jambo ambalo si tu Mungu alilipinga, bali pia lilikuwa ni kinyume na sheria za watu wa mataifa..

Jambo kama hilo utaliona  likitajwa tena katika ile Habari ya Paulo, alipokuwa kule Efeso, wale watu walipoleta vurugu kwasababu ya Paulo kuhubiri habari ambazo zinakinzana na ibada za miungu yao. Utaona pale walipopeleka mashitaka, wale waamuzi hawakuona kosa lolote juu ya akina Paulo,..Na moja ya makosa ambayo walitazamia kuyaona kwa mitume, ni hilo la kuiba vitu vya mahekalu yao.

Matendo 19:36 “Basi kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, imewapasa kutulia; msifanye neno la haraka haraka.

37 Kwa maana mmewaleta watu hawa, wasioiba vitu vya hekalu wala kumtukana mungu mke wetu”.

Sasa tukirudi katika swali, kwanini Mtume Paulo aliposema “Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?”, Alimaanisha kuwa Ikiwa umeamua kutojihusisha na ibada za sanamu, iweje basi uibe vitu vyao na kuvifanyia biashara?.. Je! Kuna tofauti yoyote na wale wanaovifanyia ibada?

Mungu alishakataza tabia kama hiyo katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati, soma;

Kumbukumbu 7:25 “Sanamu za kuchonga za miungu yao mtaziteketeza kwa moto; usitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala usiitwae iwe yako usije ukanaswa nayo; kwa maana ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako”;

Hii inatufundisha nini?

Tukikataa dhambi Fulani basi tusiwe wanafki, kuitenda katika maumbile mengine..Kwamfano,  tukisema hatunywi pombe, hatupaswi kwenda kuiba/kuchukua chupa za bia na kwenda kuziuza..Ikiwa hatuvuti sigara, hatupaswi pia kwenda kununua HISA za sigara, katika masoko ya fedha,  kisa tu zina faida kubwa. Ikiwa hatuzini, hatupaswi pia kufanya biashara za guesthouse kwa wazinzi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Maashera na Maashtorethi ni nini?

Bwana aliposema kuwa yeye ni “Mungu wa miungu” alikuwa na maana gani?..je! yeye ni Mungu wa sanamu?

Je! ni sahihi kwa mkristo kujifukiza?

Maswali na Majibu

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/01/03/uchukiaye-sanamu-wateka-mahekalu/