Bwana alimaanisha nini kusema “kila mtu atatiwa chumvi kwa moto”

by Admin | 16 January 2022 08:46 pm01

SWALI: Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “kila mtu atatiwa chumvi kwa moto.” (Marko 9:49)


JIBU: Kama tunavyofahamu kazi kubwa ya chumvi ni kiungo, kiasi kwamba chakula kinaweza kikawa ni kizuri kweli, kinavutia kwa macho, kina harufu nzuri, lakini kikikosa chumvi huwa kinapoteza ladha yote, haijalishi kilitengenezwa kwa viungo vingi kiasi gani.

Vivyo hivyo na sisi kwa Mungu, ili tuwe tumestahili kuingia katika ufalme wake wa mbinguni, ni lazima tuwe kama chakula kilichokamilika kwake, tukikosa ladha tu ya chumvi yake, kamwe hatuwezi kuuingia ufalme wake.

Sasa ili kuelewa vizuri chumvi hiyo tunaipate, au inakujaje kujaje ndani yetu, tusome Habari yenyewe, kuanzia vifungu vya juu yake kidogo, ili tupate picha kamili;

Marko 9:43 “Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika;

44 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.]

45 Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; [

46 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.]

47 Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum;

48 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.

49 KWA SABABU KILA MTU ATATIWA CHUMVI KWA MOTO.

50 Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi”.

Umeona, baada ya maagizo hayo, mwishoni kabisa Kristo ndio anasema na sisi tutatiwa chumvi lakini si kwa kitu kingine bali kwa MOTO.

Na moto wenyewe ndio huo, aliokuwa anauzungumzia hapo juu, kwamba kiungo chako kimoja kikikukosesha kikate, unapokata kiungo chako, utasikia maumivu kweli, lakini ndio tiba ya kukufikisha mbinguni, ndio chumvi yenyewe inayokufanya ulete ladha mbele ya Mungu.

Hiyo ikiwa na maana kuwa, hata wewe, binafsi unafahamu kabisa vipo vitu ambavyo vinakukosesha vinakufanya usimrudie Mungu wako kikamilifu, inawezekana ni kazi Fulani, au kampani ya marafiki zako walevi, au wahuni, au wadada wenzako wadadisi, au ndugu zako, au binti yule, au kijana yule. Kumbuka Bwana amekupa amri hii, ikiwa wanakufanya uikose mbingu,  Achana nao, haraka sana bila kuangalia nyuma.. wakatae..

Ni kweli inauma,unapoviacha hivyo vitu, au unapowaacha ni moto utausikia, lakini ndivyo unavyotiwa chumvi na Bwana. Kwasababu usipoukubali moto huo sasa, utakutana nao siku ile utakaposhuka Jehanum ukifa.

Huu si wakati, wa kuikumbatia dhambi hata kidogo, si wakati wa kumwangalia mtu Fulani anasema nini juu ya Maisha yako ya milele, mbinguni utakwenda peke yako, vilevile usipotubu jehanumu utakwenda peke yako. Ni heri upitie shida hapa duniani, kule ukaishi milele kwa rah a na Mungu, kuliko kupitia raha za kitambo hapa duniani, halafu kule ukaishia motoni milele.

Hivyo ndugu yangu kubali kutiwa chumvi sasa, kwa kukubali kuacha yale ambayo yameshikamana sana na wewe kwa wakati huu wa siku za mwisho.

Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu”,

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

“Ninyi ni chumvi ya dunia” Andiko hilo lina maana gani?

OLE WAKO KORAZINI NA BETHSAIDA.

Nini tofauti kati ya moyo na roho?

UNYAKUO.

EZEKIELI, ITABIRIE MIFUPA MIKAVU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/01/16/kwsababu-kila-mtu-atatiwa-chumvi-kwa-moto/