Nini tofauti kati ya moyo na roho?

Nini tofauti kati ya moyo na roho?

Moyo ni neno ambalo linaweza kuwakilisha aidha nafsi ya mtu au roho ya mtu, inategemea na linapotumika.

Kwa kawaida hakuna lugha ya kuielezea nafsi ya mtu jinsi ilivyo, au roho ya Mtu jinsi ilivyo, kwamba inafananaje, au iko namna gani, hivyo lugha nyepesi ambayo inaweza kuwakilisha vitu hivyo viwili (yaani Roho na Nafsi) ni Moyo.

Kama vile tunavyokosa lugha ya kuzielezea nguvu za Mungu zikoje zikoje, au uweza wake ukoje ukoje, una  rangi gani, una mwonekano gani, au unafanyaje kazi, hivyo tunaishia tu kusema “mkono wa Mungu umefanya hichi au kile”… tukimaanisha kwamba Nguvu za Mungu zimetenda hayo au uweza wa Mungu umefanya hayo. Hapo tumetumia kiungo cha mwili kuwakilisha kitu Fulani cha rohoni kisichoonekana. Na lengo la kufanya hivyo ni ile kitu kile kiweze kueleweka zaidi na kuleta maana.

Ingawa si wakati wote tutaziwakilisha nguvu za Mungu kwa “mkono wake” lakini pia tukitumia “mkono wa Mungu ” kuwakilisha “nguvu za Mungu” tutakuwa hatujakosea.

Na ni kwanini tunatumia  kiungo mkono na si mguu??… Kwasababu mkono ndio unaofanya mambo yote, mkono ndio unaotumika kutia sahihi ya jambo Fulani liwe baya au zuri.. Hivyo mkono siku zote unawakilisha mamlaka ya Mtu au nguvu zake.

Kadhalika ili ipatikane  lugha rahisi ya kuwakilisha roho ya mwanadamu au nafsi yake, ambayo haionekani kwa macho, ndipo lilipotumika neno “moyo” kama mbadala, Kwamfano badala ya kusema “Nina huzuni nyingi rohoni” unaweza kusema “nina huzuni nyingi moyoni”. Au badala ya kusema “nafsi yangu ina huzuni” unaweza kusema “moyo wangu una huzuni” ni kitu kile kile.

Sasa kwanini kitumike kiungo moyo na si kiungo kingine kama figo:

Kama tunavyojua kiungo pekee kinachoendesha na kuzungusha damu katika miili yetu ni moyo. Na ndio  kiungo pekee ambacho ni chepesi kuitikia mabadiliko yoyote ya hisia za mwili. Utaona likitokea jambo la kushtusha ghafla, mapigo ya moyo yataanza kwenda kasi!..pakitokea hali ya utulivu sana, mapigo ya moyo yanashuka.. Ni ngumu mtu ashtushwe halafu asikie maini, au figo zinabadilika tabia.. Moyo ni kama vile mtu mwingine wa pili, anaishi ndani ya mwili.

Hivyo tabia hiyo ya kipekee ya kiungo hicho ambacho kipo ndani ya mwili lakini kina uwezo wa kuitikia na kuelewa mambo yanayoendelea nje ya mwili, na zaidi ya yote ndicho kinachozungusha uhai ndani ya mwili, imekifanya kifananishwe na roho au nafsi ya mtu.

Kwahiyo popote pale katika maandiko neno hilo “moyo” linapotumika.. basi fahamu kuwa linawakilisha aidha “nafsi ” au “roho”. Kujua tofauti iliyopo kati ya nafsi na roho unaweza kufungua hapa >> Tofauti ya Nafsi, mwili na roho

Je umempokea Yesu?. Je umempenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nguvu zako zote? Au unautumikia ulimwengu na fahari zake?..Kumbuka biblia inasema..

Mathayo 6:21 “kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako”.

Moyo wako upo wapi leo? Kama upo kwa Bwana ni vyema..lakini kama upo katika ulimwengu na fahari zake, kumbuka maandiko yanasema…

Yakobo 4:4 “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu”

Ndugu kitendo cha kuipenda dunia tu tayari wewe ni adui wa Mungu, haihitaji useme kwamba wewe ni adui wa Mungu, hapana! Kitendo cha wewe kupenda fasheni tu, kitendo cha wewe kupenda kuvaa nusu uchi, kitendo cha wewe kuwa mshabiki wa mipira, kitendo cha wewe kupenda kutazama tamthilia na filamu za kidunia, tayari umejifanya kuwa adui wa Mungu. Na maadui wa Mungu wote! Sehemu yao itakuwa ni lile ziwa la Moto..(Luka 19:27).

Kama utapenda kumpokea leo Yesu, mlango wa neema upo wazi, ila hautakuwa hivyo siku zote..ipo siku utafungwa, tukiwa hapa hapa duniani, utafungwa kwa tendo linalojulikana kama unyakuo. Baada ya unyakuo kupita, kitakachokuwa kimebakia duniani ni dhiki kuu tu!, na baada ya hapo ni mapigo ya vitasa saba kama tunavyosoma katika Ufunuo 16. Duniani patakuwa si mahali salama kabisa. Hivyo kama upo tayari kumpokea Yesu maishani mwako leo, hapo ulipo jitenge kwa dakika chache tafuta sehemu ya utulivu kisha Ungama dhambi zako kwa kumaanisha kukiri makosa yako na kuyaacha. Baada ya hapo, acha vyote kwa vitendo ulivyokuwa unavifanya… Acha udunia wote!! Na hatua ya  mwisho tafuta ubatizo sahihi kukamilisha wokovu wako, Ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu, kulingana na maandiko (Matendo 2:38)

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

SHETANI ANAPOKUINGIA, ANATIA MOYO MGENI NDANI YAKO.

JINSI YA KUEPUKA KUUMIZWA MOYO KUSIKOKUWA NA SABABU.

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

nini maana ya kujikana nafsi na kujitwika msalaba?

NGUVU ZA ZAMANI ZIJAZO:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments