SHETANI ANAPOKUINGIA, ANATIA MOYO MGENI NDANI YAKO.

SHETANI ANAPOKUINGIA, ANATIA MOYO MGENI NDANI YAKO.

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tuyatafakari maneno ya uzima, ambayo ndio chakula cha kweli kutupacho afya roho zetu.

Lipo jambo moja nataka tujifunze leo linalohusiana na utendaji kazi wa shetani pale anapopata nafasi ya kumwingia mtu. Katika biblia tunaona Yuda ndiye mtu wa kwanza aliyerekodiwa kwa uwazi kabisa kuingiliwa na shetani. Tunalisoma hilo katika

Luka 22:3 “Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara.

4 Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao”.

 Na matokeo ya yeye kuingiliwa kule na shetani ilipelekea kutiwa moyo mwingine na ibilisi ambao yeye mwenyewe hakuwa nao kabisa.. Na moyo wenyewe ulikuwa ni moyo wa kusaliti.

Yohana 13:1 “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo.

2 Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti;”

Sasa moyo kama huu ukishaingia ndani yako, huwa haujali kitu kingine chochote, huwa haufikirii kwamba huyu ni ndugu yangu, au huyu ni mama yangu, au huyu ni jirani yangu, au huyu ni mwenye haki,au nani n.k. wenyewe kazi yake ni kuvuruga, kuharibu, kusaliti, kuchinja kama sio kuua kabisa. Kwasababu si moyo wa mwanadamu tena unaofanya kazi ndani ya mtu bali ni moyo wa ibilisi mwenyewe ule wa kuasi.

Ndicho kilichomtokea Yuda, alipoingiwa na moyo huo, hakujali kuwa Yesu alimpenda Upeo kama tulivyosoma hapo juu, mpaka akamfanya kuwa msiri wake, na kumpa tonge lake alilolipenda yeye peke yake.. Lakini kinyume chake ni kuwa alimwinulia kisigino chake, akaenda kumsaliti kwa maadui zake, tena mbele ya macho yake kwa kumbusu. Usifikiri ule ulikuwa ni moyo wa Yuda.. Haukuwa moyo wake hata kidogo,  na ndio maana baadaye shetani alipomwacha, alijuta sana na mwisho wa siku akaenda kujinyonga.

Zaburi 41:9 “Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake”

Moyo huu huu ndio utakaomwingia mpinga-Kristo siku ile ya mwisho, ambaye kazi yake itakuwa ni kuchinja tu wale wote ambao hawana ile chapa ya mnyama. Na baadaye itamtoka na kuyaendea mataifa ili kuleta vita duniani.

Ufunuo 16:13 “Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.

14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.

Leo hii unaona watu wanafanya mauaji makubwa ya kinyama, na kuchinja watu, au kuwatoa ndugu zao kafara usidhani ni mioyo yao inafanya hivyo. Hao ni watu ambao tayari walishamfungulia milango shetani tangu zamani ya kuwaingia, na matokeo yake shetani naye akawawekea mioyo mingine ndani yao, ambayo haijali utu tena, au haithamini kitu chochote, haijalishi itaonyeshwa upendo mkubwa kiasi gani.

Na kwa kawaida mwisho wa siku watu hawa huwa wanaishia katika majuto makubwa sana, pale ambapo wanajiona wameishia katika dhiki, au vifungo, au kukaribia kuuliwa, kutokana na makosa yao, wakati huo shetani ameshawaacha..ndipo wanaposhangaa ilikuwaje walijihusisha katika mambo kama hayo.

Mpaka mtu anafikia hatua ya kuzini zini ovyo hajali chochote, hajali huyu ni mke wa mtu, au mume wa mtu, hajali maradhi, hajali kuwa ni machukizo kwa Mungu, hata wakati mwingine anafanya hivyo na wanyama, au watu wa jinsia moja na yeye, huo ni moyo mwingine wa ibilisi umeshakwisha kuingia ndani yake. Na mwisho wa siku itakuwa ni majuto tu kwake.

Tukumbuke kuwa Yuda alikuwa ni mtume aliyechaguliwa na Yesu mwenyewe, lakini kwa uzembe wake, yalimkuta mambo kama yale, hiyo ni kutufundisha kuwa hata sisi tunaosema tumeokoka yanaweza kutukuta endapo tutakuwa ni watu wa kumpa ibilisi nafasi au upenyo ndani ya maisha yetu.

Tusidhani kuwa tukishafikia hatua hiyo itakuwa ni rahisi kumshinda ibilisi, hilo haliwezekani. Hivyo tuwe makini sana. Tukisema tumeokoka tumaanishe kweli kweli, Yuda alianza na tabia ndogo sana ya wizi, ambayo hakuna mtu aliyejua ingempelekea hata kusaliti na mwisho wa siku kujinyonga. Na sisi mambo madogo madogo tunayoyakumbatia hayo ndiyo yatakuwa upenyo wa ibilisi kutuingia na kuweka mioyo mingine ndani yetu.

Bwana atutie nguvu sote katika safari yetu hii ya wokovu.

Swali ni je, umemwamini Yesu? Je amekusafisha dhambi zako kwa damu yake?. Kama sivyo, unasubiri nini?  Una habari kuwa hizi ni nyakati za mwisho? Na shetani naye analijua hilo na ndio maana anafanya kazi zake kwa bidii kukuingia mtu kama wewe mwenye mawazo mawili, kukutia moyo mwingine ndani yako, kwasababu anajua wakati alionao ni mchache?.

Ufunuo 12:12 “..Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu”.

Huu ni wakati wa kuamka katika usingizi wa mauti, na kumgeukia Kristo, na kumaanisha kweli kumfuata yeye, hivyo tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha, kisha kuwa tayari kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo ikiwa hukubatizwa hapo kabla. Na baada ya hapo Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, atakayekulinda na kukuongoza katika kweli yote.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “Mwenye hekima huvuta roho za watu”.

JINSI YA KUEPUKA KUUMIZWA MOYO KUSIKOKUWA NA SABABU.

Nini maana ya ‘Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu’ ?

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
M
M
2 years ago

Amen