JINSI YA KUEPUKA KUUMIZWA MOYO KUSIKOKUWA NA SABABU.

JINSI YA KUEPUKA KUUMIZWA MOYO KUSIKOKUWA NA SABABU.

Mhubiri 7:20 “Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.

21 Tena, usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa; usije ukamsikia mtumwa wako mwenyewe ali anakutukana.

22 Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana watu wengine”.

Kitabu cha Mithali na Mhubiri ni vitabu vilivyojaa mafunzo mengi ya maisha ya kawaida, tukiachilia mbali yale ya rohoni.  Vitabu hivi vimeandikwa na mtu mmoja ambaye ni Sulemani. Hivyo leo tutaangalia jambo moja la kujifunza kwenye maisha yetu ya kawaida sisi kama wakristo.

Kama tunavyosoma hapo katika mstari wa 21 na 22 inasema “usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa”… Sasa ni jambo la kawaida kwa kadiri tunavyoishi hapa duniani, kupitia katika hali tofauti tofauti, kuna wakati utapitia hali ya kuzungumziwa vibaya, kusengenywa, haijalishi utakuwa ni mwema, au umefanya mazuri kiasi gani, hilo haliepukiki, hata kama wewe ni mtakatifu vipi?.

Sasa biblia inatuambia, tunapokuwa katika mazingira kama hayo, tusitie moyoni kila kitu tunachokisikia, au kwa namna nyingine tuvipuuzie, haijalishi tulichoambiwa kinachoma  kiasi gani, hiyo ni kwa faida yetu wenyewe..

Lakini tatizo linakuja kwetu pale ambapo tunakisikia kidogo tu tumezungumziwa vibaya, na sisi hapo hapo tunaanza kutafuta, ni nani huyo kasema, ni nani kamwambia, na kama hiyo haitoshi tunaendelea kutafiti na yule aliyemwambia ni nani kamweleza, na yule aliyeelezwa katolea wapi taarifa hizo, na kwanini wamefanya hivyo, hivyo tunaendelea, mpaka unazalika mlolongo mrefu ambao hauna mwisho.

Sasa ukisoma mstari wa 22 utaona unatupa madhara ya kufanya hivyo na kutuambia ikiwa mtu ataendelea kutafuta tafuta hivyo, kuchunguza chunguza hivyo.., kutafuta mchawi ni nani,.mwisho wa siku atashangaa kusikia mambo ambayo asingetazamia kusikia kutoka kwa watu wake ambao hawategemei kabisa.. Ukisoma hapo anatumia mfano wa “mtumwa”, mtu ambaye ni mjakazi wake anayekuheshimu atasikia  anamtukana..

“21 Tena, usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa; usije ukamsikia mtumwa wako mwenyewe ali anakutukana”.

Hivyo kabla hujaanza kuyafikiria mambo ya wanadamu, utakapoona habari fulani inakujia ya kusemwa vibaya, ikwepe, au ipuuzie kabisa kwa usalama wa moyo wako, kisha endelea na shughuli zako za kawaida, Watu wengi (hususani wakristo) wanaohangaika huku na huko kutafuta ni nani aliyewasengenya au Yule anazungumzia nini kuhusu mimi, mwisho wa siku wanakuwa na vinyongo na watu wote, wanakuwa na chuki zisizokuwa na sababu, wanapoteza hata imani na Mungu na kuanza kuishi maisha ya visasi, maisha ya kutokusamehe, na Maisha ya uchungu, hata maombi yao yanakuwa ni ya kuwalenga tu maadui zao,  mawazo yao ni kukomoa tu, nipate hiki nimfundishe yule adabu n.k. kisa tu alimsikia Fulani akimcheka.. Na pia kamwe hawawezi kuwa na maombi ya unyenyekevu mbele za Mungu, bali ya kunung’unika tu na kulalamika.

Na kumbe hajui yule mtu aliyemsengenya pengine hata hakuwa na chuki na yeye kwa kiwango hicho anachokifikiri yeye, alizungumza tu kama mwanadamu ambaye hawezi kuuzuia ulimi wake, na pengine alishatubu na akawa anamuombea, lakini yeye kwa kuwa alishasikia fulani alimzungumzia vibaya, hilo jambo ataendelea nalo moyoni mwake kwa miaka na miaka..Atasema kwanza yule nilishawahi kumsikia akinisema hivi au vile.

Hivyo kabla hatujamkasirikia fulani kwasababu ya kutuzungumzia vibaya, tunapaswa tujiulize je na sisi hapo nyuma hatujawahi kumsengenya mtu yeyote katika maisha yetu?. Kwasababu Ule mstari wa 22 unasema;

“21 Tena, usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa; usije ukamsikia mtumwa wako mwenyewe ali anakutukana.

22 Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana watu wengine”.

Unaona? Imetumia neno “mara nyingi”. Pengine hata wewe ulishawahi kuzungumza maneno ambayo usingeweza kuyasema mbele ya huyo jirani yako, Lakini akija mbele yako humwekei vinyongo.

Hivyo na sisi pia tunapaswa tuachilie, tusiwe wapelelezi sana kwa yale tunayoyasikia kuhusu sisi, ukisikia mtu anakuambia fulani kakuzunguzia hivi au vile, usitake kujua zaidi ya hapo.. Kwasababu utajikuta una chuki na kila mtu, pengine hata mke wako, au dada yako, au mwanao, kwa sababu hiyo tu ya udadisi.

Tunapaswa tufahamu tu, kuzungumziwa vibaya au kusengenywa ni sehemu ya maisha yetu maadamu tupo hapa duniani. Hivyo hakuna haja ya kufuatilia fuatilia. Hiyo kazi tumwachie shetani, Sisi tutafute mambo msingi ya imani yetu. Na kamwe hutapata mtu mkamilifu asilimia mia moja hapa duniani, kama unayemtaka wewe, tukilielewa hilo tutaishi Maisha ya upendo na furaha sana.

Bwana atusaidie katika hilo kwenye safari yetu ya wokovu.

Je! Umeokoka? Je! Unajua kuwa hizi ni nyakati za mwisho? Na kwamba hatutakuwa na muda mrefu sana Unyakuo utapita, na mwisho wa dunia utafika? umejiandaaje? Je! Bado upo vuguvugu? Ikiwa hujamkabidhi Yesu maisha yako ni heri ufanye hivyo sasa. Na wokovu unakuja kwa kutubu dhambi zako na kwa kubatizwa ipasavyo hivyo, zingatia hayo na uyakamilishe. Kwani hizi ni dakika za majeruhi. Bwana yupo mlangoni kurudi.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group


Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
CHARLES JAMES MBAGWA
CHARLES JAMES MBAGWA
1 year ago

Nayapenda sana mafundisho yako Mungu akubariki sana