KOIKOI ANGANI AJUA NYAKATI ZAKE ZILIZOAMRIWA.

KOIKOI ANGANI AJUA NYAKATI ZAKE ZILIZOAMRIWA.

Yeremia 8:7 “Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana”.

Koikoi, mbayuwayu na korongo ni ndege wa ajabu sana, ni ndege wenye uwezo wa kusoma majira ya dunia, Na hiyo imewasaidia sana, kuishi maisha ya salama salmini huku duniani, pasipo kukumbana na changamoto zozote  zisizo na maana.

Hawa ni ndege ambao kikikaribia kipindi cha baridi wanahama wote waeneo yao wanayoishi kwa muda, na kusafiri umbali mrefu sana, kwenye pembe ya pili ya dunia kutafuta msimu tulivu aidha wa vuli au  wa joto ulipo wakatulie, kisha baadaye hali ya baridi ikishakwisha wanarudi katika makazi yao ya awali kuendelea na maisha yao ya kawaida.

Kumbuka baridi tunayoizungumzia ni ile baridi haswaa, ya kutengeneza barafu iliyopo huko nchi za ulaya, ambayo hata mtu wa kawaida akikaa nje masaa machache tu anageuka kuwa jiwe la barafu, haijalishi atavaa masweta makubwa kiasi gani.. Baridi ya namna hiyo watu wanaoishi huko wanatumia muda wao mwingi kuwepo ndani, na hata kazi zao wanazifanyia ndani katika nyumba zilizojengwa kitaalamu kuhifadhi joto ndani, kwani nyumba za kawaida kama hizi zetu, kule hazijengwi kwasababu zinapitisha baridi, kiasi kwamba ukibaki ndani yake, ukakaa huko mpaka asubuhi ukiamka umeganda. Huku kwetu Afrika hatuna baridi ya namna hiyo.

Sasa, ndege hawa, wanaelewa kabisa kwa namna ya kawaida hawawezi kuishi katika mazingira hayo ya baridi kali, kwasababu hata viota vyao vitaganda.. Sasa ili kulitatua hilo tatizo inawagharimu wahame kwa muda, ndio hapo wanasafiri maelfu ya kilometa wanakuja mpaka huku kwetu Afrika, au nchi nyingine zenye joto, wanakaa  huko mpaka msimu wa baridi  utakaposhakwisha kule Ulaya ndio wanarudi sasa, kuendeleza maisha yao ya sikuzote.

Sasa Mungu ametumia mfano wa ndege hawa wasio na akili, kutushangaa sisi wanadamu wenye akili timamu kwanini hatujui hukumu zake alizoziweka hapa duniani..anasema..

“Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana”

Hii ikiwa na maana tunashindwa kujua wakati wa neema ni upi, na wakati wa hukumu za Mungu ni upi.. Sisi tupo tu hatujui majira yetu, tunadhani wakati wote, hii neema ya wokovu itaendelea kuwepo, tunadhani wakati wote, hali itakuwa kama ilivyo sasa hivi, utahubiriwa injili kama unavyohubiriwa sasa hivi..

Ndugu yangu, fahamu kuwa neema hii inakwenda kuisha siku sio nyingi, Dhiki kubwa ambayo haijawahi kutokea tangu dunia iumbwe na wala haitakaa iwepo itakwenda kutokea ulimwenguni kote..Dalili zote zinaonyesha, pengine katika wakati wetu huu tunaoishi tutayashuhudia hayo..Haya majira ya neema ndio yanaishia hivyo, muda huu tulionao ni wa nyongeza tu, dunia ingepaswa iwe imeshakwisha tangu zamani, lakini kwasababu tu ile nuru ndogo ya jioni ipo ndio maana unaona mambo bado yapo hivi..

Tumeshafikia wakati ambao Yesu hatuhubirii  tena injili ya kutuvuta kwenye wokovu, kama ilivyokuwa zamani bali anatuhubiria injili ya kuthibitisha ulichokiamini. Sikiliza anavyosema..

Ufunuo 22:10 “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.

11 Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.

12 Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo”.

Unaona, hiyo yote ni kwasababu ya unafki tulionao sasa, kwasababu kama tunaweza kuyatambua majira ya nchi, kwamba huu ni msimu wa masika na hivyo tunaanza kuyaandaa mashamba yetu kabla ya mvua kunyesha, au tunahama mabondeni mapema mafuriko yasitukute, inakuwaje basi, tunashindwa kuzitambua siku hizi kuwa ni siku za mwisho? Korona inakufundisha nini? Vimbunga vinakufundisha nini, Hili wimbi la manabii wa uongo unaloliona leo hii limezuka duniani kwa ghafla linakufundisha nini? . Bado tu huoni, hizo ni dalili za wazi kabisa ambazo zinatutambulisha kuwa tukio la unyakuo lipo karibu?

Yesu alisema..

Luka 12:54 “Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.

55 Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.

56 Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya”?

Itakuwa ni ajabu sana tukishindwa akili na akina koikoi. Tujitathimini sana, tuamke katika usingizi huu mzito, hukumu ya Mungu juu ya ulimwengu wote ipo karibu. Kama upo nje ya safina, anza safari upesi, mkimbilie Kristo kwa kumaanisha kabisa kwa moyo wako wote akuokoe, kwasababu hatuna muda mrefu hapa duniani,

 mbingu na nchi zitapita lakini maneno ya Bwana Yesu hayatapita milele.

Mbingu ipo,lakini pia kuzimu ipo, uchaguzi ni wa wako,

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

WAENDEE WANA WA ISAKARI, UWE SALAMA.

KWASABABU MUDA TULIOBAKIWA NAO SI MWINGI.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments