by Admin | 24 January 2022 08:46 am01
Tunguja ni aina ya mmea ambao haupatikani kirahisi, mmea huo una mizizi ambayo inakuwa na umbile kama la mtu.
Kutokana na maumbile hayo ya mizizi ya mmea huo, kufanana na maumbile ya mwili wa mwanadamu, watu wa zamani na hata wa sasa baadhi, huamini mmea huo unabeba nguvu fulani za kiungu.
Hivyo ulitumika na wachawi katika kazi za kichawi na wasio wachawi kwa matumizi mengine ya kiimani, kama leo watu wanavyotumia mti wa muarobaini kwa matumizi mbalimbali.
Katika biblia tunamsoma Raheli, ambaye wakati fulani aliamini mizizi ya mmea huo inaweza kumpatia mtoto siku za mbeleni.
Hivyo wakati fulani Rubeni mtoto wa dada yake alipokuwa shambani aliuona mmea huo (Mtunguja). Na kuuchimbua mizizi yake, na kwenda kumpatia mama yake (Lea).
Lakini Raheli (ambaye hakuwa na mtoto) alipoona kuwa Rubeni mtoto wa dada yake kamletea mama yake tunguja ambazo alikuwa anazihitaji sana, ili zimsaidie kupata mtoto, alikwenda kumwomba dada yake baadhi ya hizo, ili zimsaidie kupata uzao.
Lakini dada yake alikataa kumpa, lakini akamwambia kama anazitaka, basi amwuzie haki ya Yakobo kulala kwake siku hiyo badala ya kulala na Raheli.(Kwasababu ilikuwa ni zamu ya Yakobo kulala kwa Raheli siku hiyo na si kwa Lea). Yakobo alikuwa anaenda kwao kwa zamu.
Na kwasababu Raheli ana uchu wa kupata mtoto, akahamisha tumaini lake lote kwa Mungu na kulipeleka kwenye zile Tunguja, kwamba ndio zitamsaidia kupata mtoto.
Hivyo akauza haki yake ya kukutana na Yakobo siku hiyo, na kumpa dada yake, na yeye kuchukua zile tunguja.(Aliuza haki yake hiyo kama vile Esau alivyouza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa Yakobo ndugu yake kwasababu ya chakula kimoja tu).
Na matokeo ya Raheli kufanya vile hayakuwa mazuri, kwani badala ya yeye kupata mtoto, dada yake akapata watoto wengine watatu zaidi.
Tusome,
Mwanzo 30:14 “Reubeni akaenda siku za mavuno ya ngano akaona tunguja kondeni, akazileta kwa Lea mamaye. Ndipo Raheli akamwambia Lea, Nipe mimi baadhi ya tunguja za mwanao.
15 Naye akamwambia, Je! Ni jambo dogo kuninyang’anya mume wangu; hata wataka kuzitwaa tunguja za mwanangu pia? Raheli akamwambia, Kwa hiyo atalala kwako usiku huu kwa tunguja za mwanao.
16 Yakobo akaja kutoka kondeni jioni, Lea akatoka kumlaki, akasema, Lazima uje kwangu, kwa sababu nimekuajiri, kwa tunguja za mwanangu; akalala kwake usiku ule.
17 akamsikia Lea, naye akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana wa tano.
18 Lea akasema, Mungu amenipa ujira wangu, kwa sababu nimempa mume wangu mjakazi wangu. Akamwita jina lake Isakari.
19 Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa sita.
20 Lea akasema, Mungu amenipa mahari njema, sasa mume wangu atakaa nami, kwa kuwa nimemzalia wana sita. Akamwita jina lake Zabuloni.
21 Baadaye akazaa binti, akamwita jina lake Dina”
Hiyo inatufundisha nini?
Siku zote ahadi za Mungu ni thabiti, akisema au akiahidi basi atatimiza alichokisema.
Lakini uvumilivu unapotushinda na kuamua kutafuta njia nyingine mbadala ya kulazimisha kupata jambo ambalo tayari Mungu alishatuahidi na kutuambia tungoje, basi tunajipoteza wenyewe au ndio tunavyozidi kukikawisha kile kitu kufika.(www wingulamashahidi org).
Siku ile Yakobo alipotoka shambani pengine ndio ilikuwa siku ya Raheli kupata ujauzito, lakini shetani alimshawishi na kuhamisha imani yake kwenda kwenye mimea inayotumika na wapagani, na mwishowe Mungu akamsikia dada yake badala yake yeye, kama alivyomsikia Yakobo badala ya Esau, ikampelekea Raheli kusubiri tena miaka mingine mingi (na tunguja zake hizo hazimkusaidia chochote).
Mpaka Mungu alipomhurumia tena kupenda kumpa uzao (www.wingulamashahidi.org)
Hivyo na wewe dada/mama unayetafuta uzao sasa.. Bwana amekuahidi atakupa mwana, usianze kutanga tanga kwa waganga wa kienyeji, kuwa mvumilivu, subiri.. kwasababu kwa kutanga tanga, usidhani kwamba ndio utaharakisha uzao wako uje!..badala yake ndio utauchelewesha kabisa au hata kuupoteza.
Kadhalika na mambo mengine yote!, Ikiwemo mali na afya..hatuyapati kwa kufuata maagizo ya waganga wa kienyeji, au kupiga ramli, au kutambika Au tunguli..tutayapataa kwa sisi kuzishikilia ahadi za Mungu na kuziamini na kuziishi.
Bwana atubariki.
Maran atha!.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kwanini Raheli aliiba miungu ya Baba yake, (Labani) Mwanzo 31:19.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/01/24/tunguja-ni-nini-katika-biblia-mwanzo-3014/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.