YUKO WAPI MFALME WA WAYAHUDI?

YUKO WAPI MFALME WA WAYAHUDI?

Vipindi vya ukristo huwa vinabadilika, mambo hayawezi kubaki vilevile tangu siku ulipookoka hadi siku unakufa. Yapo majira utamwona Kristo waziwazi katika Maisha yako, yapo majira Kristo hutamwona kwa uwazi kama unavyodhani, hapo ndipo itakapokugharimu kumtafuta, ili umpate.

Hiyo ni kanuni Mungu aliyoiweka, ambayo kila mtu aliyempokea yeye hana budi kuifahamu. Kuna watu wanashindwa kulielewa hili, na ndio maana wanapofikia hatua ya kutomwona Kristo kiurahisi, kama ilivyokuwa zamani  wanaishia kurudi nyuma. Wakidhani kama hakuwa ni Mungu aliyewaita.

Embu tuitazame ile Habari ya mamajusi, wale watu walitokea nchi ya mbali sana huko Mashariki (Pengine nchi ya Babeli), lakini katika kutafuta tafuta kwao Habari za Mungu katika mambo yao ya anga, Mungu aliwapa neema ya kumwona Kristo katika njia hiyo.

Ndipo wakaiona nyota moja tofauti na nyingine iking’ara sana, na ghafla ile nyota ikaja kutua ulimwenguni, lakini haikutua sehemu nyingine yoyote Zaidi ya taifa la Israeli.. Ndipo wakaanza safari ya kuifuata.

Hivyo walipofika Israeli walitarajia kuwa wangeiona tena iwaelekeze mpaka eneo husika mtoto alipo, lakini hilo halikutokea, pengine wakatazama tena angani kwa umakini zaidi, lakini hawakuona chochote.. Hatujui ilipita muda gani wakiingojea itokee, lakini hakuna chochote kilichotokea, ndipo wakaanza kutafuta, kwa kuulizia Habari za Kristo kazaliwa awpi, wakafika mpaka wa Herode mfalme, kuulizia Habari hizo, ndipo wakapewa taarifa, kutoka kwa Herode  kuwa mfalme anazaliwa Bethelehemu ya uyahudi..

Sasa wakati wanakwenda Bethlehemu  ndipo ile nyota waliyokuwa wameipoteza wakaiona tena, katika nyumba aliyokuwa amelazwa mtoto, biblia inasema walipoiona walifurahi furaha kubwa mno,

Tusome..

Mathayo 2 :1 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema,

2 Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.

3 Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.

4 Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi?

5 Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii,

6 Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli.

7 Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota.

8 Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.

9 Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto.

10 Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno.

11 Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane.

12 Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine”.

Nachotaka uone ni kuwa, nyota ilionekana, ikapotea, ikaonekana tena..Lakini hawakukata tamaa na kusema turudi mashariki, tukaendelee na shughuli zetu, tuliona maruweruwe hapana, bali walimtafuta Kristo kwa bidii, na mwisho wa siku wakafika walipopakusudia.

Kipindi cha awali cha wokovu, ni rahisi kumwona Kristo katika kila hatua, lakini upo wakati atabadilisha mwonekano wake, atataka umtafute, atataka upate maarifa ya kutosha kuhusu yeye, hapo ndipo kunapokuja kujifunza kwa bidii, kuulizia Habari za wokovu, Habari za mbinguni, Habari za umilele, kuomba na kufunga, sio kukaa tu na kusema mimi nimeokoka Yesu ananipenda, halafu basi, hilo halipo katika safari ya wokovu.. Bwana ataruhusu hata wakati mwingine umtafute kutoka kwa maadui zake, kama vile mamajusi walivyotafuta taarifa kwa Herode adui wa Kristo.

Hivyo usiporudi nyuma, usipokata tamaa, ni uhakika kuwa mwisho wako utakuwa ni uzima wa milele. Hakuna mtu yeyote anayemtafuta Kristo kwa kumaanisha mwisho wake ukawa ni mbaya hakuna. Utamwona tu Kristo mwishoni. Utamfurahia kwa furaha kubwa, kuanzia hapa duniani hadi kule mbinguni.

Hivyo,  ikiwa upo katika hatua kama hii, usipunguze mwendo wako, kinyume chake ndio uzidishe kumtafuta Bwana kwa bidi kwasababu ndivyo unavyokaribia kukutana naye tena.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Zile tunu (Dhahabu, uvumba na manemane) Mamajusi walizozitoa kwa Bwana (Mathayo 2) . ziliwakilisha nini?

Raheli aliwalilia vipi watoto wake?

ALAMA ZA BENDERA YA ISRAELI ZINAWAKILISHA NINI?

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments